27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Nguvu ya mgomo wa kula bado inatamba karne hii

*Imebadilika kuwa mbinu fanisi ya kuleta mabadiliko ya kisiasa, kijamii duniani

JOSEPH  HIZZA, DAR, ES SALAAM

MGOMO wa wiki moja wa kutokula ulioshuhudiwa ukiendeshwa na mamia ya wagomaji mbele ya jengo la Makao Makuu ya Serikali ya Hong Kong ulimalizika Jumapili iliyopita, saa chache baada ya kiongozi wa jiji hilo kukubali kuachana na mipango ya elimu yenye utata katika shule za humo.

Si makusudio ya makala haya kuzungumzia mgomo huo wa Hong Kong kwa kina bali kuonesha jinsi gani kitendo hicho kilivyo bado na nguvu.

Migomo ya kula ni mbinu kongwe za upinzani ambazo zinaonesha bado inaendelea kutamba hata katika karne hii ya 21.

Mgomo wa kula ni sehemu ya upinzani dhidi ya jambo fulani isiyohusisha machafuko au mbinyo ambao washiriki wanafunga kula kuonesha kutoridhishwa au kupinga jambo kisiasa, kijamii au kiuchumi.

Kadhalika inalenga kuchochea hasira dhidi ya walengwa na au kuwatia hatiani walengwa hao wa ugomaji huo.

Hali kadhalika una nia ya kufikia lengo maalumu kama vile mabadiliko ya kisera.

Wengi wanaoendesha mgomo wa kula hawali chakula chochote chenye nguvu ya nishati mwilini zaidi ya kushindia maji au juisi.

Inapotokea mamlaka husika hasa serikali kuwa na uwezo wa kumdhibiti mgomaji wa kula kama vile mfungwa, mgomo wa kula mara nyingi huweza kuhitimishwa kwa mgomaji kulishwa kwa nguvu.

Wakati mgomo wa kula ulikuwa tegemeo kubwa katika kuchochea mafanikio ya kisiasa katika karne ya 20, ukisaidia kuanika uozo, ukiukaji wa haki na kupindua ukandamizaji na hata kuangusha dola zenye nguvu.

Aidha kuachiwa kwa mwanasoka wa Palestina hivi karibuni, Mahmoud Sarsak baada ya kuendesha mgomo wa kula wa siku 95, kunaonesha kuwa mbinu hii ya kale ya upinzani bado haijapoteza nguvu zake asilia.

katika kizazi hiki cha digitali, mgomo wa kula bado umeweza kupenyeza ushawishi tena kwa msaada wa digitali yenyewe.

Kuachiwa kwa Sarsak kulifuatia na mgomaji mwingine wa kula Mpalestina, Khader Adnan, na kisha makubaliano yaliyofikiwa na Israel kwa wafungwa zaidi ya 1500 wa Palestina waliokuwa wamegoma kula.

Mei mwaka huu, Mwanaharakati wa Bahraini  Abdulhadi al-Khawaja alihitimisha mgomo wake wa siku 110 wa kula uliokuwa ukifuatiliwa kwa karibu duniani kufuatia harakati za upinzani dhidi ya Serikali. Aidha kiongozi wa upinzani wa Ukraine, Yulia Tymoshenko aliendesha mgomo wa kula wa siku 20 ambao ulichafua hali ya hewa wakati taifa hilo likiwa linaandaa michuano ya Euro 2012.

Nchini Iran, waandishi wa habari kadhaa waliofungwa jela na wanaharakati wengine kwa sasa  wako katika mgomo wa kula na mwaka jana m   Mwanaharakati mkongwe, Hoda Saber alikufa kwa shambulio la moyo siku 10 tu baada ya kufunga.

Nchini Urusi, wanaharakati wa bendi ya Pussy Riot walikuwa katika mgomo wa kula ambao ulitengeneza vichwa vya habari duniani na hivi majuzi tu Waziri Mkuu wa Urusi alitoa wito kwa wanamuziki hao kuachiwa.

Kizazi hiki cha intaneti kimesaidia fursa ya kuupa nguvu ugomaji wa kula kwa kuinua uelewa na uungaji mkono kutoka pembe zote za dunia.

Hata hivyo, maelfu ya migomo ya kula inaendeshwa kila mwezi kuanzia Belarus hadi Tibet, Sahara Magharibi hadi Guantanamo Bay-pia kuna hatari kuwa baadhi kupotezwa katika ulimwengu wa mtandao.

Yeyote aliyeiona filamu ya mwaka 2008 ya mtayarishaji Steve McQueen kuhusu mgomo wa kula wa gerezani atakuwa na hisia za jinsi gani kufa kwa njaa ni kubaya mno.

Mwili hushuhudiwa ukiteketezwa wenyewe, ukichimba kwa ndani katika misuli na viungo muhimu kwa nishati. Sumu za ketone – acetone, acetoacetate na beta-hydroxybutyrate – huzalishwa na kifo kuwa njiani kutokana na kukaukiwa na maji huku figo ikishindwa kufanya kazi sambamba na kufa kwa ini na viungo vingine.

Tofauti na kitendo cha kujiteketeza kwa moto, mgomo wa kula unaweza kudumu kwa wiki au miezi, ukibadili mwelekeo wa nguvu kati ya ‘wasio na nguvu’ na ‘wenye nguvu’.

Kwa kukifanya kitendo cha kujiua hadharani, mgomaji wa kula huwezesha macho kumwelekea yeye na wale aliowalenga kwa mgomo huo hupigiwa kelele zinazowafedhehesha..

Wakati watu wengi wakidhani kuwa mgomo wa kula ni tukio la karne ya 20, likitumiwa zaidi na wanaharakati na wanawake na vuguvugu za kupigania Uhuru za Ireland na India, ukweli ni kwamba njia hiyo inarudi nyuma zaidi ya hapo katika historia ya mwanadamu.

Wagomaji wa kula waliendesha vitendo hivyo kipindi cha Ireland ya zama za kati, India ya kale na katika enzi za Waroma.

Hata kijana mdogo Tiberius aliendesha mgomo wa kula ili kumshinikiza mjomba wake, Augustus Caesar, amruhusu asafiri kwenda Rhodes.

Wakati Tiberius akigoma kula kwa siku nne, mwaka 25 Kabla ya Kristo, akipinga kuzikwa kwa uhuru wa kutoa maoni Cremutius Cordus alifunga hadi kifo.

Katika Ireland ya zama za kati, ambako ugomaji kula ulikuwa ukitambulika kisheria, ilikuwa mbinu iliyozoeleka kwa watu kufunga wakishindia nje ya mlango wa mtu wanayemlenga.

Iwapo mgomaji wa kula aliruhusiwa kufa, mtu ambaye mgomaji wa kula alimfia mlangoni mwake atahusishwa na kifo hicho na atapaswa kuilipa fidia familia ya mfiwa huyo.

Ugomaji wa kula pia uliendeshwa na baadhi ya watu wa dini kwa mujibu wa hadithi zilizopo. Hata Mtakatifu Patrick wa Ireland, aliendesha mgomo wa kula dhidi ya Mungu.

Kiongozi huyo wa kidini, alipanda kileleni mwa mlima, akikaa na kutamka kuwa hataondoka mlimani hapo hadi afe au maombi yake yote yatekelezwe’

Baada ya siku 45, hadithi inadai kuwa Mungu alisalimu amri kwa kumtekelezea madai yake ikiwamo ahadi ya Ireland kutoangukia mikononi mwa England.

Katika India ya kale, wagomaji wa kula pia waliendesha migomo hiyo nje ya milango ya wale wanaowasilisha madai yao au wanaodhani kuwa wamewafanyia vibaya, ikiwamo wadeni wao.

Mbinu hiyo nchini humo inajulikana kama ‘sitting dharna,” inarudi nyuma miaka 400-750 Kabla ya Kristo, ambapo ilionekana nyakati za Sanskrit, Ramayana na ilikuja pigwa marufuku kisheria mwaka 1861.

Mbinu hizi za jadi za jamii hizi za Ireland na India za kale zimeendelea kwa namna nyingine katika vuguvugu za Jamhuri ya Ireland na wakati wa harakati za kudai uhuru wa India.

Nchini Ireland mbinu hiyo ilipata umaarufu baada ya Pasaka mwaka 1916.

Mwaka 1920, mgomo ulioendeshwa na Meya wa Cork Terence MacSwiney uliiteka dunia.

Wakati alipokufa baada ya siku 73 bila kula chakula, watu 40, 000 walijitokeza kuangalia msafara wake wa mazishi na hata Papa alituma baraka zake.

Baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Ireland mwaka 1923, wafungwa zaidi ya 8,000 wa IRA waliopinga Mkataba wa Anglo-Irish wa mwaka 1921 walikwenda katika mgomo wa kula.

Katika miaka ya 1940 mamia ya migomo ya kula ilifanyika na katika miaka ya 1970 ikifufua mbinu hizo za kale.

Lakini ulikuwa mgomo wa gerezani mwaka 1981, ambao Bobby Sands na wafungwa wengine tisa walifunga kula hadi kufa, ambayo, ndiyo umekuwa alama kubwa zaidi ya kudumu kuhusu kitendo hiki.

Sands na wenzake waliingia katika mgomo wa kula baada ya Serikali ya Uingereza kuhujumu mkataba wa kurudisha hadhi yao ya ufungwa wa kisiasa.

Kwa siku nne baada ya Sands kukataa kula Mbunge wa Fermanagh & South Tyrone alifariki dunia na kulazimisha uchaguzi mdogo.

Chama cha Sinn Fein kikamteua Sands kuwania kiti hicho na ushindi wake mkubwa katika uchaguzi ulikuwa gumzo la dunia na kulifanya gazeti la New York Times kugusia kuwa Sands alimgaragaza vibaya Waziri Mkuu wa Uingereza.

Nchini India, Mahatma Gandhi aliendesha migomo 17 ya kula katika miaka ya 1920, 1930 na 1940.

Wakati sehemu kubwa ya migomo hiyo ilielekezwa kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza, mgomo wake wa kula wa mwaka 1948 ulilenga kukomesha machafuko ya umwagaji damu ya kidini ambayo yalishuhudia kumeguka kwa taifa hilo na kuzaliwa Pakistan.

Ijapokuwa Serikali ya Uingereza ilisalimu amri kwa mengi ya madai yake, nyaraka za siri zilizotolewa mwaka 2006 zilionesha kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo Winston Churchill alikuwa akipinga mbinu hizo na alipendelea mkakati wa kumwacha Gandhi afie jela.

Katika barua yake kwa mwanafunzi, Mahatma Gandhi, aliandika: “Katika hali fulani, kufunga ni moja ya silaha ambayo Mungu ametupatia wakati wa maisha yasiyo na matumainim,”

Kipindi cha karne nyingi mgomo wa kula umebadilika kutoka kuwa mbinu ambayo watu binafsi waliitumia kudai kitu fulani kutoka kwa wenzao hadi kuwa njia fanisi ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii.

Migomo ya kula inayoendeshwa magerezani, katika maeneo ya mbali au nchi zenye tawala kandamizi inaweza kuwa ngumu kufahamika hadharani lakini kizazi cha digital kinatoa fursa kwa watumiaji wa njia hii isiyo ya machafuko kuonesha kitendo cha moja kwa moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles