27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 2,600 Mwanza wasoma kwa zamu

BENJAMIN MASESE-MWANZA

WANAFUNZI 2,615 wa Shule ya Msingi Kanindo iliyopo Kata ya Kishili wanalazimika kusoma kwa zamu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi mawili ya wanafunzi 1,302 (darasa la pili, nne na sita) na wanafunzi 1,313 (darasa la awali, kwanza, tatu, tano na saba).

Akizungumza katika kikao cha kamati ya shule kilichowahusisha wazazi na uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kanindo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Joseph Mhuli, alisema mazingira si rafiki kwa walimu na wanafunzi.

“Mgeni akipita anaweza kudhani wanafunzi wapo mapumziko kumbe sivyo, tunalazimika kuwatoa nje ili wengine waingie darasani.  

“Mfano darasa la tano lina wanafunzi 217 wote wanaingia pamoja darasani, hebu fikiria wanakaaje, hewa haitoshi pia dawati moja wanakaa wanne na wengine wanalazimika kukaa chini mwalimu akifundisha anapita juu ya miguu ya wanafunzi,” alisema Mhuli.

Alisema matundu ya vyoo yaliyopo ni sita na kusababisha wanafunzi wengine kujisaidia nje.

“Naomba uongozi wa mtaa muone umuhimu wa kujenga hata madarasa mawili au matatu, tunashukuru kamati ya shule imejitolea kujenga ofisi ya walimu kwa fedha zao na tunasubiri Serikali kuezeka,”alisema.

Naye Mtendaji wa Mtaa wa Kanindo, Petro Mashili na Mwenyekiti wa mtaa huo, Ndalahwa Masibuka, waliwataka wananchi kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa haraka.

Katika mkutano huo, wananchi waliazimia kila kaya kuchanga Sh 3,000 au kutoa matofali matatu ambayo yanapaswa kuwasilishwa shuleni ambapo mwisho ni Februari 30, mwaka huu ili ujenzi uanze Machi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alisema kazi ya kujenga vyumba vya madarasa ni jukumu la wananchi, ispokuwa kuezeka.

Alisema ana shule nyingi zinazohitaji kuezekewa hivyo hawezi kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa maboma.

Mdau wa elimu na mkazi wa Kanindo, Mussa Maziku, aliahidi kujenga darasa moja na tayari amewasilisha matofali 300 shuleni hapo.

Awali Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM), alichangia mifuko 30 ya saruji ili kujenga matundu ya vyoo na kuwataka wazazi kuchangia ujenzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles