23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lipumba apata pigo mahakamani

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha CUF upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Jaji Dk. Benhajj Masoud akitoa uamuzi huo jana baada ya kubatilisha uteuzi huo, alisema hata majina yaliyokuwa yamependekezwa na upande wa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad nayo hayakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hiyo kwa kuwa nao hawakuwa wamekidhi matakwa ya sheria.

KAULI YA MAALIM SEIF

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Maalim Seif alisema ameupokea kwa furaha na kusema mahakama imetenda haki katika suala hilo.

Taarifa iliyotolewa na CUF na kumnukuu Maalim Seif, ilieleza kwamba chama hicho kimepokea kwa furaha uamuzi wa Mahakama Kuu chini ya Jaji Dk. Benhajj Masoud uliotolewa kuhusiana na shauri Na. 13/2017 lililofunguliwa na Mbunge wa Malindi, Ally Saleh dhidi ya RITA na wadaiwa wengine 17.

“Kimsingi imetoa tamko la kisheria (Declaratory Decree) kwamba RITA haikufuata taratibu katika kusajili wale waliodaiwa kuwa ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa CUF waliosajiliwa na RITA tarehe 12 Juni, 2017 ambao waliwasilishwa na Prof. Ibrahim Lipumba na Magdalena Sakaya na kudhaminiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Uamuzi wa Mahakama Kuu chini ya Mheshimiwa Jaji Benhajj Masoud kueleza kwamba RITA haikuzingatia matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini (Trustees Incorporation Act – Cap 318 RE 2002) umekata mzizi wa fitina kuhusiana na madai yetu tuliyokuwa tukiyasema tokea awali.

“Kwamba RITA haikuwa sahihi kusajili watu waliopitishwa na kikundi kilichojiita Baraza Kuu la Uongozi la Taifa bila ya kujiridhisha iwapo kweli kikundi hicho kilikuwa ni Baraza Kuu halali la Uongozi la Taifa la CUF.

“Mahakama Kuu imetamka wazi kwamba mbali ya kwamba ni masharti ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini (Trustees Incorporation Act – Cap 318 RE 2002) kwamba RITA inapaswa isimamie (monitor) kikao kinachopitisha wadhamini wa taasisi yoyote, lakini kwa mazingira ya CUF ambapo kuna kambi mbili zinazokinzana, walipaswa kujiridhisha zaidi kuhusu uhalali wa chombo kilichopitisha wadhamini .

“Kwa ufupi Mahakama Kuu imetamka kuifuta rasmi bodi feki ya Lipumba na kikundi chake na kuitanabahisha RITA kwamba ifanye kazi zake kwa kuzingatia sheria,” alisema Maalim Seif katika taarifa hiyo.

Alisema CUF imezingatia maelezo aliyotoa Jaji Benhajj Masoud kwamba pamoja na kutotakiwa kujielekeza kuhusu hadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF, lakini kupitia ushahidi uliotolewa kwamba muda wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini waliokuwepo kabla ya Juni 12, 2017 ulikuwa haujamalizika na kwamba unamalizika mwaka huu wa 2019.

“Nikiwa Katibu Mkuu wa CUF, napenda kumpongeza kwa namna ya pekee Mheshimiwa Ally Saleh kwa kuchukua hatua ya kufungua shauri hili ambalo limeondoa utata uliokuwepo kuhusu Bodi ya Wadhamini ya chama chetu. Mheshimiwa Ally Saleh amekifanyia chama kazi kubwa sana na ya kuheshimika na kuthaminika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles