28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mrema aiangukia Serikali iruhusu mikutano ya siasa

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MWANASIASA mkongwe nchini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, ameipigia goti Serikali akiomba iruhusu mikutano ya kisiasa ifanyike ili kuvinusuru vyama vidogo ambavyo havina uwakilishi bungeni.

Akizungumza juzi jijini hapa, Mrema aliiomba Serikali ipitie upya uamuzi wake wa kuzuia mikutano ya hadhara kwani vyama vyote vya siasa vinajenga nchi moja.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, alisema hatua ya kuzuiwa kwa mikutano bado inaendelea kuvidhoofisha vyama vidogo kwani kwa sasa hawana eneo la kusemea kama ilivyo kwa vyama vyenye wabunge ndani ya Bunge.

 “Kwa mfano nataka Serikali iruhusu mikutano ya kisiasa kwa vyama vyote vya siasa kwani vyama vyote vinajenga nchi,” alisema.

Licha ya ombi hilo pia ameitaka Serikali inapofanya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa iweze kuangalia umuhimu wa kuvipatia vyama vidogo ruzuku ili viweze kujiendesha.

“Lakini pia ikumbukwe kuwa vyama vyote vinatakiwa kupewa ruzuku ili viweze kujiendesha,” alisema.

Mrema alisema yapo mambo ambayo katika marekebisho ya siasa lazima yaingizwe na kutoa nafasi sawa kwa vyama vya siasa vidogo na vikubwa kwani vyote vinafanya siasa za kulijenga taifa kwa misingi ya utaifa.

Katika hatua nyingine, alivitaka vyama vya siasa hasa vya upinzani kuangalia uwezekano wa kuunganisha nguvu kuusoma vyema muswada wa vyama vya sheria na kuona ni wapi kuna mapungufu ili yaweze kurekebishwa na yale mazuri yakubaliwe.

Mwenyekiti huyo wa TLP, alisema licha ya kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali kwa sasa, lakini hawezi kufumbia macho mambo maovu ambayo yanafanywa na Serikali na kama yatakuwepo atayasema.

“Mimi pamoja na kuwa mtumishi wa Serikali, lakini ikumbukwe kuwa nimeitumikia sana nchi hii kwa nafasi mbalimbali, hivyo basi siwezi kunyamaza pale ninapoona mambo yanaenda vibaya, lakini pia ninapoona mambo yanaenda vizuri nitasema ukweli,” alisema.

Mrema pia alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kusimamia vizuri ujenzi wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara na reli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles