28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge kuwasilisha hoja binafsi lugha ya kufundishia

TIGANYA VINCENT, TABORA

MBUNGE wa Tabora Kaskazini,  Almas Maige (CCM), amesema wakati umefika kwa Watanzania kuanza kutumia   Kiswahili kwa ajili ya kufundishia katika shule za sekondari na elimu ya juu kwa masomo yote.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha vijana wengine kuelewa wanachofundishwa na kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.

Maige alisema hayo jana mjini Tabora alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hoja yake aliyoiwasilisha bungeni  kutaka Kiswahili kitumike kama lugha ya kifundishia na kujifunza katika shule za sekondari na vyuo  nchini.

Alisema utafiti uliofanywa na wataalamu na wanazuoni mbalimbali umeonyesha  asilimia 50 ya wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa kutokana na matumizi ya Kiingereza.

Maige alisema hata wanavyuo vya ufundi wanaofundishwa kwa   Kiingereza wanapomaliza masomo yao wanapokuwa kazini hawatumii lugha hiyo katika kutekeleza  majukumu yao ya kila siku bali wanatumia Kiswahili.

Mbunge huyo wa Tabora Kaskazini alisema   tayari maandalizi ya vitabu vya kufundishia kidato cha kwanza kwa masomo yote vimekamilika pamoja na kamusi kubwa ya tafsiri wa maeneo yote ya Kiswahili iko tayari.

Alisema  wataalamu walioandika vitabu hivyo wanasema ikiwa Kiswahili kitaanza kutumia wako tayari kuandaa na vitabu vya kidato cha pili na kuendelea kwa muda mfupi na wanafunzi waanze kuvitumia.

Maige alisisitiza kuwa kwa juhudi hizo za wataalamu hakuna sababu ya kuendelea kutumia lugha ambayo baadhi ya wanafunzi  hawaelewi wanachofundishwa.

Alisema  hata wananchi wamekuwa wakizielewa zaidi hotuba za Rais Dk. John Magufuli na mijadala ya vikao vya Bunge kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili.

Maige alisisitiza kuwa wakati umefika wa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa moyo wake aliouonyesha wa kukiimarisha Kiswahili ndani na nje ya Tanzania  anapohutubia mikutano mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles