22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Vurugu zaibuka mpaka wa Tanzania, Kenya

ELIYA MBONEA-ARUSHA

WAKAZI katika eneo la mpaka wa Kenya na Tanzania wa Namanga upande wa Kenya, wamezuia magari kuingia nchini kwao kwa kile walichodai kutekwa kwa mfanyabiashara wa kubadili fedha za kigeni.

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo raia wa Kenya aliyetajwa kwa jina moja la Moha, linadaiwa kutokea juzi saa 3 usiku.

Wananchi hao wa Kenya walikuwa wakishinikiza kuachiwa kwa mfanyabiashara huyo.

Katika vurugu hizo ambazo ziliendelea hadi jana, wakazi wa upande wa Kenya walichoma matairi barabarani na kuzuia magari kutoka Namanga jambo ambalo linadaiwa kuathiri shughuli za mwingiliano wa kibiashara kati ya Tanzania na Kenya.

Kuibuka kwa vurugu hizo kulisababisha shughuli za kibiashara kusimama siku nzima, hatua iliyofanya wafanyabiashara kupoteza muda na mali kuharibika.

Akizungumzia tukio hilo jana, Meneja Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka wa Namanga, Godfrey Kitundu, alisema vurugu zimeathiri mwingiliano wa biashara kwa nchi hizo na nyingine.

“Magari hayawezi kuingia Tanzania wala kutoka Kenya, vurugu hizi zitashusha mapato kwa asilimia fulani.

“Tukio hili limesababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuendelea na shughuli zao za kawaida za kuwaingizia kipato,” alisema Kitundu.

Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Frank Mwaisumbe, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo hasa kwa upande wa Kenya.

“Kwetu Namanga-Tanzania hakuna athari za kibindamu zilizotokea kutokana na vurugu hizo, zaidi ya wafanyabiashara kuzuiwa kuingia nchini Kenya.

“Tunaendelea na majadiliano na viongozi upande wa Kenya kuangalia namna sahihi ya kutatua vurugu hizi,” alisema Mwaisumbe.

Aliwataka wakazi wa mji wa Namanga kuwa watulivu kwani sasa Serikali imeanza uchunguzi wa suala hilo na kuweza kuwabaini wahusika.

“Hakuna haja ya kufanya vurugu kwani tunachunguza tukio hili kwa kina ili kuweza kubaini ni watu gani wamehusika na ninawaomba wananchi watuamini viongozi wao,” alisema.

Mwaisumbe alisema wananchi wachache hawawezi kuzuia shughuli za mpakani kwa kuzuia magari ya Tanzania kuingia Kenya.

“Kitendo cha kuzuia magari kwa kuchoma matairi ni kuvunja sheria na tumelazimika kutumia vyombo vya dola kudhibiti vurugu,” alisema.

Mwaisumbe aliwataka wakazi wa eneo hilo la mpakani kuheshimu sheria na taratibu ili kutoingia katika migogoro na vyombo vya dola.

Alisema katika vurugu hizo hadi kufikia jana mchana hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Kwa upande wake, mkazi wa Namanga upande wa Tanzania, Simon Ledupa alisema Namanga ni mpaka mkubwa na kuna watu wengi kutoka mataifa mbalimbali wanapita hapo, hivyo huyo mtu wanayedai ametekwa na Watanzania inawezekana yupo ndani ya Kenya.

 “Huyu Moha anayedaiwa kutekwa upande wa Tanzania si kweli, yupo huko upande wao. Wanapodai alichukukiwa na gari yenye namba ya Tanzania sidhani kama ni sahihi.

“Mpakani kuna biashara za magendo nyingi, watu wanatumia namba za kila nchi kufanya uhalifu,” alisema Ledupa.

Mkazi huyo aliweka wazi kwamba vurugu hizo zinaweza kuwa zimesababishwa na vitendo vya wivu miongoni mwa wafanyabiashara wa kubadilishia fedha upande wa Kenya.

Alisema wanapotuhumu gari yenye namba ya Tanzania wanakosea kwa kuwa mpakani biashara za magendo ni nyingi na watu kutumia namba za nchi kwa nchi kwa biashara haramu ipo katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Naye mkazi wa Namanga, upande wa Kenya, Odinga Nguduu alidai juzi saa 3 usiku lilifika gari lenye namba za Tanzania kwenye ofisi ya mfanyabiashara Moha na kumchukua kisha kuelekea upande wa Namanga ya Tanzania.

Nguduu ambaye ni mkazi wa Kenya alidai kwamba tangu Moha alipochukuliwa hajarudishwa na ndipo zilipoanza vurugu za kushinikiza aachiwe.

“Akirudishwa Moha wetu tutaacha vurugu hizi na kuruhusu magari kuendelea na shughuli zao,” alisema Nguduu.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, lakini simu yake iliita bila kupokewa.

Lakini taarifa za ndani ya Jeshi la Polisi zilieleza kuwa Kamanda Shana alikuwa njiani kuelekea Namanga kufuatilia kwa kina kiini cha mgogoro huo.

“Kwa sasa kamanda hayupo kwani muda huu nahisi yupo njiani ameelekea Namanga kujua ukweli, lakini kama akiwahi kurudi atatoa taarifa kwa umma, kama si leo hata keshi,” alisema mmoja wa wasaidizi wa Kamanda Shana ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini kwa kuwa si msemaji wa Jeshi la Polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles