24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mfundishe mtoto kushirikiana na watu


CHRISTIAN BWAYA

UMEWAHI kuona watu wasioweza kufanya kazi vizuri na watu? Hawa ni watu wanaoweza kuwa na uwezo mkubwa katika maeneo yao ya utaalam lakini hawajui kukaa vizuri na watu. Uzoefu unaonesha kuwa watu wa namna hii huwa hawafiki mbali kwa sababu bila kushirikiana na watu huwezi kufanya vingi.

Tunapozungumzia  kushirikiana tunamaanisha ule uwezo wa mtoto kuelewa watu wengine wanatarajia nini kwake. Mtoto mwenye ushirikiano na watu, ni mwepesi kutoa alichonacho, ni msikivu, hufanya kazi na wenzake, hucheza kwa ushirikiano na wenzake na huwa na uwezo wa kutafuta suluhu pale anapojikuta katika mazingira ya ugomvi.

Tabia ya kushirikiana na wengine ni tofauti kidogo na nidhamu. Nidhamu ni kufanya kile unachojua kinatarajiwa na wengine hata kama moyoni unaamini vinginevyo. Mfano, mtoto anapokwenda kulala kwa sababu anajua ni lazima afanye hivyo, hiyo ni nidhamu na si lazima iwe ushirikiano.

Ikiwa unataka mwanao awe na tabia ya kushirikiana na watu, ni muhimu uanze wewe kuwa mfano wa namna tunavyoweza kushirikiana na wengine. Kwa mfano, wape watu vitu mbele yake, shiriki kazi za ndani pale inapowezekana na onesha kuwapenda watu wengine wakiwamo rafiki zake. Kufanya hivyo kutakuza imani ndani ya mtoto kuwa katika maisha si rahisi mtu mmoja kufanya kila kitu bila msaada wa wengine.

Kadhalika, unapoongea naye tumia lugha inayoonesha kuelewa ‘dunia’ yake. Mtoto anayejisikia kueleweka, ni rahisi kuwa na ushirikiano. Kwahiyo, badala ya kupambana naye kwa ugomvi, jifunze kuwa mtulivu hata pale unapokuwa na hasira. Mtoto atajifunza kushirikiana na wewe.

Lakini pia, ni vizuri kuweka mazingira ya mtoto kuona faida za kushirikiana na wengine kwa kushiriki michezo yake. Kwa mfano, anapokuwa na changamoto ya kutatua kitu fulani, msaidie ili atumie muda mfupi zaidi. Tafsiri atakayoipata ni kuwa unapofanya kazi na watu wengine, unaokoa muda na unaweza kufanya vizuri zaidi.

Kadri inavyowezekana mshirikishe kazi zako ukihakikisha kuwa atapata faida ya moja kwa moja. Kwa mfano, anaweza kutegemea kuwa ifikapo saa fulani utamsomea kitabu. Lakini wewe unayo kazi ya kufanya usafi kabla ya muda huo. Mkaribishe akusaidie ili mmalize kwa wakati mpate muda wa kufanya kile anachokitarajia.

Aidha, ukiweza kutoa maelezo ya kirafiki, unaongeza uwezekano wa mtoto kushirikiana na wewe kuliko unapotoa amri. Kwa mfano, kama unataka akalale mapema ili awahi shule kesho asubuhi, kumwambia, ‘Zima TV nenda kalale!’ ni kumwamuru. Lakini unaweza kutumia lugha ya kirafiki, ‘Saa zimeenda na kesho utahitaji kuamka saa 12 ili uwahi gari la shule. Unaonaje ukalale?’ Lugha ya pili inakaribisha ushirikiano kuliko ya kwanza.

Sambamba na hilo, mpe fursa ya kuchagua. Mtoto anapokuwa na fursa ya kuchagua kipi afanye inamfanya ajisikie kuheshimika zaidi na hivyo anakuwa tayari kutoa ushirikiano. Mwekee mazingira ya kuchagua kipi anachopendelea zaidi na anapochagua kisicho bora mpe maelezo mepesi kumsaidia kutafakari uamuzi wake.


Vilevile ni muhimu kutambua jitihada wanazofanya watoto katika kushirikiana na wenzao. Mtoto anapoonesha ushirikiano na wengine, onesha kutambua jitihada zake. Anapowapa wenzake vitu, usijifanye hujaona. Tambua tabia hiyo na ipongeze. Unapomsifia unamfanya ajitahidi kuendelea kushirikiana na wenzake ili tu atambuliwe.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano,[email protected], 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles