23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu amwita RC Iringa kujieleza

MWANDISHI WETU – Mbinga

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, kufika ofisini kwake jijini Dodoma kesho saa tano asubuhi ili kujieleza sababu za halmashauri kuzuia nguzo za umeme hadi zilipwe posho.

Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyoni wilayani hapa.

Katika sakata hilo, alisema Hapi anatakiwa kufika ofisini kwake akiwa ameambatana na wakuu wa wilaya na wakurugenzi na  wenyeviti wa halmashauri zote zinazozalisha nguzo za umeme katika mkoa huo.

Mbali na Hapi, pia alimtaka Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kuhudhuria kikao hicho.

“Waziri wa Tamisemi mwenye halmashauri, halmashauri zake za Mufindi na Iringa wamezuia nguzo zisitolewe eti wanataka posho, wanataka zilipiwe kodi,” alisema na kuongeza:

 “Nimewaagiza tarehe saba wote saa tano kamili waje ofisini kwangu Dodoma, waniambie kwanini wamezuia nguzo, wananchi wanasubiri umeme wao wamezuia nguzo, eti wanasubiri posho, wanaidai Serikali na wakati wenyewe ni Serikali, tutakutana ofisini.

“Waziri wa Tamisemi aambatane na wakuu wa wilaya zenye halmashauri zote zinazozuia, wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi wa halmashauri hizo na RC wa Iringa na Waziri wa Nishati.

“Nataka nisikie kwanini wanazuia, wananchi wanasubiri umeme na sisi tunasubiri umeme uwake kila nyumba ya Mtanzania, hata ya yule mnyonge, halafu wanazuia nguzo tena kwenye nchi hii tuliyoipata wenyewe.”

Majaliwa alichukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliolalamikia kutofikishiwa huduma ya umeme katika maeneo yao kutokana na kukosekana kwa nguzo zilizozuiwa kwa sababu ya wahusika kuidai Serikali posho.

Pia alisema Serikali imedhamiria kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini vikiwamo vya wananchi hao watakaounganishiwa huduma hiyo kwa gharama ya Sh 27,000.

Alisema Serikali imeondoa gharama za kulipia nguzo na fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu tayari zimeshabebwa na Serikali na kwa vijiji ambavyo viko katika maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola hivyo kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi kwa wananchi na taifa.

 Majaliwa alisema Serikali imefanya uamuzi huo kwa sababu huduma ya umeme ni muhimu.

Katika hatua nyingine, alibaini mazingira ya ufisadi katika mradi wa ukarabati wa jengo la mama na mtoto  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.

Alisema hajaridhishwa na kiasi cha Sh milioni 129 zilizotumika na alimwagiza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile afuatilie suala hilo ili kumbaini aliyehusika kupitisha zabuni ya ukarabati wa jengo hilo na kisha kumpelekea taarifa.

 “Sijaridhishwa na gharama za ukarabati wa jengo hilo kutokana na kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika.

“Serikali inajenga vituo vya afya vyenye jengo la maabara, jengo la kujifungulia, wodi ya mama na mtoto, chumba cha upasuaji, nyumba ya watumishi kwa gharama za shilingi milioni 400 hadi 500 sasa inawezekajane jengo moja linalokarabatiwa ligharimu kiasi hicho?” alihoji Majaliwa.

Pia aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu utoaji wa huduma ya watoto walio chini ya miaka mitano kwa sababu baadhi ya wahudumu wa afya wamekuwa wakiwatoza gharama za dawa wakati wanatakiwa watibiwe bure.

Majaliwa alitoa maelekezo hayo baada ya mwananchi mmoja, Kanisia Fusi ambaye amelazwa na mtoto wake katika hospitali hiyo, kumweleza kwamba ameandikiwa dawa wakati mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu anatakiwa atibiwe bure.

Pia alizindua mpango wa usambazaji wa x-ray za kidigitali katika hospitali mbalimbali za rufaa ili kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mionzi.

Alisema kwa kuanzia x-ray hizo zitasambazwa katika hospitali za rufani kwenye mikoa 11 na kisha baadaye zitasambazwa katika hospitali nyingine 20.

Kwa upande wake, Ndungulile alisema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika kuboresha huduma za afya nchini.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wote karibu na maeneo yao ya makazi tena kwa gharama nafuu.

 “Katika kufikia azma hii, mojawapo ya kipaumbele ni kununua vifaa vya kisasa vinavyoendana na teknolojia iliyopo,” alisema.

Pia alisema kwa sasa wizara hiyo imenunua mashine 11 za x-ray za kidigitali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni zilizokusudiwa kupelekwa katika hospitali 11 zenye x-ray za zamani.

Alizitaja hospitali hizo kuwa ni Amana, Bukoba, Katavi, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Singida na nyingine tatu zitafungwa Chato, Magu na Nzega.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles