23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Mpaka wa Holili si salama- Majaliwa

Na UPENDO MOSHA, ROMBO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema mpaka wa Holili haupo salama kutokana na kuwapo njia nyingi za panya zinazotumiwa na wahalifu kupitisha silaha na bidhaa za magendo.

Mpaka huo ambao upo Rombo mkoani  Kilimanjaro ndio wenye njia kuu inayounganisha Tanzania na Kenya kwa upande wa mkoa huo.

Kauli hiyo aliitoa jana mpakani hapo  baada ya kutembelea kituo cha pamoja cha forodha cha Holili ambapo alisema kuwa zipo dalili kubwa zinazoashiria kutoweka kwa usalama katika mpaka huo.

Alisema hali hiyo inatakiwa kudhibitiwa  haraka na vyombo husika.

Aliongeza kwa kusema uwapo wa njia nyingi za panya katika mpaka huo kunahatarisha  usalama wa nchi zote mbili za Kenya na Tanzania na kwamba matukio ya uhalifu yanayoendelea kutokea katika baadhi ya mikoa iliyopo mipakani ni dalili ya kwamba mipaka haipo salama.

“Vipo viashiria vingi  vya uvunjifu wa amani katika mpaka huu wa Holili na sio hapa tu bali kuna baadhi ya mikoa iliyopo mipakani tumeshuhudia matukio ya uhalifu ikiwamo utekwaji wa watoto, hali hii inatokana na kuwapo kwa njia nyingi za panya  na ili tuwe salama lazima tubadilike.

“Nchi hizi mbili Tanzania na Kenya ni ndugu lakini undugu huo umekuwa ukidumishwa kwa kufuata sheria za nchi husika na Kila nchi inawajibu wa kulinda usalama wake lakini kwa utamaduni huu  wa kuaminina  hatuwezi kuwa  salama,”alisema Waziri Mkuu.

Katika muktadha huo alisema kila mwananchi anawajibu wa kulinda mpaka huo na sio kuliachia jeshi la polisi peke yake.

Aliongeza kwamba kila raia wa Kenya anayetaka kuvuka mpaka huo kuja upande wa Tanzania anapaswa kufuata sheria, vivyo hivyo kwa raia wa Tanzania wanaotaka kwenda nchini Kenya.

“Mtanzania anayetaka kuvuka kwenda Kenya lazima atoe taarifa katika kituo hichi vilevile kwa wakenya wanaotaka kuja Tanzania kwa sababu masharti yaliopo sio magumu na iwapo mtaendelea kutumia njia za panya mnatoa fursa kwa wahalifu  kupata mwanya wa kupitisha silaha na bidhaa za magendo,”alisema.

Alisema iwapo mwananchi yeyote atakamatwa akipita njia hizo za panya hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na kwamba kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro inawajibu wa kusimamia suala hilo kikamilifu.

“Mpaka wetu unamatatizo makubwa, kuna vitu vinafanyika ambavyo havizingatii sheria  hivyo tupunguze kuaminina katika ulinzi wa mpaka wetu na kamati ya ulinzi na usalama hakikisheni mnawachukulia hatua watu wote mtakaowakamata wakivuka mpaka kinyume cha sheria.

“Kila mwananchi anahaki ya kuvuka mpaka huu kwa kuzingatia sheria lakini pale inapotokea  mtu yeyote anayetaka kupita bila kuzingatia sheria hatutaweza kuvumia suala hilo”alisema

Aidha alionyesha kukasirishwa kwa kitendo cha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Magreth John cha  kushindwa kulipa asilimia 20  ya fedha za mapato zinazotokana na uchimbaji wa madini ya Pozolana.

Kutokana na hali hiyo Waziri Mkuu  alimpa siku 15 mkurugenzi huyo kuhakikisha analipa fedha hizo zaidi ya sh milioni 118.

 “Asilia 20 ya Fedha zinazotokana na mapato ya madini haya mnawajibu wa kukipa kijiji fedha hizo na hilo lipo kisheria kwa sababu hamuwezi kuchimba madini na kuwaachi wananchi mashimbo bila wao kunufaika”alisema

Awali Mkuu wa Wilaya  ya Rombo, Agness Hokororo alisema mpaka wa Holili unakabiliwa na changamoto ya uwapo wa njia nyingi za panya ambazo ni zaidi ya 260 na zimekuwa zikitumika kupitisha magendo na wahalifu.

“Tumeomba pikipiki kwa mamlaka ya mapato nchini na lengo kubwa ni kudhibiti magendo  katika vipenyo hivyo pamoja na wahalifu wanaopita kwa njia za panya hapa mpakani,” alisema Hokororo.

Pia alikizungumzia kituo cha pamoja cha forodha cha Holili kwa kusema kimesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato hadi  kufikia asilimia zaidi 100  kwa mwaka 2018/2019 ikilinganishwa na mwaka 2017/2018  ambapo mapato yalikuwa yakikusanywa kwa asilimia 80.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles