22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Tiger Woods ni wakati sahihi wa kustaafu Gofu

BADI MCHOMOLO

KILA Ufalme una mwisho wake, hakuna kitu kizuri kama kumaliza Ufalme wako huku watu wakiwa bado wanakuhitaji.

Eldrick Tont, maarufu kwa jina la Tiger Woods ni nyota wa mchezo wa Gofu duniani akiwa raia wa nchini Marekani, mbali na kuwa hodari kwenye mchezo huo, lakini anatajwa kuwa mmoja kati ya wanamichezo wenye ushawishi mkubwa duniani.

Huyu ni staa ambaye aliwahi kutikisa dunia katika mchezo huo pamoja na kuwa mwanamichezo ambaye anaongoza kwa kulipwa fedha nyingi miaka ya nyuma kutokana na ubora wake.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 43, alianza kuwika katika mchezo huo huku akiwa na miaka 20, ilikuwa mwaka 1996 na mwaka mmoja baadae akaweza kuwa namba moja kwa ubora duniani.

Aliweza kudumu kwenye ubora huo hadi ilipofika 2010, lakini alianza kushuka kiwango baada ya kutangaza kuwa yupo kwenye mipango ya kufunga ndoa na mpenzi wake Elin Nordegren na baada ya kufunga ndoa miezi michache baadae alitangaza kuachana.

Woods alitajwa kuwa mwanaume ambaye sio mwaminifu kwa mkewe, alikuwa na wasichana wengine pembeni na ndio maana ndoa yake haikudumu, kitendo hicho kilimfanya staa huyo akosolewe kwa kiasi kikubwa na kusababisha kiwango chake kushuka.

Ilivyofika 2011, nyota huyo katika orodha mpya ya wachezaji bora wa Gofu alijikuta akiangukia kwenye nafasi ya 58, kitendo hicho kiliwashtua mashabiki wake wengi, lakini aliwatoa wasiwasi na kuwaambia lazima arudi katika nafasi yake walioizoea.

Aliweza kupambana kwa miaka miwili na ilipofika Machi 2013 aliweza kurudi kwenye ubora wake na kushika nafasi ya kwanza, aliweza kudumu hadi Mai 2014.

Kwa kuwa alikuwa anatumia nguvu nyingi katika mazoezi ili kuweza kurudisha kiwango chake, alijikuta akipatwa na maumivu ya mgongo na mkono.

Majanga yalianza kumkuta mwaka 2013 baada ya kufanyiwa upasuaji wa mkono, lakini mwaka 2014 majanga yalizidi kwa kuwa alifanyiwa upasuaji wa mgongo mara nne kwa vipindi tofauti, hivyo hakuweza kuwa vizuri kwenye ushindani na kujikuta jina lake kwenye mchezo huo likipotea.

Mwaka 2017, alionekana kuingia kwenye ulevi, hivyo aliwahi kukamatwa na polisi na kuwekwa ndani kutokana na kuendesha gari huku akiwa amekunywa pombe na ametumia dawa za kulevya.

Hapo ndipo ndoto zake za kurudi kwenye nafasi ya kwanza au 10 bora ikaanza kugonga mwamba hasa kutokana na hali yake.

Kutokana na matatizo hayo, Woods alitangaza kuwa anataka kustaafu mchezo huo kutokana na kashfa anazokumbwa nazo pamoja na hali ya afya yake.

Alikaa muda mrefu bila ya kushiriki michuano mikubwa, hata hivyo mara ya mwisho kuchukua taji kubwa ilikuwa mwaka 2008, hivyo hakuna aliyeamini kama ataweza kuja kuwa bora tena kama ilivyo zamani.

Mbali na kashfa zote hizo, lakini wiki iliopita staa huyo alirudi kwenye ufalme wake na kutwaa taji kubwa la mchezo huo ambalo linajulikana kwa jina la Masters, huku ikiwa ni miaka miwili tangu alipotangaza nia ya kutaka kustaafu.

Haikuwa kazi rahisi kuchukua ubingwa huo, alitumia nguvu nyingi sana kufanikisha hilo, lakini hatimaye ameweza kuandika historia nyingine mpya ambayo imeshtua wengi ikiwa pamoja na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Imefikia hatua rais huyo amepanga kutaka kumpa tuzo ya heshima kutoka Ikulu hasa kwa kuthamini kile alichokifanya kwa kipindi chote cha maisha yake ya mchezo huo pamoja na kurudi kwa nguvu na kutwaa taji hilo baada ya kukumbwa na majanga mbalimbali kwa kipindi cha miaka 11.

Huu ni wakati wake sasa wa kufanya maamuzi sahihi ya kuamua kustaafu mchezo huo kwa kuwa taji kubwa ambalo alikuwa analitafuta amefanikiwa, hakuna kitu kingine ambacho anakitafuta.

Umri wake unaruhusu kustaafu hasa kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya mgongo. Akistaafu muda huu litakuwa jambo sahihi kwa kuwa atakuwa amelinda heshima yake kwa kustaafu huku akiwa na taji kubwa mkononi la Masters.

Taji hilo limemfanya ajisafishe kwa yale mabaya aliyoyafanya kipindi cha nyuma, hivyo hatakiwi kustaafu huku akiwa kwenye kiwango cha chini au akiwa kwenye matatizo, anatakiwa kustaafu huku akiwa anazungumziwa kwa jambo kubwa alilolifanya itakuwa analinda heshima yake kwa kiasi kikubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles