27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Msiba wa Mengi wakutanisha vigogo

  • Mwili wake kuletwa leo nchini, kuagwa kesho Dar

NORA DAMIAN

MSIBA wa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya IPP, Dk. Regnald Mengi, umewakutanisha viongozi mbalimbali wa Serikali, wakiwamo mawaziri, wabunge na wafanyabiashara wa kada mbalimbali.

Wakati viongozi hao wakiendelea kumiminika nyumbani kwa marehemu Kinondoni Ada Estate, mwili wa mfanyabiashara huyo maarufu nchini unatarajiwa kuletwa leo na ndege ya Emirate saa 8:30 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

MTANZANIA jana lilipiga kambi nyumbani kwa marehemu ambapo viongozi mbalimbali walifika na kutoa rambirambi zao akiwamo Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba pamoja na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM).

Baadhi ya vigogo hao waliofika nyumbani kwa Dk. Mengi jana ni Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

Wengine ni Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CCM), Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais ambaye pia ni mke wa Rais Mstaafu, Salma Kikwete.

Pia wamo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, Katibu Mkuu Mstaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti vigogo hao walimzungumzia Dk. Mengi kama mtu jasiri aliyeweza kusimamia kila alichokiamini.

“Alikuwa msaada mkubwa sana kwa Watanzania bila kujali imani zao, kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa. Mimi nitamkumbuka sana kwa sababu akiwa mapumzikoni Zanzibar mume wangu (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete), aliongea naye na mimi niliongea naye.

“Kuna jambo aliniambia kuhusu taasisi yangu ya Wama na akasisitiza atalitatua na akasema atamhitaji mwanangu Ally aende ofisini kwake pindi atakaporudi,” alisema Salma.

Alisema Dk. Mengi alimsaidia mambo mengi hasa katika shule zake ikiwamo ya Nyamisati iliyoko wilayani Kibiti.

“Ninaamini kazi aliyotumwa na Mwenyezi Mungu ameifanya kwa uadilifu mkubwa, tuyakumbuke aliyoyafanya ili tumuenzi vizuri,” alisema.

Naye Hawa Ghasia alisema, Dk. Mengi alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara waliowasaidia wabunge wanawake kwenye majimbo yao.

“Urithi aliotuachia ni kufanya kazi, kujiamini, kuendeleza uzalendo na kusaidia wasiojiweza,” alisema Hawa.

Mbunge wa Kinondoni, Mtulia, alisema ameondokewa na mpigakura wake na kiongozi mwenye maarifa mapana.

“Tulipokwenda kupokea ndege Airport nilionana naye tukazungumza, ni masikitiko makubwa kwani tulikuwa tumepanga kukutana. Ameondoka kimwili lakini kimawazo bado tuko naye,” alisema Mtulia.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Mwapachu, alisema alimfahamu Dk. Mengi tangu Julai mwaka 1982 na kwa muda wote huo walikuwa wakishirikiana katika mambo mengi hasa ya kiuchumi.

“Ni rafiki yangu hivyo nimemkosa mtu ambaye alikuwa moyoni mwangu. Nitamzungumzia zaidi Jumanne (kesho),” alisema Balozi Mwapachu.

Waziri wa Madini, Biteko, alisema Dk. Mengi alikuwa mdau muhimu katika sekta ya madini na aliyemiliki leseni.

MAZISHI

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Familia, Michael Ngalo, mwili wa Dk. Mengi utaletwa nchini leo na baada ya kufika utapelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi, Lugalo.

Kesho ataagwa katika Viwanja vya Karimjee na keshokutwa atasafirishwa kwenda Machame mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi.

HISTORIA YAKE

Dk. Mengi alizaliwa Machame, Kilimanjaro mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Abraham Mengi na Ndeekyo Mengi.

“Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki si zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu, napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile,” aliwahi kusema wakati wa uhai wake.


Dk. Regnald Mengi

Alianza safari yake kielimu katika Shule ya Msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School na baadaye Shule ya Sekondari Old Moshi. Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika (KNCU), Mengi alisomeshwa masomo yake ya Shahada ya Kwanza ya Uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya masomo alirudi nchini mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania (sasa Price Water House Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.

Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited ambayo baadaye ilifahamika kama IPP Limited.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio.

Mpaka umauti unamfika Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (MOAT).

Mengi pia amekuwa akijitoa katika kusaidia wasionacho na wenye uhitaji kwenye jamii wakiwamo wenye ulemavu na kugharamia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo nchini India.

Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia dola milioni 560.

TAMKO LA MOAT

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mtendaji wa Chama cha wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), Henry Muhanika, ilieleza kwamba wameendelea kupokea salamu za pole na masikitiko kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi, kutokana na kifo cha Mwenyekiti wake, Dk. Reginard Mengi.

Mengi alifariki Mei 2, mwaka huu Dubai, Falme za Kiarabu.

“MOAT inaendelea kuwashukuru wadau hao kwa ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa katika kufanikisha msiba huu mzito kwa tasnia mzima ya habari na taifa kwa ujumla wake.

“Aidha, MOAT kupitia kikao chake maalumu cha Kamati ya Uongozi kilichofanyika leo (jana) jijini Dar es Salaam, inaendelea kutoa wito kwa wadau wa vyombo vya habari, wakiwamo waandishi wa habari na wahariri wake, kuvitumia vyombo vyao kuendelea kumuezi Dk. Mengi kwa kutangaza yale yote yaliyomema ambayo mzalendo huyo wa taifa alikuwa akiyasimamia,” alisema Muhanika katika taarifa yake.

Dk. Mengi alikuwa Mwenyekiti wa MOAT tangu kuanzishwa kwa taasisi hii mwaka 2001 na katika kipindi chote hicho hadi mauti yalipomkuta.

Alisema Kamati ya Uongozi imekubaliana kwa kauli moja kwamba, wanachama wa MOAT wataendeleza ushirikiano wao ili kumuezi Mwenyekiti wao, Dk. Mengi na kuendeleza falsafa yake ya kuviunganisha vyombo vya habari nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles