23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

…Zitto ahoji zilipo bilioni 800/-

MAREGESI PAUL-DODOMA

KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ameitaka Serikali ionyeshe mahali zilipo Sh bilioni 800 ambazo hazikukaguliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha 2017/18.

Zitto aliyasema hayo mjini hapa jana, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akichambua ripoti ya CAG.

“Katika uchambuzi wetu wa mwaka jana, tulionyesha kwamba, asilimia sita ya fedha zilizokuwa zimekusanywa na Serikali, hazijulikani zilikokwenda na hizo zilikuwa ni shilingi trilioni 1.5 ambazo mjadala wake ulichukua mwaka mzima.

“Hoja yetu hiyo, ilipeleka kufanyika kwa uhakiki maalum wa CAG na baadaye Serikali ikasema ilihamishia ikulu matumizi ya shilingi bilioni 976.

“Katika ukaguzi wa CAG wa bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo ni bajeti ya pili ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kwamba, katika bajeti ya shilingi trilioni 31.7 iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi trilioni 27.7 kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.

“Kwa maana hiyo, Serikali ilishindwa kukusanya shilingi trilioni nne, kama ilivyokuwa mwaka uliopita wa fedha. Hata hivyo, katika ripoti hiyo ya CAG, ameonyesha shilingi trilioni 26.9 tu ndizo zilizotolewa kutoka mfuko mkuu wa Serikali na kwenda kutumika.

“Kwa hiyo, shilingi bilioni 800 kati ya Sh trilioni 27.7 zilizokusanywa, hazijulikani zilipo na hazikutolewa kwa ukaguzi.

“Kwa hiyo, tunaomba Serikali ieleze mahali zilipokwenda fedha hizo kwa sababu ni fedha za wananchi,” alisema Zitto.

Pamoja na hayo, Zitto alionyesha kutoridhishwa na jinsi Serikali inavyotumia fedha za umma kwa kuwa katika mwaka huo wa fedha, CAG alionyesha kwamba Sh bilioni 678 zilizotakiwa kutumika katika mamlaka zingine za Serikali, zilichukuliwa na Serikali na kutumiwa katika matumizi mengine.

“Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18, imeonyesha bado Serikali inatumia fedha ambazo siyo zake kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya mwaka 2017/17.

“Yaani, kwa mwaka 2017/18, CAG ameonyesha jumla ya shilingi bilioni 678 zilizokusanywa na TRA kwa niaba ya taasisi nyingine kama REA, TRL, wadau wa korosho na taasisi zingine, hazikupelekwa kwenye taasisi hizo na badala yake zilipelekwa kwa Katibu Mkuu Hazina na wakati wa ukaguzi wa CAG, hazikuoneka kama sheria inavyotaka.

“Kwa hiyo, katika eneo hili, CAG anapendekeza Serikali iheshimu fedha za taasisi zingine. Pamoja na hayo, ripoti hiyo ya CAG imeeleza kuna shilingi trilioni 4.8 zimetumiwa na Serikali bila kupita kwenye mfuko mkuu wa Serikali, jambo ambalo ni ukiukwaji wa taraibu za matumizi ya fedha za umma,” alisema Zitto.

Akizungumzia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, Zitto alisema hali hiyo inasababisha kukua kwa deni la Taifa.

“Ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18, inaonyesha deni la Taifa limefikia shilingi trilioni 50 hadi kufikia Juni 2018 kutoka shilingi trilioni 46 za Juni 2017.

“CAG, ameeleza kwamba, kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni, kumechangia kuongezeka kwa deni hilo kwa asilimia 20 kwa mwaka wa fedha 2017/18.

“Pia, CAG anasema kuwa, sababu kuu zaidi ya kukua kwa deni la Taifa kunatokana na Serikali kuendelea kukopa zaidi kwani mwaka 2017/18, Serikali ilikopa mikopo ya ndani ya shilingi trilioni 5.7,” alisema Zitto.

Ili kukabiliana na mambo hayo, Zitto alisema chama chake kinawashauri wabunge watimize wajibu wao bungeni wa kuisimamia na kuishauri Serikali, Serikali itazame upya sera zake za uchumi na pia Serikali ieleze kwanini Sh trilioni 4.8 hazikupita katika mfuko mkuu wa Hazina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,631FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles