27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa ametia chumvi kwenye kidonda

MARKUS MPANGALA 

TAARIFA ya kujiuzulu Mkuu wa timu ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Benjamin Mkapa, imewashtua wengi katika duru za kisiasa na kidiplomasia.

Kwa vyovyote vile uamuzi wa kuachana na usuluhishi katika mgogoro wa Burundi kunaibua mjadala ambao kama Taifa tunaguswa moja kwa moja na hali ya jirani zetu Burundi.

Usalama na utulivu wa Burundi ni jambo muhimu kwa Tanzania kama jirani yake pamoja na mwanachama mwenzake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Baada ya marais wa Uganda, Kenya na Tanzania kukabidhiwa majukumu na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea na mazungumzo na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kutatua mgogoro nchini Burundi, msuluhishi mkuu  Mkapa, ameamua kujiuzulu kwenye nafasi yake, hali ambayo inaongeza shaka na wasiwasi mwingi kuhusiana na mustakabali wa kisiasa nchini Burundi pamoja na hasimu wake nchi ya Rwanda na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Mkapa amejiuzulu huku akitoa shutuma nzito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo anaishambulia kwa kushindwa kuunga mkono jitihada zake za usuluhishi wa kisiasa nchini Burundi.

Januari 31, mwaka huu Mkapa aliwasilisha ripoti ambayo ilikuwa bado ni siri kwa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni taarifa nzima ya kueleza majukumu yake katika usuluhishi wa taifa hilo ambalo limekuwa katika hali mbaya ya vita ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 1994.

Mkapa amekaririwa na vyombo vya habari akisema: “Serikali na upinzani wanapaswa kuzungumza na kukubaliana kuhusu mfumo wa kisheria na taratibu zinazohitajika kufanyika kwa uchaguzi ujao.”

Duru za kisiasa zinasema kuwa Mkapa amekuwa akisikitishwa na hatua ya Serikali ya Burundi kususia kikao cha mwisho cha mazungumzo. Ametafsiri kuwa ni ushahidi wa msimamo wa muda mrefu wa viongozi wa Burundi wa kutoshiriki katika mazungumzo baina ya Warundi.

Aidha, Mkapa alikwenda mbali kwa kuongeza kuwa masikitiko yake zaidi ni kutoungwa mkono vya kutosha katika jitihada zake na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

Hatua ya Mkapa mbali ya mgogoro wa ndani wa Burundi, inatukumbusha mzozo ulioibuka kati ya Rwanda na Burundi hali ambayo inaongeza msuguano ndani ya EAC.

Mgogoro baina ya Rwanda na Burundi umefika mahali pabaya baada ya Rais Nkurunziza, kuandika barua kwenda kwa aliyekua Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda na kueleza kinaga ubaga juu ya hali ya kisiasa nchini mwake, uhusiano wake na jirani yake Rwanda na sababu za kutohudhuria vikao vya Jumuiya hiyo vilivyotakiwa kufanyika jijini Arusha nchini Tanzania.

Ndani ya barua hiyo Rais Nkurunziza, ametangaza kuwa mzozo wa wazi kati ya taifa lake na taifa jirani la Rwanda katika kinachoonekana kuwa kudorora zaidi kwa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Rwanda na Burundi zimekuwa na uhasama kwa muda mrefu na kusababisha wabunge wa Burundi katika Bunge la Afrika Mashariki kushindwa kuhudhuria baadhi ya vikao vilivyofanyika mjini Kigali Februari mwaka 2017.

Serikali ya Burundi imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindikana la mwaka 2015 dhidi ya Rais Nkurunziza.

Hatua ya Burundi kudai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao, imesababisha taharuki miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Serikali ya Rwanda, mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo, huku ikibainisha kuwa ni Burundi ndiyo inahusika kuwasaidia waasi wanaopambana na Serikali ya Rais Paul Kagame.

Barua ya Desemba 4, mwaka jana ya Rais Nkurunziza iligusia uadui wa nchi yake na Serikali ya Rwanda na kusisitiza kuwa nchi hiyo si washirika tena ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bali ni kama maadui.

“Rwanda ndiyo nchi pekee katika kanda hii ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui ya nchi yangu,” ameeleza Rais Nkurunziza katika barua hiyo.

Nkurunziza alitaka kufanyike mkutano maalumu wa wanachama wa EAC kujadili mgogoro huo kati ya Rwanda na Burundi.

Viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo ambayo kwa sasa inajumuisha Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudan Kusini, walipanga kukutana Desemba 27, mwaka jana, hata hivyo mkutano huo uliahirishwa tena kutokana na ujumbe wa Burundi kutowasili mkutanoni.

Burundi imekuwa ikisisitiza kwamba, Rwanda ndiyo chanzo kikuu cha machafuko yaliyotokea kwao tangu Aprili 2015 na kwamba mzozo huo ulianza mapema mwaka 2010, baadhi ya makundi ya upinzani yalipoanza kusema hakungekuwa na Uchaguzi Mkuu 2015.

Aidha, Burundi inadai kwamba Rwanda imekuwa ikihusishwa katika matukio ya ukosefu wa amani, ikishirikiana na mkoloni wa zamani Ubelgiji ili kudhoofisha Serikali na ustawi wa wananchi wa Burundi.

Barua hiyo imeongeza kuwa “Rwanda ilikataa kushirikiana na kundi la pamoja la kutathmini hali halisi lakini Burundi ilishirikiana kikamilifu na huu ni ushahidi tosha kwamba taifa hilo halijawahi kutaka ukweli ufahamike kwa sababu ya uchokozi wake dhidi ya Burundi. Ni wazi kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haipaswi kufumbia macho mateso haya yanayowakuta wana Burundi.”

Burundi imesema kamwe haitakubali pendekezo la Jumuiya ya Kimataifa la kuruhusu vikosi vya kulinda amani kutoka nje na kutolewa kwa msamaha kwa wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya Serikali ya mwaka 2015, kama masharti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2020. Barua hiyo inasema kukubaliwa kwa mapendekezo hayo kutakuwa ni ukiukaji wa sheria za Burundi.

“Wahusika katika mapinduzi ya Serikali kote huwajibishwa na kushtakiwa katika mahakama na majopo ya mahakama, kwanini basi hawa wa Burundi iwe tofauti kwao? Nasikitika, Mheshimiwa Rais Museveni kukufahamisha kwamba kamwe sitaketi meza moja na wahusika wa mapinduzi, ninapendekeza kuandaliwa kwa kikao maalumu cha viongozi wa mataifa ambacho ajenda yake itakuwa kutatua suala la mzozo wa wazi kati ya Burundi na Rwanda,” amesema Nkurunziza kwenye barua hiyo.

Inakadiriwa kwamba, watu zaidi ya 1,000 wameuawa kutokana na mgogoro wa Burundi. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), ilitangaza kwamba inafanya uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

Novemba 30, mwaka jana, Rais John Magufuli, Rais Museveni na Rais Uhuru Kenyatta, walipokwenda kwenye Mkutano wa 20 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), hawakuweza kuendelea na kikao, kwa kuwa Burundi hawakuwepo.

Mwenyekiti wa EAC aliyemaliza muda wake, Museveni, alikaririwa na vyombo vya habari akisema mkutano huo uliahirishwa kutokana na Burundi kutohudhuria.

Katika majibu yake kwa Rais wa Burundi, mwenyekiti wa EAC aliyemaliza muda wake, Museveni, alisema mgogoro wa Burundi unasimamiwa na mikataba ya Mwanza na Arusha.

Vile vile alimkumbusha Nkurunziza juu ya jitihada za Mwalimu Nyerere kutatua mgogoro wa ndani ya Burundi kabla ya kurukia ‘maadui’ wa nje ya nchi hiyo. Museveni amekiri kuwa mgogoro wa Rwanda na Burundi unaathiri suala la soko la pamoja la biashara katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki.

“Nakiri kuwa mgogoro baina ya Rwanda na Burundi unapaswa kujadiliwa. Hilo ni kwa mantiki ya soko la pamoja. Suala la soko la pamoja ni muhimu, linahusu usafirishaji au usambazaji wa bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine na kinyume chake. Uhuru wa watu na kufanya biashara miongoni mwa nchi wanachama. Iwapo kuna mgogoro, ni kwa kiasi gani familia, wafanyabiashara, kampuni zinaweza kuwa na maendeleo?” ilisema barua ya Museveni.

Kwa muktadha huo, uamuzi wa Mkapa kung’atuka katika usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ndio unamwaga chumvi kwenye kidonda kinachowasumbua wakuu wa nchi zote wanachama wa EAC.

Uganda na Kenya wanagombania kisiwa cha Mingingo. Rwanda na Burundi wanahasimiana kwa kufadhili waasi. Tanzania imewahi kuingia kwenye vita baridi na Rwanda. Tanzania na Kenya wamo kwenye misuguano mara kwa mara kuhusu biashara na diplomasia ikikumbukwa suala la Uchaguzi wa Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika ambapo Kenya ililaumu jirani zake kutompigia kura mgombea wao Balozi Amina Mohammed.

Kwa mazingira kama hayo, inapotokea  msuluhishi wa mgogoro wa Burundi akiamua kuachia ngazi huku akilalamikia masuala mbalimbali ya ndani ya Jumuiya ni ishara mbaya na ya dalili kufuga matatizo yenye madhara baadaye. Ndiyo kusema uamuzi wa Mkapa umetia chumvi kwenye kidonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles