28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wote Tusiime wafaulu kwenda kidato cha tano

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WANAFUNZI wote 272 wa Shule ya Sekondari ya Tusiime ya Tabata, Dar es Salaam waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana wamefaulu kwenda kidato cha tano huku 204 kati yao wakipata daraja la kwanza na la pili.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), wanafunzi 86 wa shule hiyo wamepata daraja la kwanza na 118 daraja la pili.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wengine 60 wamepata daraja la tatu, wanane wamepata daraja la nne lakini wote wamefanikiwa kupata alama za kuendelea na kidato cha tano.

Mkuu wa Taaluma shuleni hapo, John Kishefu, alisema matokeo hayo ni mazuri hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa nao ambayo ni kubwa kuliko shule nyingi zilizofanya mtihani huo.

Kishefu alisema miaka yote Tusiime huwa haichagui wanafunzi wa vipaji maalumu kama zinavyofanya baadhi ya shule bali huchukua wa aina zote hata wale wenye uwezo mkubwa na mdogo darasani na kuwaandaa vizuri.

“Sisi hatuchagui mwanafunzi, unaweza kukuta amekuja hapa akiwa na uwezo mdogo lakini timu mahiri ya walimu waliopo hapa wanamtengeneza hadi anapata daraja la kwanza au la pili, hilo ni jambo la kawaida hapa Tusiime,” alisema.

Kishefu alisema matokeo hayo mazuri ni mwendelezo ya matokeo kama hayo kwa shule za Tusiime kuanzia shule ya msingi na kidato cha pili na wamekuwa wakifaulisha kwa alama za juu.

Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi wa shule hizo, Albert Katagira, alisema ni mazuri na yanatokana na dhamira waliyonayo kama taasisi kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata elimu bora katika mazingira yaliyo safi na salama.

“Napenda kuwathibitishia wadau wote wa elimu kuwa shule za Tusiime zimejipanga kuendelea kutoa elimu bora hapa nchini na hivyo tumewekeza vya kutosha katika miundombinu, zana za kufundishia, motisha kwa wafanyakazi na ushirikiano mzuri baina yetu, Serikali na wazazi, haya yote kwa pamoja ndiyo yametufikisha kwenye matokeo haya,” alisema.

Alisema shule hizo zimejipanga kuendelea kufanya vizuri kwa kuimarisha mifumo ya utoaji wa elimu na huduma katika shule hizo ili kuwajengea watoto uwezo na kuwapa maarifa stahiki na aliwataka wazazi waendelee kuwaamini na kuwapa ushirikiano katika azma yao ya kutoa elimu bora kwa vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles