27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu akagua ujenzi mji wa Serikali

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa eneo la mji wa Serikali lililoko Ihumwa na kubaini baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi inayotarajiwa.

Majaliwa aliamua kuitisha kikao cha mawaziri na makatibu wakuu wote leo saa 5 asubuhi ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini.

Alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za wizara zote pamoja na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Mtumba lililoko kilometa 17 kutoka jijini hapa.

“Nimekagua maeneo yote na kukuta baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo ya wizara nne hadi tano. Sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao cha mawaziri wote kesho (leo) ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu hii kazi.

“Nimebaini kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto, nondo, matofali na kikao cha kesho (leo), kitahusisha mawaziri, makatibu wakuu, viongozi wa mkoa na Jiji la Dodoma pamoja na wakandarasi wote ili tukubaliane kazi hii inaisha lini,” alisema.

Akitoa mfano, Majaliwa alisema wajasiriamali wanaotengeneza matofali Dodoma wako wengi, lakini matofali yao yako chini ya kiwango, kwahiyo wanatakiwa watu wa kutengeneza matofali mengi yenye uimara.

“Tuna ujenzi wa wizara 24, tunataka matofali imara siyo yale ambayo ukilishika tu mchanga unamomonyoka,” alisisitiza.

Akisisitiza uharaka wa kazi hiyo, alisema ina malengo maalumu na inatakiwa ikamilike haraka sana.

“Tarehe ya mwisho ya kukamilisha ujenzi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais ilikuwa Desemba 31, mwaka huu lakini kuna sababu zimetajwa kukwamisha ujenzi huo zikiwemo mvua na uhaba wa kokoto,” alisema.

Hata hivyo, alipongeza kazi iliyofanywa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Utumishi, Ujenzi, Katiba na Sheria, Maji na Elimu.

Kazi hizo zimefanywa na wakandarasi ambao ni Magereza, SUMA JKT, Wakala wa Majengo (TBA) na vikosi vya ujenzi vya Mwanza na Dar es Salaam vilivyoko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Wakandarasi walioboronga ni JWTZ – Mzinga, National Housing na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Majaliwa alimwagiza Katibu wa kamati ya kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Meshack Bandawe ahakakishe anapokea taarifa kutoka kila taasisi inayohusika na ujenzi huko Ihumwa na akishaijumuisha, aiwasilishe kwake ifikapo leo jioni.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ashirikiane na mkurugenzi mwenzake wa Chamwino kuhakikisha vijana wengi wanapata fursa za ajira kwenye mradi huo.

“Mkurugenzi wa Jiji wasiliana na Mkurugenzi mwenzako wa Chamwino mhakikishe vijana na akina mama wanakuja kufanya kazi hapa.

“Pia itisha kikao cha waandishi wa habari uwaeleze wananchi wako fursa zilizopo, kuanzia ufyatuaji wa matofali, uuzaji wa nondo, kokoto na utengenezaji wa pavement blocks, hizi zote ni fursa, tuna wizara 24 na mahitaji ni makubwa,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles