29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Meli ya Korea Kaskazini yakamatwa

NEW YORK, MAREKANI

SERIKALI ya Marekani imetangaza kukamata meli ambayo ni mali ya Korea Kaskazini na kuilaumu kwa kukiuka vikwazo vya kimataifa dhidi ya taifa hilo ambalo limekuwa kwenye mgogoro kutokana na mpango wake wa kurutubisha silaha za nyuklia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Haki ya Marekani, meli hiyo ilitumika kusafirisha makaa ya     mawe ambayo ndiyo biashara kubwa ya taifa hilo licha ya kupigwa marufuku na Umoja wa Mataifa kuendelea kuyauza nje ya mipaka yake.

Aidha, imeelezwa kuwa meli hiyo imewahi kukamatwa nchini Indonesia Aprili mwaka 2018.

Hii ni mara ya kwanza Marekani kuikamata meli ya Korea Kaskazini kwa kukiuka vikwazo na hatua hiyo inajiri wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umedorora kupindukia.

Mkutano kati ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na rais wa Marekani, Donald Trump, uliisha bila makubaliano Februari mwaka huu huku Marekani ikiisisitizia Korea Kaskazini kusitisha mpango wake wa kinyuklia huku naye Kim Jong Un alisisitiza kuondolewa vikwazo.

Korea Kaskazini imetekeleza majaribio mawili ya makombora yake angani katika kipindi cha wiki moja katika kile kinachoonekana kuwa jaribio la kuishinikiza Marekani kufanya makubaliano.

Meli hiyo kwa jina The Wise Honest, ilikamatwa mara ya kwanza mwaka uliopita na Marekani ilitoa kibali cha kuikamata Julai 2018. Indonesia imeikabidhi Marekani meli hiyo na sasa inaelekea Marekani.

Maofisa wa Marekani wamesema kuwa tangazo hilo halitokani na majaribio ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini.

“Ofisi yetu iligundua mbinu ya Korea Kaskazini kuuza nje tani za makaa ya mawe ya kiwango cha juu kwa wanunuzi wa kigeni kwa kuficha asili ya meli, The Wise Honest,” alisema mwendesha mashtaka wa Marekani, Goeffrey S Berman.

“Mbinu hiyo iliifanya Korea Kaskazini kukwepa vikwazo na kwamba meli hiyo ilitumika kuingiza mashine nzito nchini Korea Kaskazini, ikiisaidia uwezo wa taifa hilo na kuendeleza msururu wa ukiukaji wa vikwazo,” aliongeza kiongozi huyo.

Malipo ya utunzaji wa Wise Honest yalidaiwa kufanywa nchini Marekani kupitia benki zisizojulikana hivyo basi kuipatia mamlaka ya Marekani fursa ya kuchukua hatua hiyo.

Korea Kaskazini imekumbwa na msururu wa vikwazo vya Marekani na vile vya kimataifa kutokana na hatua ya kutengeneza silaha za kinyuklia pamoja na majaribio ya silaha.

Hatua zilizochukuliwa na mataifa hayo mawili yanaelekeza kurudi kwa uhasama, lakini mjumbe maalumu wa Marekani kuhusu masuala ya Korea Kaskazini, Stephen Biegun, kwa sasa yuko Korea Kusini kujadiliana kuhusu njia za kuanza upya mazungumzo ya usitishwaji wa mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini.

Rais Trump amenukuliwa akisema kuwa: ”Hakuna mtu anayefurahia majaribio ya hivi karibuni ya Korea Kaskazini. Najua wanataka kujadiliana, wanazungumzia kuhusu majadiliano lakini sidhani kwamba wako tayari kujadiliana,” alisema.

Trump amekuwa rais wa kwanza aliyepo madarakani kukutana na mwenzake wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, wakati walipokutana Juni 12 mwaka 2018, lakini licha ya hayo na mkutano uliofuatia kumekuwa na hatua chache sana zilizopigwa katika kuhakikisha kuwa rasi hiyo ya Korea inaangamiza mipango ya kinyuklia.

Mwaka uliopita, Kim Jong Un, alisema kuwa atasitisha majaribio ya silaha za kinyuklia na kwamba hatafanya tena majaribio ya makombora ya masafa marefu yanayoweza kufika katika bara jingine lakini mipango yake ya kinyuklia inaonekana ikiendelea.

Mojawapo ya matokeo ya mazungumzo yao, juhudi za pamoja za kutoa mabaki ya wanajeshi wa Marekani waliouawa wakati wa vita ya Korea zimesitishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles