24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 28, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali iongeze kasi kutatua migogoro ya ardhi nchini

JUZI Rais Dk. John Magufuli, amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na viongozi wengine wa Mkoa wa Mbeya kutoa orodha ya wananchi waliogawiwa ekari 5,900 zilizorudishwa na mwekezaji pamoja na Mbunge wa Mbarali, Haroon Primohamed.

Kwamba anataka hizo ekari 4,600 pamoja na 1,300 apate orodha ya watu waliopewa na wampangie nani na nani waliopewa.

Pia anasema aliunda tume ya mawaziri wanane ikiongozwa na Lukuvi kwa ajili ya kuchunguza migogoro ya ardhi nchi nzima na tayari imetoa ripoti yao na itatolewa katika Baraza la Mawaziri ili itolewe uamuzi.

Pamoja na mambo mengine, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunamwona Lukuvi anajitahidi kutoa majawabu ya migogoro ya ardhi iliyokithiri hapa nchini.

Sisi tunaamini migogoro mingi ya ardhi hapa nchini inasababishwa na ukosefu wa uadilifu na umakini kwa baadhi ya watendaji wa wizara hiyo. Pengine kwa sababu ya ushawishi au msukumo wa vitu fulani katika mchakato mzima.

Kwa hiyo tunashauri uchunguzi uendelee kufanyika ili maofisa wanaohusika kusababisha migogoro hiyo wachukuliwe hatua.

Tunaamini Serikali haiwezi kukubali kuona Watanzania wakisumbuliwa kila siku katika migogoro ya ardhi.

Pia tunaiomba wizara iendelee kufanya juhudi kutatua migogoro yote nchini na iendelee kuielimisha jamii na wawekezaji kufuata taratibu ili kutozalisha migogoro mipya.

Pia tunaomba hatua ziendelee kuchukuliwa ili kuwabana maofisa ardhi wanaoendekeza vitendo vya rushwa.

Kwa kuwa tunafahamu ardhi kwa masikini ndiyo nyenzo ya uhakika ya kumkomboa katika lindi la umasikini, lakini wananchi wengi hasa wa hali ya chini wamekuwa wakikumbwa na migogoro ya ardhi inayosababishwa ama na wawekezaji au matajiri wanaofika na kuwapora kinyemela.

Pia tunafahamu kuwa migogoro ya ardhi inajenga chuki na wakati mwingine imekuwa ikisababisha mauaji kwa pande mbili zinazosigana.

Tunaikumbusha Serikali kufanya utafiti wa kina na kuwagundua wote wanaomiliki ardhi pasipo kuiendeleza na kuwanyang’anya.

Hatutarajii kuendelea kuona maeneo yasiyoendelezwa yakiendelea kuwapo kwa sababu pamoja na mambo mengine ndiyo yanasababisha wahalifu wayafanye ndiyo maficho yao au kufanya sehemu ya kuhifadhia silaha zao.

Tunaamini maeneo hayo yakiendelezwa kwa kugawiwa wananchi yatasaidia kukua kwa uchumi na kuwakwamua wale waliokuwa hawana maeneo.

Pia changamoto hiyo ya ardhi inapaswa kuangaliwa kwa macho mawili pasipo kuona huyo ni nani na ana cheo gani ndani ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,224FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles