28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wataka ubunge kwa rushwa CCM waonywa

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Queen Mlozi, amewatahadharisha wanachama wanaojiandaa kuwania uongozi katika nafasi mbalimbali kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Amesema zama za uchaguzi wa 2015 na za uchaguzi ujao ni vitu viwili tofauti na kwamba watahakikisha wanafuta dhana iliyojengeka, kwamba umoja huo ni wa watu fulani tu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA jana, Mlozi alisema wameanza kupambana na watu wanaotumia rushwa kuhakikisha hawapati nafasi katika uongozi.

Mlozi alikuwa akizungumza baada ya kufanya ziara katika ofisi za magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, kujionea jinsi inavyofanya kazi zake.

“Tunapambana kweli kweli kuhakikisha rushwa inatokomezwa, kwanini kiongozi ununue uongozi? Uongozi ni madaraka yanayotoka juu…unayanunua ili uwatumie kitu ambacho tunakipiga vita,” alisema Mlozi.

Katika kudhihirisha hilo, alisema hata katika chaguzi ndogo walipambana na watu waliojaribu kutoa rushwa kwa kuhakikisha majina yao hayarudi.

“Chaguzi za marudio aliyethubutu kutoa rushwa jina lake lilikatwa, kiongozi hanunuliwi kwa fedha, hivyo usithubutu kutoa kwa sababu utakamatwa tu au unaweza kukuta jina lako halipo,” alisema.

Aliwataka wanachama wa umoja huo kufuta dhana iliyojengeka kwa muda mrefu, kwamba jumuiya hiyo iko kwa ajili ya watu fulani bali ni ya watu wote na hivi sasa wanahakikisha wanamfikia hadi mwanamke wa chini.

Kuhusu viti maalumu, alisema vitaendelea kuwepo kwa sababu vinasaidia kuweka uwiano kijinsia na kuwafanya wanawake wawepo katika ngazi za uamuzi.

“Upo umuhimu mkubwa na usiotiliwa shaka kwamba ni lazima tuwe na viti maalumu, vinatusaidia kuweka uwiano wa 50/50 bungeni. Vimewekwa kwa makusudi kuwafanya wanawake wawepo katika ngazi za maamuzi.

“Cha msingi tupokezane vijiti kwa mujibu wa katiba, lakini kuviondoa tutakuwa hatujamtendea haki mwanamke,” alisema.

Alisema kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao, wameanza kuwajengea uwezo wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwahamasisha wajitokeze kugombea nafasi za uongozi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wamekuwa wakifanya makongamano ya wanawake katika maeneo mbalimbali hasa ya vijijini kwa lengo la kuwawezesha wajitambue na kuvunja mfumo dume uliokuwa umezoeleka kwa miaka mingi.

“Tarehe 24 mwezi uliopita nilikwenda Kijiji cha Mondorara kilichopo wilayani Longido, nilikuta mwenyekiti wa kijiji na makamu mwenyekiti wa halmashauri ni wanawake wa jamii ya kimasai. Wameelimishwa na sasa wameanza kuondoa mfumo dume.

“Hata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tunajitahidi sana kuwahamasisha wanawake wagombee na naamini tunao uwezo mkubwa kuliko wanaume, lakini jambo linaloturudisha nyuma ni kutojiamini.

“Tumewaeleza viongozi wawahamasishe wanawake wenye uwezo wagombee, tukiwa wengi itatusaidia hata katika uchaguzi wa 2020 wanawake wengi watapata nafasi,” alisema.

 Pamoja na hayo, Mlozi alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ikiwamo kuwapelekea huduma za maendeleo ikiwamo kupeleka maji na umeme vijijini.

Alisema hatua hiyo inakwenda kuakisi kwa vitendo kazi inayofanywa na Serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli ya kuleta maendeleo kwa taifa na watu wake.

“Leo nchi haikuwa na ndege hata moja, lakini sasa tumenunua ndege sita, ni zetu zilizotokana na fedha za walipakodi kama njia ya matunda yao.

“Nilikuwa Tabora, ili uweze kuja Dar es Salaam kwa wakati ule ulilazimika kulipa hadi shilingi milioni moja uende hadi Kigoma kuja Dar.

“Lakini sasa ukiwa na Sh 250,000 unasafiri vizuri kwa usalama na uhakika kutokana na kuwapo kwa ndege zetu za ATCL. Na si hilo tu bado hata sekta ya mawasiliano ya barabara hivi sasa kila Mtanzania ni shahidi kwa kazi inayofanywa na Serikali.

“Kwetu sisi wanawake tunajivunia, Rais Magufuli ni kiongozi aliyejipambanua kumsaidia mwanamke wa Tanzania ikiwamo kutua ndoo kichwani,” alisema Mlozi.

Katika ziara hiyo Mlonzi alitembelea idara mbalimbali zilizoko katika Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na kufurahishwa na namna inavyozingatia dhana ya usawa wa kijinsia.

“Nimefurahi tumejifunza nini kinachofanyika katika magazeti ya New Habari na kila nilikopita nimekuta kuna wanawake viongozi na sehemu zingine wako hadi watatu, hii inaonyesha ni kwa namna gani mnazingatia dhana ya usawa kijinsia,” alisema Mlozi.

Alisema wataendelea na ziara hiyo katika vyombo vingine vya habari kwa lengo la kutengeneza wigo mpana na kuwa na mahusiano ya karibu kati ya vyombo hivyo na jumuiya hiyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa UWT, Jesca Mbogo alisema; “Haiwezi kuwa UWT kama hakuna vyombo vya habari au watu wanaoitangaza jumuiya na kazi zake, hivyo tunaomba ushirikiano wenu ili kuwa na umoja katika kufanya kazi za jumuiya na kukitangaza chama.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles