24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Trump kutangaza hali ya hatari Marekani?


WASHINGTON, MAREKANI

MAJADILIANO yameanza upya Marekani kati ya chama cha upinzani cha Democrat na kile kinachotawala cha Republican kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa muda wa mvutano wa bajeti uliopelekea watumishi wengi wa serikali kulazimika kubaki nyumbani mwao kwa kuwa shughuli za serikali zilifungwa kutokana na kukwama bajeti ya kuendesha.

Gazeti la Washington Post jana limeripoti kuwa, mpango uliopendekezwa na Rais Donald Trump na ule mbadala uliopendekezwa na Chama cha Democrat ili kukwamua mzozo wa bajeti haukusaidia kuungwa mkono vya kutosha katika Baraza la Seneti.

Kwa zaidi ya mwezi sasa, wabunge na Rais Trump wanazozana kuhusiana na suala la ujenzi wa ukuta ambao Rais Trump anataka kuujenga katika mpaka wa Marekani na Mexico, ili kukabiliana na wahamiaji kinyume cha sheria.

Waliutaja mpango huo kuwa haulingani na manufaa yanayoweza kupatikana na zaidi kuliko yote hauna maana. Wabunge wa chama cha Democrat wanapinga moja kwa moja kutengwa dola bilioni 5.7 ili kuugharimia ujenzi huo.

Wabunge hao wanapendekeza mpango mbadala wa ulinzi wa mpakani. Matokeo yake tangu Desemba 22 mwaka jana takribani watumishi 800,000 wa serikali na watumishi wengine kadhaa wanalazimika kubaki nyumbani bila malipo.

Juhudi za chama cha Republican hazikufaulu, kwakuwa pendekezo lake lililowasilishwa kupigiwa kura kwa mara ya kwanza juzi lingesaidia kugharimia shughuli za serikali hadi mwezi wa Septemba mwaka huu na linajumuisha pia fedha za kugharimia ukuta.

Chama cha Republican ndicho kinachodhibiti Baraza la Seneti, lakini kwa vile wanadhibiti viti 53 kati ya 100, walihitaji kuungwa mkono na wabunge wa Democrat ili kujipatia asilimia 60 zinazohitajika ili pendekezo la Rais Trump liweze kufikishwa katika zoezi la mwisho la kupigiwa kura. Hata hivyo, hawakufanikiwa kuwashawishi Democrat.

Mara baada ya malumbano makali,  viongozi wa Republican na Democrat katika Baraza la Seneti wakakutana kujaribu kuikwamua hali ya mambo.

Ikulu ya Marekani ilikubali kuwaachia wajadiliane kuhusu sheria ya kugharimia kwa muda wa wiki tatu kwa masharti kwamba gharama hizo zinajumuisha sehemu kubwa ya fedha za kujenga ukuta.

“Wakiniletea makubaliano ya maana nitayaunga mkono. Bila ukuta, hatuwezi kudhibiti usalama wetu,” alisema Rais Trump, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kadhia hiyo.

Hata hivyo, Trump amebakiwa na karata moja, kutangaza sheria ya hali ya hatari.

Ufumbuzi wowote inabidi upitie katika Baraza la Wawakilishi ambalo linadhibitiwa na Democrats.

Kwa upande wake, Spika wa Baraza hilo, Nancy Pelosi, ameshasema hakubaliani na bajeti ya kugharimia ukuta.

Bado haijulikani kwa hivyo mzozo utafumbuliwa vipi. Kutokana na kutofikiwa maridhiano, Rais Trump amelazimika kuahirisha hotuba yake kwa taifa aliyokuwa aitoe wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles