23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaoanza kidato cha kwanza watakiwa kwenda na meza, kiti


LILIAN JUSTICE-MOROGORO

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kayombe Lyoba amewaagiza wazazi na walezi wenye watoto wanaotarajia kujiunga kidato cha kwanza  mwaka huu kuhakikisha wanakwenda na kiti  na meza ili waweze kuingia darasani.

Hali hiyo imekuja baada ya halmashauri hiyo kuongeza kasi kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kila mwanafunzi aliyechaguliwa kuingia kidato cha  kwanza  apate fursa ya kuanza masomo. 

“Tunawaomba wazazi na walezi wawezeshe watoto wao kuja na kiti na meza pindi wanapokuja kuanza masomo Januari 7, kwani tayari tumeshaongeza jitihada kuhakikisha vyumba vya madarasa vinakuwepo vya kutosha ili asikose kuingia mwanafunzi hata mmoja,” alisema  Lyoba.

Alisema jumla ya wanafunzi 4,136 wamepokewa na halmashauri iwemeweza kujenga vyumba vya madarasa 87 na kubakiwa na upungufu wa vyumba 32.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema mbali na jitihada za kujenga maabara katika shule zao kuna changamoto ya uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi.

“Halmashauri yetu ina upungufu wa walimu 41 wa kufundisha masomo ya sayansi, hivyo tunamwagiza Ofisa Elimu Sekondari kulifuatilia suala hilo kwa ukaribu ili tuweze kuondokana na changamoto hiyo,” alisisitiza Kingo.

Aidha Ofisa Elimu Sekondari, Hatujuani Ally alisema Serikali ndiyo inayopanga walimu na hadi sasa imeweza kuleta walimu wa sayansi katika Shule ya Sekondari Nelson Mandela, Matombo, Kibogwa na Mvuha na matarajio ni kuongeza walimu wengi zaidi kwenye shule ambazo zina uhitaji mkubwa.

Ally aliongeza kwamba Wilaya ya Morogoro kwa sasa ina jumla ya walimu wa kufundisha masomo ya sayansi 42 huku mahitaji yakiwa ni walimu 83 katika shule 28 zilizopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles