27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Simba mawindoni Mbeya leo


WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM

BAADA ya kutakata Kanda ya Ziwa kisha Dar es Salaam, kikosi cha Simba leo kinatarajia kuanza msako wa pointi  tatu Nyanda za Juu Kusini,  itakapoikabili Mbeya City, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa  Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Kikosi cha wachezaji 22 na benchi zima la ufundi, kiliondoka Dar es Salaam jana kwenda Mbeya tayari kuwavaa wenyeji wao hao, huku ikiisubiri Tanzania Prisons ambayo jana ilicheza na Yanga Uwanja wa Uhuru.

Wekundu wa Msimbazi hao wanashuka dimbani wakiwa wametoka kushinda mechi nne mfululizo kati ya tano za Ligi Kuu.

Mechi nne kati ya hizo ilicheza Kanda ya Ziwa, ikipigwa mabao 2-1 na Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba, ikaichapa  KMC 2-1, ikaitungua Alliance mabao 2-0, zote zikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kabla ya kuitandika Biashara United mabao 2-0, Uwanja wa Karume, Musoma.

Baada ya kukamilika ziara yake Kanda ya Ziwa, Simba ilirejea Dar es Salaam na kuikandamiza JKT Tanzania bao 1-0, mchezo uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa jijini humo.

Baada ya michezo hiyo, Wekundu hao walifikisha pointi 72 na kuzidi kuikaba koo Yanga iliyoko kileleni ikiwa na pointi 77.

Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu ulivyo, pointi hizo zinawafanya Wekundu wa Msimbazi hao wazidi kuonesha matumaini ya kutetea ubingwa wao, kwani wamecheza mechi 28 pekee hadi sasa, wakipishana pointi chache na Yanga.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amezungumzia mchezo huo  na kusema watawakosa wachezaji wao wanne ambao ni John Bocco aliyeumia mechi iliyopita.

Wengine ni Pascal Wawa, Asante Kwasi ambao ni majeruhi pamoja na Haruna Niyonzima, anayetumikia kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo dhidi ya Biashara United.

Alisema waliondoka Dar es Salaam jana mchana kuelekea Mbeya baada ya kukosa ndege ya asubuhi lakini hiyo haijaharibu mipango yao ya kusaka ushindi jijini Mbeya.

“Tulitaka kuondoka leo (jana) asubuhi lakini tumeshindwa baada  ya kutokea changamoto ya ratiba ya ndege ya asubuhi, lakini hakuna tatizo muhimu kufika,” alisema Rweyemamu.

Kwa upande wa Mbeya City, wanaingia uwanjani kutafuta pointi za kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja baada ya kujikusanyia alama 40 pekee katika mechi 33 walizocheza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles