PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Dickson Maimu na wenzake, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi inayowakabili vigogo hao haujakamilika.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa (Nida), Avelin Momburi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Wakili wa Serikali, Janeth Magoho, alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa na kuiomba Mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hata hivyo, Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.
Maimu na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi pamoja na kuisabishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.175.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 100 kati ya hayo, 24 yakiwa ni ya utakatishaji fedha zaidi ya Sh bilioni 1.1, 23 ya kughushi nyaraka; 43 ni kiwasilisha nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wao na kuisababishia mamlaka hiyo hasara.
Mashtaka mengine ni ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu (mawili), shitaka moja la matumizi mabaya ya madaraka na mashtaka mawili ya kula njama.
Wanadaiwa kati ya Julai 19, mwaka 2011 na Agosti 31, mwaka 2015, washtakiwa wakiwa maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam walikula njama ya kufanya udanganyifu wa Sh bilioni 1.175 dhidi ya NIDA.
Maimu na Raymond wanatuhumiwa Novembe 7, mwaka 2011 wakiwa makao makuu ya NIDA, Kinondoni, walitumia madaraka yao vibaya na kusababisha Kampuni ya Gotham International Ltd kupata faida ya sh.899,935,494.