20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Viporo vya Simba vyamtesa Zahera

DAMIAN MASYENENE-MWANZA

VIPORO vya watani wao wa jadi, Simba kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, vinazidi kumuumiza Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye haridhishwi na upangaji wa ratiba hasa inayohusu michezo ya timu yake.

Licha ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, bado kocha huyo anaamini wachezaji wake hawako sawa kimwili ndiyo sababu kubwa ushindi wao umekuwa wa taabu na umakini katika ufungaji haupo.

Zahera alisema anashtushwa sana na wingi wa viporo walivyonavyo Simba wakati timu yake ikifululiza kucheza na kusafiri, jambo ambalo halikubaliki na duniani kote hajalishuhudia.

“Tatizo kubwa ni namna wanavyopanga mechi zetu, iko shida kubwa sana wachezaji wangu wanachoka, mbanano huu wa ratiba inakuwa ngumu kuandaa programu za mazoezi hasa ya kukimbia…utamkimbiza nani na uchovu wote huo wa safari.

“Tunabaki kucheza tu kwa morali tushinde, ushindi mwembamba tunaoupata unatosha kutokana na hali iliyopo, wachezaji wanakosa nafasi kwa sababu hakuna umakini mbele ya goli,” alisema.

Akizungumzia maandalizi dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo ujao, Zahera alisema hakutakuwa na mazoezi ya ziada kwa wachezaji wake, bali watapumzika kwa siku mbili wakifanyiwa tu mazoezi ya kusingwa mwili.

Katika hatua nyingine, Zahera alisema katika kipindi cha takribani mwaka mmoja aliochokaa nchini kuinoa Yanga, ameshuhudia soka la Tanzania na anaamini kwamba asilimia kubwa ya wachezaji waliopo nchini hususan Ligi Kuu Tanzania Bara ni wavivu wa mazoezi na hawana tabia za soka lililostaarabika.

Mkongomani huyo amejipambanua kwa kusimamia nidhamu ndani ya Yanga kutokana na maamuzi yake kadhaa ambayo amekuwa akiyachukua dhidi ya wachezaji wake akiwemo nahodha Ibrahim Ajibu, aliyekuwa mlinda mlango namba moja, Beno Kakolanya, aliyekuwa nahodha, Kelvin Yondani na wengine.

Zahera alitoa kauli hiyo juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon, ushindi ambao anaamini umekuwa si rahisi kutokana pia na timu yake kuwa inapata matokeo kwa bahati.

Zahera amewahi kukaririwa pia akisema kuwa timu yake inakosa ushindi na kufunga mabao mengi kutokana na kukosa wachezaji wenye kasi, mbio na wanaoweza kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwa haraka.

“Timu haina kasi, timu inapata ushindi mwembamba, kama mnavyojua problem (tatizo) iliyopo ni kwamba wachezaji wengi wa Tanzania tulionao kwenye klabu zetu hawako serious (makini) hasa kwenye mazoezi ni wavivu pia na hawana tabia za ki-profesionalism,” alisema.

Ushindi huo pia umezidi kuifanya Yanga ijichimbie kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 71 baada ya kucheza michezo 30.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles