22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Rungu la watoro liwageukie wabunge wasiochangia mijadala


Na LEONARD MANG’OHA

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, juzi ametangaza kumvua ubunge Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kwa kile kilichodai kuwa hakuhudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge.

Kama hiyo haitoshi Ndugai, ameitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jaji Semistocles Kaijage, kuwa jimbo hilo liko wazi.

Kupitia taarifa ya Spika, Nassari anadaiwa kutohudhuria Mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, mwaka huu, Mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, mwaka jana pamoja na Mkutano wa 14 uliofanyika kati ya Januari 29 na Februari 9 mwaka huu.

Uamuzi huo wa Spika unaelezwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (c), ambayo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

Kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, inaeleza kuwa ‘Kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge na kwamba mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano mitatu Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Uamuzi wa Spika unaibua mjadala mzito kwani ni tukio la aina yake kuwahi kutokea. Sintofahamu pia imeibuka baada ya kauli ya Nassari ambaye licha ya kukiri kutohudhuria mikutano hiyo hata hivyo amedai kuiandikia Ofisi ya Bunge barua ya kuomba ruhusa ya kutokuhudhuria Mkutano wa 14 ulioanza Januari 29 hadi Februari 9, kwa kuwa alikuwa akimuuguza mkewe.

Hata hivyo wakati uamuzi huu unatolewa Nassari alikuwa kwenye majukumu ya kibunge katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo yeye ni mjumbe. Jambo la kujiuliza ni kwamba Je; ni kweli Spika hajapokea barua ya mbunge huyo?. Ikiwa ni kweli hafahamu, hajapokea taarifa hiyo basi atakuwa sahihi kutoa  uamuzi huo kwa sababu anasimamia matakwa ya Katiba. Ikiwa ni tofauti na hivyo basi kutakuwa na jambo nyuma ya pazia.

Malalamiko juu ya utoro wa wabunge yalishapata kutolewa na Spika Ndugai na kumlazimu kutoa taarifa Novemba 15, mwaka jana na kuwataja hadharani baadhi ya wabunge, mawaziri na manaibu waziri wanaoongoza kwa utoro pasi kuwapo jina la Nassari.

Hoja yangu si kumkingia kifua Nassari bali inafikirisha kutokana na mkanganyiko ulioibuka hasa baada ya majibu ya Nassari kwamba aliiandikia Ofisi ya Bunge barua ya ruhusa lakini Spika naye akionyesha kutokuwa na taarifa zake.

Baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wameonyesha kutokubaliana na uamuzi wa Spika huku wakirejea kauli yake ya awali ya nia ya kusimamisha mshahara wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, akidai kuwa ofisi yake haina taarifa kuhusu mahala alipo, ilhali inafahamika wazi kuwa anaendelea na matibabu nje ya nchi yaliyotokana na kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 jijini Dodoma.

Spika, baada ya kutoka kwenye mkutano wa Bunge.

Kwa sababu Spika amepata kututajia majina ya wabunge wengi wanaotoroka vikao vya Bunge wakiwamo wa Chama chake ni vema akalisimamia hilo nalo bila kuwa na upande wowote, kwa kufanya hivyo itaondoa minong’ono ya kuukandamiza upinzani kama ambavyo mara zote ofisi yake imekuwa ikilalamikiwa.

Wakati suala la Nassari linaendelea kuwa gumzo kwenye viunga vya siasa itoshe kueleza kuwa ni ishara ya taa nyekundu kwa wabunge wetu hasa watoro halisi.

Wabunge wanachaguliwa kuwawakilisha wananchi hivyo kushindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge kwa makusudi ama bila kutoa taarifa ni kuwanyima haki wananchi wao.

Kama nilivyoeleza awali kuwa tukio la Nassari ni taa nyekundu ‘hatari’ kwa wabunge, basi taa hiyo pia iwe kwa wabunge ‘mabubu’ wasiochangia chochote katika mijadala mbalimbali inayohusu masuala ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Wabunge hao ni pamoja na wale wanaosubiri kuunga mkono hoja tu kwa kauli ya NDIYO au HAPANA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles