27.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Profesa Ndalichako fanyia kazi ushauri wa Mkapa, Kikwete


ANDREW MSECHU

KATIKA mjadala wa vijana na harakati ulioendeshwa na taasisi ya Change Tanzania wiki hii, kwa mara ya kwanza mwanahabari nguli, mwanasheria na mwanasiasa wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu, alionekana akisifia juhudi za Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.

Kwenye mjadala huo, Jenerali Ulimwengu anasema japokuwa hapendi kumsifu, lakini amefanya mambo mengi kwa uthubutu, japokuwa wakati mwingine anakosea angalau anathubutu.

 “Anachohitaji ni kusikiliza zaidi watu wanamwambia nini pale ambapo inaonekana tunadhani kwamba amekosea, watu wana nia njema ya kumsaidia Rais lakini wakati mwingine anaonekana kama vile hasikilizi sawasawa. Lakini ninajua kwamba angalau anao uthubutu, sasa kinachobaki ni kusikiliza kwamba watu wanasema nini,” anasema.

Kwa kuwa suala la ubora wa elimu limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu sasa, Jenerali Uliwmengu ananikumbusha hasa katika suala hili la kusikiliza maoni ya watu wenye nia njema ya kumsaidia rais, lakini inaonekana kuna kutosikilizwa sawasawa kwa watu hao.

Ushauri wa Mkapa na Kikwete

Kwa haraka, katika elimu, kutokana na kauli hiyo ya Jenerali Ulimwengu, inanikumbusha kuwa viongozi wawili waliomtangulia, ambao ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wamewahi kutoa ushauri kuhusu kuzorota kwa hali ya elimu nchini na kuona haja ya kutafuta namna ya kutatua hali hiyo.

Viongozi hawa watangulizi, huenda hawakufanya vizuri katika nyakati zao lakini kwa nafasi yao, wameweza kuona tatizo hilo baada ya kuondoka madarakani na kukaa pembeni, pengine waliamua kufanya hivyo ili kumkumbusha mwenzao eneo hilo ambalo waliona kwamba kuna mahala walikosea.

Machi 18, 2018, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mkapa alisema ipo haja ya kuitishwa mjadala wa kitaifa wa kujadili hali ya elimu nchini kufuatia shule za Serikali kuendelea kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Mkapa ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma alisema hayo akiwa mkoani Dodoma wakati wa kumuingiza kazini Makamu Mkuu mpya wa chuo hicho, Profesa Egid Mubofu na kumuaga makamu mkuu aliyemaliza muda wake, Profesa Idrisa Kikula.
Mkapa anasema mjadala huo unatakiwa kuhusisha makundi yote ya jamii bila kujali kama ni ya sekta binafsi ama ya umma sambamba na watu wa kawaida siyo wasomi pekee, ambapo kupitia njia hiyo anaamini suluhu ya kudumu itapatikana.

Hiyo ilikuwa mara ya pili Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu, kuzungumzia mustakabali wa sekta ya elimu ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.
Novemba 11, 2017; akizungumza katika kongamano la wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Mkapa alisema kwa hali ilivyo, “Tunahitaji kufanya mapinduzi kwenye elimu.”
Kwa mara nyingine, Machi 18, 2018 Mkapa alirudia kauli kama hiyo katika hafla hiyo ya kumuaga Profesa Kikula, Mkapa akisisitiza kuna janga katika elimu.
“Ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga) ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu, private university (vyuo binafsi). Napata pia minong’ono kutoka kwa vyuo vya umma kwamba kuna (crisis) katika elimu,” alisema.
Mkapa alisema aliwahi kuwa mhariri wa magazeti ya chama (Uhuru na Mzalendo) na baadaye ya Serikali (Daily News na Sunday News) na kwamba njia moja ya kujua mwenendo wa mambo ni kusoma barua kutoka kwa wasomaji.
“Nimeendelea kusoma magazeti sana hadi mke wangu ananilalamika. Lakini nyingi (barua za wasomaji) zinalalamika zinasema hivyo hivyo. Zinasema elimu yetu ina mushkeli,” alisema.
Alisema wapo watu wanaolalamika juu ya lugha, ratiba, ushirikiano, lakini pia juu ya ushirikishwaji wa wahitimu, wanaofanya kazi na wazazi ili kuamua Taifa linakwendaje katika elimu siku zijazo.
“Kwa nini ukisoma katika orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu wao katika 10 za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za Serikali ni za watu binafsi? Kama Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?” alihoji.
Alisema ni vyema kukaitishwa mdahalo wa uwazi ambao utashirikisha makundi yote na kusikia maoni yao badala kuwaachia wanataaluma pekee ambao wanaegemea kwenye ujuzi.

Kikwete aungana na Mkapa

Aprili 28, 2018 ikiwa ni mwezi mmoja baada ya Rais Mkapa kutoa ushauri huo,  Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, pia aliingia kwenye mjadala kuhusu hali mbaya ya elimu, lakini akijikita zaidi kwa kuangalia Bara la Afrika.

Kikwete aliangazia suala hilo katika wigo mpana zaidi wakati alipokuwa akizungumza kwenye kongamano lililopewa jina la ‘Mageuzi ya Afrika Katika Karne ya 21’ lililoandaliwa na Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.

Kikwete, ambaye alikuwa mmoja wa wasemaji wakuu wanne kwenye kongamano hilo, alisema Afrika inaweza kuwa inapiga hatua katika kuendeleza elimu, lakini inahitaji kuongeza juhudi hasa kutoka elimu ya msingi hadi sekondari.

Wazungumzaji wengine katika kongamano hilo walikuwa John Agyekum Kuffor, ambaye alikuwa Rais wa Ghana, Olesegun Obasanjo (Rais wa mstaafu wa Nigeria) na Carlos Verga (Waziri Mkuu mstaafu wa Cape Verde).

Shule za Serikali zazidi kuporomoka

Wakati mamlaka zinazohusika ikiwamo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zikisubiriwa kuandaa mjadala huo wa kitaifa, matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne uliofanyika Novemba 2018 na kutangazwa Januari 25 mwaka huu, mwaka mmoja baada ya Mkapa kueleza mtazamo wake, yakionesha shule za Serikali kuporomoka zaidi katika orodha ya shule 100 bora kitaifa.

Katika orodha hizo, shule sita za Serikali ambazo kwa miaka mitatu mfululizo ndizo zilizoingia katika orodha ya 100 bora zimeporomoka, isipokuwa shule ya Ilboru pekee, ambayo imeweza kupanda na kuongoza miongoni mwa shule hizo.

Shule hiyo inashika nafasi ya 36 na kuongoza miongoni mwa shule za Serikali katika matokeo ya mwaka jana, kutoka nafasi ya 39 yaliyoipa nafasi ya tatu miongoni mwa shule hizo mwaka 2017 na kutoka nafasi ya 42 mwaka 2016 iliyopata nafasi ya sita na ya mwisho miongoni mwa shule za Serikali zilizokuwa zimeingia kwenye 100 bora hivyo, kuziondoa shule za Serikali katika 30 bora.

Shule zinazofuatia ni Sekondari Kibaha, Mzumbe, Kilakala na Tabora Wavulana, Tabora Wasichana.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Avemaria Semakafu, anasema hana maneno mengi ila jibu lake ni kwamba Shule za Serikali haziwezi kulinganishwa na binafsi kwa sababu za Serikali hubeba wanafunzi wote kwa wingi wake bila kufanya mchujo wowote.

Anasema shule hizo zimekuwa zikipika wanafunzi vizuri kwa pamoja bila kuwachuja na kuwapa wote uwezo wa kufanya vizuri, tofauti na shule za binafsi ambazo zimekuwa zikifanya mchujo kila mara na kuwaacha wanafunzi wengine, hivyo kubaki na wale wanaowahitaji wao.

Nini kinachosubiriwa?

Kulingana na kauli hizo za viongozi wakuu waliopita, ambazo zimeonesha umuhimu wa kuwa na mjadala wa kitaifa kutafuta suluhu ya tatizo hilo, wadau wa elimu wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuandaliwa kwa mjadala huo, ili kujua chanzo halisi cha tatizo.

Kwa upande mmoja, Rais Magufuli ambaye huenda amekuwa akionekana kutokuwa msikivu kidogo wa ushauri wa ‘maana’ unaotolewa hata na wale wanaomtangulia ana wasaidizi wake ambao pia wanatakiwa kumsaidia kwa usikivu na kuwajibika moja kwa moja katika masuala yanayowahusu.

Tunalazimika kukumbushana, kuwa hatima ya taifa letu ni yetu sote, kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako, kumsaidia Rais kutafuta njia nzuri ya kupata suluhu ya tatizo linalozikumba shule za Serikali kwa kufuata ushauri wa ‘wakuu wa nchi’ waliotangulia, ambao wamekuwa wakijaribu kuonesha sehemu zenye upungufu na kusaidia namna ya kupata suluhu.

Iwapo tatizo hili litaendelea na itaonekana kuwa hakuna haja ya mjadala wa kitaifa, au labda iwapo Rais Magufuli hakusikia, na Waziri wake pia hakusikia, basi ni vyema Rais awe msikivu na awasaidie wasaidizi wake kuandaa mjadala huo utakaoweza kutoa suluhu ya matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles