29.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 19, 2022

Siyo Mr P wala ‘Trainer’, chanzo kuachana Mondi, Zari hiki hapa

CHRISTOPHER MSEKENA

HUWEZI kumtoa Diamond Platnumz kwenye kilele cha habari za burudani Afrika kwasasa, kutokana na uwezo wake wa kutengeneza matukio yanayokuwa gumzo kila kona.

Wiki hii pia staa huyo wa singo The One,  amefanikiwa kukata kiu ya mashabiki kwa kutoa majibu ya maswali mengi ambavyo yamekuwa yakiwavuruga kwa muda mrefu kuhusu muziki, maisha na mapenzi.

JE NI KIKI KUITANGAZA NGOMA MPYA NA WASAFI FM?

Diamond alikaa kimya mwaka mzima bila kuzungumza na vyombo vya habari. Muda mwingi aliutumia kufanya shoo, kushiriki kwenye kolabo za wasanii wake na kuiandaa Wasafi Media.

Hivyo hamu ya mashabiki kufahamu mengi kutoka kwake ilikuwa juu.  Kumbuka kwa kipindi chote alichokuwa kimya hakuwahi kuzungumzia ishu ya baba yake mzazi, mzee Abdul Juma.

Mondi hakuwahi kuzungumzia uhusiano wake kibiashara ya Mkurugenzi wa Clouds Media, Joseph Kusaga pia hakuwahi kusema chochote kuhusu sakata lake na marehemu Ruge Mutahaba.

Mashabiki pia walikuwa wanatamani kufahamu chanzo au sababu za yeye kuachana na mzazi mwezake Zari The Boss Lady kwani ndiyo mambo ambayo walitaka kuyasikia kutoka kwake.

Kwa kuwa anatambua yeye ni bidhaa adimu, Diamond aliamua kuipa nafasi Wasafi Fm ili ahojiwe kwa saa 3 katika kipindi cha kwanza kwenye redio hiyo Block 89.

Lengo lake limetia kwa asilimia 100 kwani ameweza kuitangaza Wasafi Fm na Block 89 hicho ambacho ndani ya muda mfupi kimekuwa maarufu kikifuatilia na wasikilizaji wengi.

Kwa mafanikio hayo huwezi kusema alitumia nafasi hiyo kama kiki ya kuipaisha ngoma yake The One. Nasema hivyo kwasababu wimbo huo tayari ulikuwa umeshatoka, upo mtaani, unafanya vizuri mtandaoni na umetazamwa na watu zaidi ya milioni 1 kwenye chaneli yake ya YouTube hata kabla hajafanya mahojiano hayo.

AUA NDEGE KIBAO KWA JIWE MOJA

Kupitia mahojiano hayo, Diamond amefanikiwa kuua ndege wengi kwa jiwe moja. Tayari ameweka pembeni tofauti zake na baba yake mzazi baada ya kukutanishwa studio kwa ‘surprise’ ikiwa ni miaka 20 imepita toka waonane ana kwa ana.

Mondi amewajibu wale waliotaka kujua kwanini hakuonyesha kuguswa kama wasanii wengine na msiba wa Ruge Mutahaba kwa kukiri kuwa hawakuwa kwenye uhusiano mzuri mpaka anafariki hivyo hakutaka kuwa mnafiki wa kuonyesha ameguswa.

Hali kadharika ishu ya kuachana na Zari The Boss Lady ambayo ndiyo imekuwa gumzo kila kona kutokana na kumhusisha na kuchepuka na aliyekuwa memba wa kundi la P Square, Peter Okoye maarufu kama Mr P na mwalimu wake wa mazoezi, tuhuma mbazo mrembo huyo wa Kiganda alizikana usiku ule ule Mondi alipo mtuhumu.

SABABU YA KUACHANA HII HAPA

Kwenye sakata hili la Mondi na Zari wengi wanaweza wakaangalia zaidi upande wa usaliti na mapungufu ya wawili hao ambayo waliyaonyesha walipokuwa pamoja hivyo kupelekea kuachana.

Ila sababu ya msingi na kubwa iliyofanya wawili wapigane chini ni uhusiano wa mbali (Long Distance Relationship). Diamond anaishi Tanzania na Zari yupo Afrika Kusini.

Katika mahojiano hayo Diamond Platnumz mwenyewe anasema: “Katika mahusiano yangu na yeye (Zari), mimi ndiyo nilikuwa mzinguaji kuliko yeye, alikuwa ‘smart’ alikuwa ‘wife material’ vizuri kabisa, sema tu kikubwa ambacho kilisababisha haya yote ni, unajua wakati tunaanza kama masihara akazaliwa Tiffah, alipokuja Tifffah ikaja tena mimba ya pili,

“Nikamwambia mimi nafikiri sasa hivi tukae wote Tanzania kwasababu ukikaa mbali kwangu mimi ni mtihani kidogo, mtihani kwasababu mimi bado kijana, harafu mimi ni staa kwelikweli, harafu mademu wananizimia kweli kweli, kwahiyo unanipa mitihani nikiwa nimetoka ofisini narudi nyumbani sina mpenzi wangu tunaongea tu kwenye simu, nitavumilia wiki moja mbili kisha nitashindwa, akasema sawa ila siku zilivyoendelea kwenda akaonyesha hayupo tayari, mnakaaa mwezi hamjaonana ndiyo hapo sasa vijini vikaanza kuingia katikati.”

TANASHA JE?

Kama sababu ya kuachana na Zari ilikuwa ni mahusiano ya mbali vipi kwa Tanasha, mrembo kutoka Kenya ambaye ni mpenzi wa Diamond kwa sasa? Tanasha amekuwa akifunga safari mara kwa mara kuja Tanzania lakini je  ataweza kuendelea kutumia gharama za ndege kila wiki?

MR P AMPUUZA DIAMOND

Katika mahojiano aliyoyafanya na kituo cha redio Cool Fm, Mr P alisema: “ Siwezi na sitaweza kusema chochote tafadhari, nina wimbo wangu mpya na sitataka uvurugwe, ni upuuzi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,987FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles