25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

‘Watachakaa’ ya RPC Muruto yawayeyusha ACT

*Wasitisha maandamano ya CAG, ripoti kutinga bungeni bado kizungumkuti

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kuonya maandamano ya Chama cha ACT-Wazalendo na kwamba watakaoingia barabarani kuandamana watachakazwa, chama hicho kimetangaza kuyaahirisha.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho, Licapo Licapo, ilieleza kwamba wamepokea kwa masikitiko kile walichoita hamaki kubwa ya taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kuhusu kusitisha maandamano yao ya amani.

Licapo alisema kuwa ngome hiyo ya vijana imeazimia kuyasogeza mbele maandamano hayo na kuamua kushughulika na hoja namba mbili iliyotolewa na Jeshi la Polisi na kisha kuyarudisha tena kwa siku nyingine, hasa endapo taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haitojadiliwa bungeni na pia Bunge kutoondoa azimio lake la kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad.

 “Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT-Wazalendo kwa niaba ya mabaraza, jumuiya na ngome za vijana wa vyama vya NCCR-Mageuzi, CHAUMA, UPDP tumepokea kwa masikitiko na hamaki kubwa taarifa ya polisi kuhusu maandamano yetu.

“Kwa vijana wa ACT-Wazalendo na ushirikiano wa vyama vingine vya upinzani ambao walikuwa wameshafika Dodoma, tunawaomba wawasiliane na kamati yetu ya uratibu iliyokuwa ikiendesha zoezi hili kwa maelekezo zaidi ya namna wale waliotoka mikoa ya jirani kurudi katika mikoa yao.

“Ngome ya Vijana wa ACT-Wazalendo bado inaendelea kufuatilia, taasisi na asasi zingine ambazo nazo zimeamua kulichukulia swala la CAG kwa uzito na tuko tayari wakati wowote kushirikiana na yeyote ambaye yupo tayari kusimamia haki, utawala wa sheria na kupinga uvunjivu wa katiba,” alisema Licapo katika taarifa yake.

Alitoa wito kwa Spika wa Bunge na wabunge watafakari tena azimio lao la kutofanya kazi na CAG kwa mapana na marefu na wasitishe ili kulinda katika ambayo wameapa kuyalinda.

Maandamano hayo yalikuwa yanaratibiwa na ngome ya vijana ya chama hicho yakiwa na lengo la kushinikiza Bunge kufuta azimio lake la kutokufanya kazi na CAG, Profesa Assad.

Hata hivyo juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alitoka hadharani na kuonya kuwa hatua kali zingechukuliwa kwa yeyote ambaye angeingia mtaani kuandamana.

Alisema zipo taarifa zinasambaa katika mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya vyama vya upinzani ikiwamo ACT-Wazalendo wamepanga kufanya maandamano jana kushinikiza Bunge kubadili uamuzi wake wa kutofanya kazi na CAG Profesa Assad.

Kamanda Muroto alisema wapo wengine wamepanga kusafiri kwenda Dodoma kufanya maandamano hayo, huku akiwataka kuacha mara moja kwani wataambulia kipigo kikali.

“Niwatake wale wote waliopanga kufanya maandamano Aprili 9, 2019 kusitisha maandamano yao haramu, wasije kuingia barabarani maana watapigwa vibaya,” alisema Muroto.

Alisema kazi za Bunge zinahojiwa ndani ya Bunge na si nje ya Bunge, hivyo aliwataka wananchi wa Dodoma kuendelea na kazi zao kama kawaida kwani hakuna maandamano yoyote yatakayofanyika.

RIPOTI YA CAG

Wakati hayo yakiendelea, hadi sasa bado giza limetanda kuhusu hatua ya Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya CAG kama katiba inavyoelekeza.

Hatua hiyo ilimfanya juzi Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) kuhoji hatua hiyo ya Serikali huku akidai kutofanya hivyo ni kinyume na katiba.

Mnyika alitumia kifungu cha 143 (4) cha Katiba ya Tanzania kuomba mwongozo, ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama walimtaka kusoma vyema sheria na tafsiri ya sheria ili kuelewa kwa kina muda wa uwasilishwaji wa taarifa hiyo bungeni.

Ibara ya 143 (4) inasema; “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atawasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hii. Baada ya kupokea taarifa hiyo Rais atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha kwanza cha Bunge kitakachofanyika baada ya Rais kupokea taarifa hiyo na itabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.”

Machi 28, 2019 Rais alipokea ripoti za ukaguzi kutoka kwa CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2018, na kikao cha kwanza cha Bunge kilianza Aprili 2, mwaka huu na hadi sasa taarifa hiyo hajawasilishwa bungeni.

Wakati Mnyika akiomba mwongozo huo, Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhagama alisimama na kuomba mwongozo, akitoa ufafanuzi kuhusu hoja ya Mnyika.

“Mnyika wakati akiomba mwongozo ameonyesha kujua kuitafsiri katiba na kunukuu vifungu vya sheria ya CAG, lakini hakwenda mbali zaidi na kusoma sheria nyingine ambazo zinaambatana na maagizo hayo ya kikatiba na kisheria katika kufanya tafsiri ya siku ambazo zimeandikwa katika katiba na sheria zinazohusika na uwasilishwaji wa ripoti ya CAG na hasa sheria ya tafsiri za sheria na hivyo kuonyesha wazi kuwa Serikali haitaki kuwajibika ama haijawajibika,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles