24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Ni nani huyu Inayat Kassam?


MARKUS MPANGALA

SHAMBULIZI la kigaidi lililotokea wiki hii nchini Kenya, limemwibua mwokoaji yule aliyekuwa kinara wa kuwasaidia wahanga wa tukio kama hilo miaka minne iliyopita, lilipotokea katika majengo ya Westgate nchini humo.

Jina lake ni Inayat Kassam ambaye ameibuka kuwa mmoja wa waokoaji wenye sifa nyingi na mwelekezaji mzuri kwa watu wote wanaojaribu kuokoa maisha yao kwenye matukio ya kigaidi.

Katika tukio la kigaidi la Westgate, Kassam alishirikiana bega kwa bega na vikosi vya usalama vya Kenya ili kukabiliana na magaidi waliokuwa wanaongozwa na gaidi mwanamke, Samantha Lewthwaite.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya usalama zinasema kuwa, wakati huo Samantha aliingia nchini Kenya baada ya kupita Tanzania akitumia hati feki ya kusafiria akijieleza kuwa raia wa Afrika Kusini badala ya Uingereza.

Tukio la mwaka huu limewakumbusha wananchi wa Kenya pamoja na Afrika Mashariki kwa ujumla wake kuwa Kassam ni mtu aliye tayari kuwasaidia binadamu wengine.

Mwalimu wa kupambana na magaidi

Uwepo wa Kassam katika eneo la tukio na jinsi alivyoshirikiana na Jeshi la Polisi, umeshangaza wengi ambao sasa wamemtaja kuwa shujaa wakati magaidi walipovamia Hoteli ya DusitD2 eneo la 14 Riverside Drive, jijini Nairobi.

Maofisa wa usalama wa Kenya walitumwa katika eneo hilo mara moja kuokoa maisha ya wananchi waliokuwa kwenye hatari ya kuangamizwa na magaidi hao.

Maofisa hao hawakuwa pekee yao, ndipo alipoonekana Kassam. Kimsingi Kassam ni mwalimu wa masuala ya ulinzi wa Elite Defence Academy (EDA).

Vyanzo mbalimbali kutoka nchini Kenya vinasema Kassam NI mtaalamu wa mafunzo ya kupambana na matukio ya kigaidi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Scorpio Africa Limited ya jijini Nairobi.

Tovuti ya kampuni hiyo imeeleza kifupi shughuli za Kassam. Inasema anajihushughulisha na mafunzo kutumia silaha, kupambana na uhalifu, kupambana na ugaidi, kutoa mafunzo ya ulinzi, huduma za ulinzi akiwa na uzoefu wa miaka 9 katika kazi yake.

Kassam alikuwa mmoja wa maofisa waliofika katika Hoteli ya DusitD2. Rekodi za Elite Defence Academy (EDA), Kassam pia alikuwapo wakati wa tukio la kigaidi la Westgate 2013 lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 70.

Akiwa kiongozi wa oparesheni, alifanikisha shughuli za uokoaji Westgate Mall na alikuwa msaada mkubwa sana katika kuyaokoa maisha ya wengi.

Inasadikiwa timu ya Kassam hupeana mafunzo ya kujilinda kwa silaha ama bila  silaha na matumizi ya bunduki na silaha nyingine za vita.

Aidha, Kassam anafanya kazi na mashirika mbalimbali likiwamo SKOPOS, ACT na AMOK pia ni mtaalamu katika masuala ya kulenga shabaha kwa risasi.

Taarifa zinasema Kassam amekuwa akishiriki masuala ya usalama wa jamii nchini Kenya kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Wakenya wamevutiwa na umahiri wake, walimwona akishirikiana na maofisa wa polisi wa vitengo mbalimbali kuwaokoa majeruhi na watu waliokuwa wametekwa nyara katika jumba hilo.

Zaidi ya watu 700 waliokolewa hai kutoka Dusit na Rais Uhuru Kenyatta, amevipongeza vikosi vya dola kwa kazi yao nzuri katika kukabiliana na magaidi.

Krav Maga ni nini?

Katika shughuli ya uokoaji inaelezwa Kassam ni mtaalamu wa kujilinda yaani Krav Maga kama inavyojulikana nchini Israel.

Labda swali hapa ni Krav Maga ni kitu gani? Krav Maga ni mfumo wa Jeshi la Ulinzi la Israel na vyombo vya usalama vya Israel ambao unatumia katika masuala ya ulinzi kwenye maeneo mbalimbali.

Mfumo wa Krav Maga unahusisha mbinu kama vile ngumi, mieleka, judo, kareti, Aikido pamoja na mafunzo mengine mbalimbali ya ulinzi la usalama.

Kwa mujibu wa taarifa inayopatikana kwenye mtandao wake inaeleza, Krav Maga inafahamika zaidi kulenga kukabiliana na matukio halisi ya kigaidi yanayotokea duniani.

Ufundi huo umechukuliwa kutoka kwa mkufunzi wa mabondia na wanamieleka ambaye aliwanoa mbinu za mapigano ya mitaani, mwenye asili ya Hungary na raia wa Israel, Imi Lichtenfeld.

Mkufunzi huyo alitumia mbinu hizo katika kipindi cha kuwatetea Wayahudi dhidi ya utawala wa Kifashisti wa Czechoslovakia katikati ya miaka 1930. Kassam ni mtaalamu wa Krav Maga, ambayo pia ina viwango tofauti kwa wajuzi wake.

Miaka minne iliyopita

Septemba 21 miaka minne iliyopita pale watu wanne walipoingia ndani ya majengo ya Westgate na kurushia risasi watu waliokuwepo katika eneo hilo.  Magaidi walikwenda ghorofa kwa ghorofa ili kuwashambulia, ambapo takribani 62 walipoteza maisha yao. Ni tukio hilo ndilo lililomwibua Kassam baada ya kushiriki kuokoa mamia ya watu waliozingirwa na magaidi.

Sonia Bhandari ni nani?

Kassam ni jina linalovuma mno, lakini jijini Nairobi hayuko peke yake kwenye taasisi anayoongoza. Mwingine ni Sonia Bhandari naye mkufunzi wa Karav Maga jijini Nairobi, nchini Kenya. Huyu ni miongoni mwa maofisa wa wanaotoa mafunzo kama Kassam kwa watu binafsi, mashirika ya umma, makundi ya watu, jamii na taasisi mbalimbali zinazoendesha shughuli zake jijini Nairobi. Sonia ameelekeza mafunzo yake kwa makundi ya wanawake pamoja na kuwezesha mafunzo. Amewahi kutoa mafunzo hayo katika nchini nyingine za Marekani na Afrika Kusini akiwa na uzoefu mkubwa.

Sonia anaongoza kampuni yake ya Power2You (P2U), ambayo huwezesha na kuimarisha uwezo wa wanawake na watoto kujilinda katika maisha yao. Alipata mafunzo ya mfumo wa jeshi la Israel yaani Krav Maga kupitia programu yao ya EDA Krav Maga.M

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles