26.2 C
Dar es Salaam
Friday, December 3, 2021

Viongozi wa dini wasikwepe majukumu yao

MARKUS MPANGALA

HIVI karibuni tumeshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli akikutana na kuzungumza na viongozi wa dini Ikulu jijini Dar es Salaam, kikao hicho kimetajwa kuwa ni kujenga uhusiano mwema baina ya viongozi hao na serikali ya awamu ya tano.

Rais Magufuli amefanya hivyo ikiwa ni njia ya kukutana na wadau wa sekta mbalimbali, kwa madhumuni ya kusikiliza ushauri na maoni yao kuhusiana na masuala ya uongozi wake na yanayogusa jamii kwa ujumla.

Ifahamike kuwa viongozi wa dini ni sehemu ya jamii zetu. Viongozi wa dini ndiyo walezi wa jamii yetu pia.

Mazungumzo hayo yameibua mjadala. Tuliona baadhi ya viongozi wakimuomba Rais Magufuli alegeze kidogo kwenye masuala ya demokrasia, kwamba awaache watu wapumue na wafanye mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali.

Baadhi yao wamelalamikia kushamiri michezo ya kubahatisha (kamari). Vilevile walilalamikia watu wanaovaa nusu utupu kuwa wamezidi kushamiri mitaani hali ambayo inachafua taswira ya jamii yetu.

Viongozi wa dini wameongelea masuala mengine ya uchumi, jamii na siasa,lakini kubwa zaidi ni ujenzi wa uhusiano mwema baina ya taasisi za serikali, umma, wadau,wawekezaji na kadhalika.

Tunawaheshimu viongozi kwakuwa wana umuhimu mkubwa katika maisha ya wananchi wa Tanzania.

Viongozi wa dini wanahusika pakubwa sana katika kujenga, kuimarisha, kuboresha na kuendeleza jamii ya Kitanzania. Wao ni walezi kama nilivyoeleza awali.

Jamii yetu inawahitaji viongozi wa dini ambao kwa namna moja ama nyingine ili wawezeshe ustawi wetu pamoja na kuhakikisha tunakuwa na kizazi chenye maadili mema.

Ni viongozi hawa pia wanachochea ustawi na amani katika familia mbalimbali pamoja na taasisi mzima ya familia katika nchi yetu.

Si hapa nchini pekee,bali hata kwingineko duniani, viongozi wa dini wanahusika katika kuhakikisha taasisi ya familia na watu wake wanaishi kwa amani ya roho na ustawi wenye tija kwa jamii.

Ingawaje changamoto za maadili zinazidi kuongezeka, kutokana na kuporomoka kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo hatuwezi kusema viongozi wa dini wameshindwa kabisa kujenga jamii yenye maadili, bali tutawakumbusha na kuwaomba wahakikishe wanazijenga familia.

Baada ya kusema hayo, nije kwenye hoja yangu. Kwamba ni muhimu kutambua sisi wana jamii tunahitaji malezi ya kiroho na ustawi wa familia zetu unaofanywa na viongozi wa dini hapa duniani.

Hili ni jukumu lao ikiwemo kuhakikisha nyumba za ibada zote zinakuwa mifano ya kuigwa kwa watu waumini wao kuwa wastaarabu. Kuhakikisha jamii yote mitaani inakuwa na wema,upole,uungwana na mengine yanayohusika kwa viongozi hao.

Hata hivyo katika mazungumzo hayo ya Ikulu nimeshangaa jambo moja. Katika video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi ya viongozi wa dini wamemlalamikia Rais Magufuli kana kwamba yeye anatakiwa kuchunga kila kitu cha kuijenga na kuilinda nchi yetu.

Viongozi wetu wa dini nao wanashtaki kwa Rais Magufuli badala ya kuwapa mwongozo waumini wao huko kwenye mimbari ya dini zao juu ya kuenenda vizuri katika jamii ili kurithisha kizazi bora.

Viongozi wa dini walimwambia Rais kuwa huku mitaani watu wanavaa nusu utupu, kiasi kwamba hata mtu yeyote anaweza kushangaa awaonapo.

Mshangao huo ni ule wa kusema ni kwanini viongozi ambao wanatakiwa kujenga taasisi za familia na maadili ya jamii wanakwepa jukumu lao kubwa na adhimu kabisa duniani na badala yake wanakwenda kumtwisha Rais?

Licha ya kutaka ujumbe wao usikike zaidi kwa watu wanaofuatilia mkutano wa Rais na viongozi wa dini, lakini upande mwingine unaonyesha wazi kuwa viongozi wetu wa dini wanajaribu kujenga taswira ya kujiondoa kwenye jukumu la kulinda maadili na taasisi za familia.

Kwamba waumini wanaovaa nusu utupu wanaingia nyumba za ibada wadhibitiwe. Hii inatuletea, swali; hivi viongozi hawa wanataka Rais Magufuli afanye nini?

Mamlaka ya rais ni kutuma vikosi vya ulinzi ambao vinahakikisha utulivu na amani, lakini kwenye suala la maadili ya waumini na taasisi za familia ni suala la viongozi wa dini kusimamia na kusisitiza kila wakati.

Suala hilo halihitaji nguvu za jeshi la polisi, magereza, wala jeshi la wananchi ili kuhakikisha waumini wanaingia katika nyumba za ibada wakiwa na mavazi yanayoeleweka.

Tunafahamu kuwa katika nyumba zetu za ibada kuna walinzi wa amani ambao wanawajibika kuhakikisha kila muumini aingiapo humo anakuwa mstaarabu kimavazi. Je hili tunataka kumtwisha Rais wa nchi ili achukue hatua gani?

Tafsiri unayoweza kuipata katika maombi ya viongozi wa dini kwenye suala la mavazi ni kama vile wanataka Rais Magufuli awe anapita kila nyumba ya wananchi wake au kuwatuma wasaidizi wake waanze msako kwa wanaovaa nusu utupu ili waswekwe korokoroni.

Ni dhahiri wananchi tunatambua nafasi ya viongozi wetu wa dini katika malezi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,875FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles