28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mgongano wa masilahi zimwi linalotafuna maadili yetu

LEONARD MANG’OHA

KUMEKUWAPO na mashauri mbalimbali yanayofunguliwa mahakamani yakihusisha viongozi na watumishi wa umma ama kwa kufanya biashara na taasisi wanazoziongoza au kutoa kandarasi kwa ndugu na jamaa zao kinyume cha matakwa ya sheria na kusababisha mgongano wa masilahi.

Mgongani wa masilahi ni nini?

Ni mgongano kati ya wajibu wa mtumishi wa umma na masilahi binafsi ya kiongozi au mtumishi wa umma ambao ana masilahi na uwezo binafsi, unaweza kumshawishi visivyo mtumishi au kiongozi huyo katika kutekeleza majukumu na wajibu wake.

Kwa mujibu wa mjadala wa kuadhimisha siku ya maadili na haki hivi karibuni, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, anasema ili kuwe na mgongano wa masilahi lazima kuwe na mambo manne yaani masilahi ya msingi au ya awali au masilahi ya umma au masilahi ya taaluma, pili kuwe na masilahi ya pembeni au binafsi, tatu kuwe na jukumu au wajibu kwa umma na kisha kuwe na mgongano wenyewe.

Jaji chande anasema masilahi binafsi ndiyo kishawishi basi ni lazima yatolewe kafara dhidi ya masilahi ya umma, ambayo mara zote ndiyo yanayotakiwa kusimama.

“Ikumbukwe pia kuwa wanaohudumia umma si tu viongozi na watendaji. Kuna wataalamu, wao pia wanabanwa na masharti na matakwa ya mgongano wa masilahi. Mgongano wa masilahi hasa unahusu uhusiano wa kindugu, kirafiki, kijamaa, kibishara, kifedha, ubia na mwenendo au vitendo” anasema Jaji Chande.

Anadai kuwa mgongano huo unashawishi na kudhoofisha uwezo wa kiongozi au mtumishi kuamua kwa ufanisi kadiri ya sheria, taratibu na ubora wa hoja, hivyo panapotokea mgongano wa masilahi maamuzi yanafanywa, lakini motisha na hamasa yake ni tofauti na kwa sababu ambazo si sahihi.

Madhumuni makuu ya kulipa uzito na kulisimamia kwa karibu suala hili la mgongano wa masilahi ni kuimarisha imani ya wananchi kwa uongozi wa nchi, utendaji kazi na sekta ya umma.

Madhumuni mengine ni kujenga dhana kuwa maamuzi yanayotolewa na viongozi au mtumishi hayakushawishiwa visivyo. Pia kuimarisha uhalali (legitimacy) wa taasisi na maamuzi.

Watumishi wanatakiwa si tu wafanye kwa usahihi mambo ya kiufundi na mambo ya kitaalamu kwa ufanisi, bali wanatakiwa kufanya maamuzi hayo kwa maadili sahihi.

Kwa kawaida mgongano wa masilahi unatishia ubora wa maamuzi na kuyafanya maamuzi yenyewe yasiaminike na mwananchi.

Ifahamike kuwa mgongano wa masilahi unaweza kutokea kwa sababu za makusudi, lakini pia kwa sababu zisizokusudiwa au kwa mtumishi hata bila kuhisi kuwa ana upendeleo.

Wanazuoni wanasema kwa mara ya kwanza maneno “mgongano wa masilahi” yaliingizwa kwenye Kamusi ya kisheria mwaka 1971, hivyo basi si ya muda mrefu lakini kwa msingi maalumu na kwamba kabla ya mwaka huo hakuna kamusi yoyote iliyokuwa na maneno hayo, kamusi iliyobobea (Black’s Law Dictionary), kwa mara ya kwanza yaliingizwa mwaka 1979.

Kwa mujibu wa Jaji Chande hata Kamusi ya Kiingereza-Kiswahili ya Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Toleo ya III, 2006, Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la 2014 ya Chuo Kikuu cha Oxford hazina maneno ‘mgongano wa masilahi’. 

Mji wa Basel, Uswisi ndiyo unaotajwa kuwa wa kwanza kutunga kanuni zinazohusu mgongano wa masilahi mwaka 1872, ambako ilimlazimu diwani kujitoa na kutopiga kura kwenye Baraza la Madiwani endepo suala lolote mbele yao litahusu masilahi ya mwenza wa diwani husika au familia yake.

Kwa hiyo, msingi wa mgongano wa masilahi si mtindo ambao unabadilika kila msimu, bali una nguzo yake imara na ni jambo la haki ya msingi katika uongozi, na utumishi wa umma.

Nini kifanyike? Ziko njia kadhaa za kusimamia, kuepukana, kupunguza na kudhibiti migongano ya masilahi, Mosi ni kuwepo na Sheria mama na kanuni za maadili na mienendo.

Sheria na Kanuni hizi huweza kutofautiana kati ya taasisi/taaluma moja na nyingine zake zinazodhibiti migongano ya masilahi.

Njia nyingine ni kutoa taarifa hadharani. Moja kati ya tiba inayokubalika duniani kote ya kuepuka migongano ya kimasilahi ni kueleza wazi kabla ya maamuzi au utekelezaji wa jukumu la umma kuwa una mgongano wa masilahi na jambo au shauri lililoko mbele yako kwa maamuzi, maelekezi au ushauri.

Panapotokea au kuwa na uwezekano wa kutokea mgongano wa masilahi unaopingana na hauendani na jukumu la umma, kujiuzulu ni mmoja ya njia ya kuepuka mgongano wa masilahi.

Njia ya nne ni kujitoa. Kwa kuwa kiongozi au mtumishi kwa kawaida ndiye wa kwanza kujua uwepo au uwezekano wa kutokea mgongano wa masilahi au hata kuambiwa kuwa itadhaniwa kuwa akishughulikia jambo kutakua na mgongano wa maslahi, njia inayopendekezwa na sheria na kanuni za maadili ni yeye kujitoa kwenye uamuzi au kikao cha maamuzi.

Kwa majaji na mahakimu kuna matakwa maalumu ya sheria ili kujitoa, na kutokana na kiapo chao na majukumu yao ya kutendaji haki, si kujitoa tu kilaini na kumruhusu mwenye shauri kutafuta mwamuzi anayemtaka yeye.

Kwa watumishi na wataalamu kwenye fani nyingine, kujitoa pia ni mwenendo bora japo wako wale ambao ni wazito wa kufanya hivyo! 

Njia ya kujivua hutumika pale panapokuwa na uwezekano na mgongano wa masilahi unaohusu jukumu la umma na biashara au masilahi binafsi yanayohusu fedha au mali.

Na njia ya mwisho ni haki ya kupata taarifa. Hii inatajwa kuwa ni miongoni mwa njia mpya za kuepuka migongano ya masilahi, inaelezwa kuwa mifumo inayowapa watu taarifa kwa wakati inasaidia kupunguza migongano ya masilahi kwa watu kupima wenyewe tararibu na namna maamuzi yanavyotolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles