24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto, Kubenea kumnusuru CAG mahakamani


*Pia wapo wabunge Makamba, Komu na Bobali 

*Ujumbe wa Jumuiya ya Madola kutua kwa Spika

Na NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na wabunge wengine wanne wanatarajia kufungua kesi ya  katiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kumzuia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuitikia wito wa Spika wa Bunge.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Zitto kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) akimuomba kuingilia kati mgogoro unaoendelea baina ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na CAG, Profesa Mussa Assad.

Januari 9 mwaka huu Zitto alimuandikia barua Katibu Mkuu wa CPA, Akbar Khan, akimuarifu kuhusu hatua ya Spika Ndugai kumuagiza CAG aripoti kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kuhojiwa kwa madai ya kulidhalilisha Bunge.

Akizungumza jana, Zitto alisema wameona watu wengi wametoa maoni tofauti ndiyo maana wameona ni muhimu waende mahakamani kupata tafsiri ya  sheria.

Wabunge wengine ni Saed Kubenea (Ubungo), Salome Makamba (Viti Maalumu), Hamidu Bobali (Mchinga) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).

“Sisi wabunge watano kupitia wakili wetu Fatma Karume, tunaiomba mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kwa mujibu wa katiba, tafsiri ya sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge.

“Tumemwagiza wakili wetu kusajili kesi hii kwa hati ya dharura na tunaiomba mahakama itazame jambo hili kwa muktadha mpana kwa vile  ni kesi yenye masilahi makubwa kwa umma.

“Tukiacha CAG aitwe aende, madhara yake ni kwamba ipo siku pia jaji mkuu anaweza kuitwa mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa maoni yake kutokumpendeza Spika.

“Je, kutakuwa na uhuru wa mahakama?” alihoji Zitto.

Wabunge hao wanaiomba mahakama itoe tafsiri ya mamlaka ya Spika wa Bunge   kumuita mtu yeyote kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge bila azimio la bunge zima.

“Tunaiomba mahakama imzuie CAG kuitikia wito wa spika na kama akienda mbele ya kamati ya bunge tunaamini amevunja katiba na tutamshtaki,” alisema.

Pia wanaiomba mahakama imkataze spika kutekeleza wito wake kwa CAG kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Zitto alisema  wao hawamtetei Profesa Assad bali wanatetea heshima na uhuru wa ofisi ya CAG kwa sababu  wanaamini hatua hiyo ikiachwa itaweka msingi mbaya wa CAG kuingiliwa uhuru wake na taasisi mbalimbali kinyume na katiba.

“Bunge la Tanzania ni mdau na mteja wa ofisi ya CAG kwavile  hesabu zake hukaguliwa na CAG na hesabu za taifa zima, tukiruhusu kutomaswa tomaswa tunaweka hatarini hadhi na heshima ya ofisi ya CAG.

“Wakifanikiwa sasa watu wengine pia wanaokaguliwa wanaweza kuendelea kumtomasa tomasa CAG,  hivyo Watanzania wanapaswa kumlinda asitomaswe tomaswe.

“Mwaka 2011 bunge lilianza kumjadili CAG Utouh dhidi ya suala la Jairo (aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini).

“Nilisimama na kuliambia bunge halina mamlaka hayo na wala hakuitwa mbele ya kamati. Tumekubaliana ni lazima tulinde hadhi na ofisi ya CAG,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT – Wazalendo alisema kama kuna mtu analidharau bunge au kumvunjia heshima spika sheria inaelekeza jambo hilo lijadiliwe ndani ya bunge  apelekwe kwenye kamati ya maadili na si vinginevyo.

“Ndiyo maana nilisema Ndugai ninayemjua mimi anajua umuhimu wa ofisi ya CAG, hata kama angekuwa na hasira namna gani ni jambo ambalo lingeweza kuwa ‘settled’.

“Bunge na CAG wakiwa na uhusiano mbaya watakaoumia ni wananchi…Spika na Profesa Assad walipaswa kulimaliza jambo hili wenyewe,” alisema Zitto.

JUMUIYA YA MADOLA

Zitto alisema Umoja wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola umekubali kulifuatilia suala hilo kuhakikisha linaisha bila kuathiri uhuru wa  katiba na  sheria wa ofisi ya CAG.

“Jana (juzi) nilipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CPA ikiniarifu kuwa amelifikisha jambo hili kwa Mwenyekiti wa CPA na Spika wa Bunge la Cameroon, Emil Lifaka  aweze kushauriana na Spika wa Tanzania namna bora ya kushughulikia migongano kati ya Bunge na CAG.

“Nimetiwa moyo na hatua hiyo ya CPA kulifanyia kazi jambo hili kwa haraka na ni imani yangu Spika Ndugai atazingatia heshima aliyojijengea katika mabunge ya CPA,” alisema.

Alisema mwaka 2015 CAG wa Uganda, John Muwanga, alilisema bunge la nchi hiyo hadharani kwa kutofanya kazi sawasawa lakini Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga, hakuchukua hatua kama zilizochukuliwa na Spika Ndugai za kumpeleka akahojiwe kwenye bunge.

“Ndugai ni rafiki yangu   lakini rafiki mzuri ni yule anayekukosoa, sitaki aingie kwenye rekodi ya jumuiya ya madola kuwa spika wa kwanza kufanya tendo kama hili.

“CAG na bunge wanapaswa kufanya kazi pamoja na si kuwa na mgogoro kama huu,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles