28.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Siku ‘Mchina’ Howing Kao Hojofat akigombea urais wa Tanzania

Mwandishi wa makala haya, akifanya mahojiano na Kao.

SAADA SALIM

JANUARI 12 kila mwaka visiwa vya Zanzibar vinaadhimisha sherehe ya Mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964. Maadhimisho ya sherehe hizo huambatana na mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo hushirikisha timu za Zanzibar na Tanzania Bara.

Kilele cha maadhminisho ya mwaka huu kilifanyika katika uwanja wa Gombani, huko visiwani Pemba. Kwenye upande wa michezo fainali ya mwaka huu ilizikutanisha klabu ya Simba na Azam. Mabingwa watetezi Azam waliichapa Simba mabao 2-1.

KIVUTIO CHA MAPINDUZI

Maadhamisho ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka huu kivutio kikubwa kilikuwa kwa kocha wa timu ya Malindi ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya China Howing Kao Hojofat mzaliwa wa Pemba.

Mtanzania huyo aliiongoza Malindi hadi kwenye mchezo wa nusu fainali ambako walichapwa na Simba kwa mikwaju ya penati 3-1.

“Mimi ni Mtanzania kwa kuwa nimezaliwa nchi hii, hivyo nikirudi China nitaenda kuanza moja,” anasema Howing Kao Hojofat, na kusababisha niendelee kudadisi zaidi historia yake na namna jamii inavyomchukulia visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake.

Kitendo cha Mchina huyo Howing Kao Hojofat kujishughulisha na michezo badala ya kufanya biashara kama ilivyo kwa watu wenye asili hiyo, ndicho kilichowafanya wengi kupigwa na butwaa.

BINADAMU AMEVUNJA MIPAKA

Niliamua kumtafuta kwa udi na uvumba Howing Kao Hojofat kwa sababu alikuwa mtu adimu sana na alikuwa mtu sahihi wa kufikisha ujumbe kwa wananchi wenzetu kuwa suala la mipaka ya nchi kushindwa kuzuia mahusiano ya binadamu alilowahi kuzingumzia rais mstaafu wa Marekani, Barrack Obama ni lipo dhahiri kwetu.

Niwakumbushe wasomaji wetu juu ya hoja ya Rais Obama. Mwaka 2009 Obama  akiwa ziarani nchini Ghana, alitamka kuwa mipaka ya dunia hii imevunjwa na mahusiano ya binadamu.

Tafsiri ya kauli ya Obama ni kwamba mahusiano ya binadamu yameondoa kabisa mipaka iliyopo baina ya nchi na nchi na kujenga mahusiano mapya ya kijamii.

Mathalani, uhusiano wa Barrack Hussein Onyango Obama wa Kenya na binti wa Kimarekani ulizaa mtoto aitwaye Barrack Obama ambaye alikuja kuwa rais wa Marekani. Si hilo, kwa sasa jamii tofauti zimeibuka katika mataifa mbalimbali.

ASILI YA YAKE

Katika mahojiano niliyofanya na Howing Kao Hojofat, anasema amezaliwa mwaka 1969. Elimu yake ya msingi na sekondari

ameipatia visiwani Pemba. Baada ya masomo alifanikiwa kuja Unguja kuishi kwa

kaka yake mkubwa, Hoko Kung.

Anasema akiwa Unguja, aliungana na kaka yake huyo katika biashara ya usafirishaji wa mizigo na watu kutoka Unguja kwenda Pemba, na Unguja kwenda Dar es Salaam kwa kutumia boti zao wanazomiliki zijulikanazo kwa jina la ‘Ras Nungwi’.

“Nimezaliwa Pemba, ni Mzanzibar mwenye asili ya China, wazazi wangu walikimbilia China kutokana na kuhofia maisha yao kipindi cha miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na vurugu za kisiasa,” anasema Kao.

Anaongeza kuwa kwa sasa wazazi wake wanaishi katika Kisiwa cha Macau nchini China na kwa upande wake, hafikirii kwenda huko kwa kuwa yeye ni Mtanzania.

“Mimi ni Mtanzania kwa kuwa nimezaliwa nchi hii, hivyo nikirudi China nitaenda kuanza moja, ikiwamo kuomba uraia lakini kutokana na umri wangu sioni sababu ya kurudi huko, maisha yangu yataendelea hapa Tanzania,” anaongeza Kao.

BIASHARA

Kutokana na wazazi wake kukimbia nchini kwao, Kao na ndugu zake walifika

Pemba na kuanzisha biashara ya usafirishaji wa boti pamoja na kujenga kiwanda cha kutengeneza chakula aina ya tambi.

“Usafirishaji haikuwa ni kazi maalumu kwa wazazi wangu, ilitokea ila kiwanda cha tambi ndio ulikuwa msingi katika kuendesha maisha ya wazazi wetu, walifanikiwa kufungua kiwanda hicho kilichopo eneo la Kariakoo, Unguja,” anasema Kao.

UONGOZI WA SOKA

Kao anasema aliwahi kucheza mpira nafasi ya kipa akiwa na umri wa miaka 18 katika timu ya Chipukizi iliyopo Pemba, baada ya kuja Unguja aliachana na masuala ya soka na kujikita katika biashara za wazazi

wake.

“Sikuingia katika soka kama bahati mbaya, ila soka nimeanza kulipenda toka nikiwa shule, wakati naishi Pemba kwa wazazi wangu nilikuwa mlinda mlango wa Chipukizi kipindi hicho nikiwa nasoma shule ya sekondari,” anasema Kao.

Anasema kilichomfanya aachane na soka, ni wazazi wake kumtaka aende Unguja kumsaidia kaka yake katika masuala ya usafirishaji, hivyo kutokana na kukosa muda wa kufanya mazoezi alishindwa kuendelea kisoka.

“Nilishindwa kufanya mazoezi kipindi hicho nilikuwa na umri wa miaka 18, sababu kubwa ni muda ulikuwa mdogo sana kwangu kujishuhulisha na masuala ya soka maana mara zote nakuwa bandarini katika kukagua na kusimamia boti.

“Licha ya kubanwa na kazi lakini kaka yangu alikuwa kiongozi wa timu ya Malindi, nilimuomba anipe nafasi ya kuongoza baada ya yeye kukaa pembeni na masuala ya soka,” anasema Kao.

Baada ya kaka yake kumruhusu kujihusisha na soka kwa upande wa uongozi, ndipo Kao alipoanza kujikita katika uongozi wa timu hiyo, lakini licha ya kutamani kucheza, umri ulikuwa umemtupa mkono na hakuwa na mazoezi.

CHANGAMOTO

“Changamoto kwangu ilikuwa katika masuala ya mahusiano. Nilipata bahati ya kuingia katika uhusiano na mwanamke wa Kizanzibari lakini wazazi wake walikuwa wagumu sana miaka ya nyuma kumkubalia,” anasema.

Kao anasema sababu kubwa ilikuwa ni dini, hivyo ilimlazimu kubadilisha dini na kuoa mwanamke huyo aliyebahatika kupata naye watoto wawili, Leith anayesoma kidato cha tatu na Labeeb yuko shule ya Awali (chekechea).

Akizungumzia upande wa vyakula, Kao anasema hajapata shida kwenye vyakula kwani kuna wakati alikuwa anakula ugali na samaki aina ya papa bila ya mboga nyingine hasa kipindi alichokuwa kwenye boti.

Anasema watoto wake wanakula chakula chochote kama baba yao kwa kuwa amewajenga kuishi maisha ya Kitanzania, kwa kuwa hajui kama watoto wake watakwenda kuishi kwenye maisha mengine zaidi ya wanakoishi sasa.

“Mimi nitaendelea kuishi hapa na kutafuta fedha na kuwasomesha watoto wangu, ila nitawapa uhuru wa kuchagua kama wakitaka kuendelea kuishi hapa au kwenda kufuata babu zao itakuwa juu yao,” anasema Kao.

KUMBUKUMBU YA ‘MJUKUU WA CHINA’

Kufika hapo akilini mwangu naanza kumfikiria mwanasiasa mahiri kabisa aliyepata kutikisa Afrika akitokea nchini Gabon, Jean Ping, ambaye amwahi kuwa Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Ingawa katika mazungumzo yangu sijamgusia Howing Kao Hojofat matamanio yake ya kuingia kwenye siasa lakini akilini nafikiria kuwa yeye ni mtanzania na mwenye sifa zote za kugombea nafasi za serikali za mitaa, udiwani,ubunge hadi urais.

Jean Ping alizaliwa kwa wazazi mchanganyiko wenye asili ya Gabon na China. Ni mtu ambaye alimvutia rais wa zamani wa China Hu Jintao kufanya ziara nchini Gabon wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje huku China ikimwona kama ‘mjukuu wao’.

Aliyekuwa mgombea urais wa Gabon kwa tiketi ya kambi ya upinzani. Baba yake ametokea China, anaitwa Cheng Zhiping akiwa mzaliwa wa mji wa Wenzhou.

Tofauti ya Hussein Onyango Obama (Baba yake rais Obama) na Cheng Zhiping (Baba yake Jean Ping) ni moja; Cheng Zhiping alikuwa raia wa Gabon na alipata kuwa diwani katika mji aliokuwa akiishi, lakini Hussein Onyango Obama alikuwa Mkenya, kule Marekani alienda masomoni tu.

Kwa upande wake Cheng Zhiping alioa binti wa Chifu huko Emboue nchini Gabon na kumzaa Jean Ping. Huyo Jean Ping anatambulika pia kama kijana mtiifu wa damu ya watu wa mji wa Wenzhou nchini China alikotokea baba yake na anatajwa kuwavutia zaidi viongozi wa China kuihusudu Gabon.

KUNA ‘DIWANI’ WA ANC

Jianling Wu ni mwanasiasa aliyejitokeza kuwania udiwani katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Afrika kusini mnamo mwaka 2016. Jianling Wu anafahamika zaidi kwa jina la Jenny, aligombea katika Kata ya 118 jijini Johanesburg.

Alizaliwa mjini Jilin nchini China, lakini alihamia Afrika kusini miaka 22 iliyopita akiwa na familia yake baada ya mumewe kupata kazi nchini humo. Badala yake akaomba uraia kabisa.

DUNIA MOJA

Kama nilivyoeleza huko juu, wakati tunayaona mabadiliko hayo kwa wenzetu, hata hapa kwetu akina Howing Kao Hojofat tunao wengi, na wakati utafika hatuwezi kuwa na mustakabali wa peke yetu.

Yatakapokuja kwetu tusigombe, tukubali kutambua uraia wa wenzetu bila rangi au asili za kizazi chao. Watakuwa  watumishi wetu kama Jean Ping au Jianling Wu. Tukumbushane kuwa tunao akina Howing Kao Hojofat hapa nchini, labda hawajaamua kuingia kwenye siasa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,663FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles