31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa limepoteza mzalendo wa kweli

TAIFA limempoteza mzalendo wa kweli aliyesimama imara kuhakikisha nchi yetu na jamii vinapiga hatua za kimaendeleo kwa kila hali.

Huyo si mwingine, bali ni Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi  mwenye umri wa miaka 76, aliyefariki dunia  nchini Dubai, Falme za Kiarabu jana alfajiri.

Kifo cha Mengi kimepokewa kwa hisia kali na Watanzania kila kona, huku wakionekana kuguswa na tukio hili na kumweleza kwa kadri wanavyomfahamu.

Tunakumbuka mara nyingi katika shughuli zake, marehemu Mengi  siku zote alikuwa akisema amezaliwa  wilayani Hai tarafa ya Machame mkoani Kilimanjaro katika familia masikini kutokana na  kuchangia chumba kimoja alichokuwa akilala na mifugo kama mbuzi.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana wakati wa uhai wake aliamua kupambana kweli kweli hadi kufikia utajiri mkubwa  ambao amefanikiwa kuupata. Mzee Mengi hakuwa mtu wa kukata tama jambo alilisitiza wakati wa uhai wake.

Pamoja na kukilia katika mazingira kama haya hakukata tamaa na ndoto yake ya kufanikiwa kimaisha ilimsababisha  kusoma kwa bidii ambapo alifanikiwa kusomea masuala ya uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya kuhitimu masomo  yake, Mengi alirudi nyumbani mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Uhasibu na Ukaguzi wa Mahesabu ya Coopers & Lybrand Tanzania (kwa sasa inajulikana kama PriceWaterHouseCoopers) hadi Septemba 1989 na katika kipindi hicho alichaguliwa kuwa mwenyekiti na kiongozi mwenza.

Kwa kuwa alikuwa naonekana kuwa mtu mwenye kiu ya maenedeleo, Oktoba 1989 , aliondoka Coopers & Lybrand Tanzania na kujielekeza kwenye biashara zake binafsi na kuanzisha Kampuni ya IPP Limited, ambayo ikuja kuwa kampuni kubwa kabisa ya kibinafsi nchini Tanzania.

Mbali na  hiyo, aliweza kumiliki vyombo vya habari mashuhuri kama ITV/Radio One, kampuni ya magazeti ya The Guardian Limited, Kampuni ya kuzalisha vinywaji baridi ya Bonite.

Leo hatua naye, lakini katika siku za hivi karibuni  alisaini kandarasi ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari hapa nchini na kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu na vingine vingi.

Hii yote ni namna gani ambavyo Mengi aliwezesha kuonyesha wakati wa uhai wake.

Tunaamini katika  uhai wake, makampuni yake yalikuwa nguzo kubwa katika sekta binfasi kwa kuajiri Watanzania wengi kuanzia ngazi  za juu hadi mfanyakazi wa kawaida

Tunaamini mchango wake ni mkubwa katika ujenzi wa taifa kupitia uwekezaji mkubwa aliofanya kwenye biashara,miradi mbalimbali, sekta ya habari pamoja na ushiriki  mkubwa wa kutatua changamoto za kijamii hususani kwenye sekta ya afya, elimu, na watu wenye ulemavu.

Tunatambua namna ambavyo siku zote alivyokuwa mstari wa mbele kukutanisha makubwa makubwa ya watu wenye ulemavu, bila kujali gharama ni kubwa au ndogo tofauti na viongozi wengine. Tunasema hili utakumbukwa  milele na milele na Watanzania wataendelea kukulia.

Leo hii tunasema umeondoan mapema mno  kabla ya kutimiza ndoto ya miradi mikubwa miwili aliyokuwa ameianzisha katika kuimarisha huduma za afya katika ujenzi wa kiwanda cha dawa (M-Pharmaceuticals) na  kuanzisha huduma mpya ya matibabu kwa kutumia chembechembe za mwili na maabara ya kutoa huduma ya magonjwa ya kijenetiki (Stem Cell & Genetic Engineering Technology) ili kuwasaidia Watanzania wenye magonjwa kama ya selinundu.

Sisi MTANZANIA, tunasema taifa limepoteza mzalendo wa kweli ambaye alihakikisha anaishi na makundi yote ya masikini na tajiri bila kujali kipato cha mtu. Tunamalizia kwa kuipa pole familia ya marehemu Mengi na Watanzania wote kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles