31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa ataja sababu idadi ndogo ya watalii

 AZIZA MASOUD – Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu,Kassim Majaliwa amesema idadi ya watalii inayoingia nchini ni ndogo ukilinganisha na vivutio vilivyopo nchini.

Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali inajipanga kuwaongeza ili wafike milioni mbili kwa mwaka 2020 kutoka milioni 1.3 wanaowasili kwa mwaka.

Akizungumza Dares Salaam jana wakati wa uzinduzi wa chaneli ya utalii ya Tanzania Safari Channel uliofanyika katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), alisema uchache wa watalii wanaoingia nchini umetokana na sababu mbalimbali ikiwamo kasi ndogo ya kujitangaza kimataifa.

 “Licha ya mafanikio tunayoyapata, lakini hatupaswi kuridhika nayo kwa sababu Tanzania inapokea watalii milioni 1.3 kwa mwaka wakati Misri na Afrika Kusini hupokea zaidi ya watalii milioni 10.

“Lazima tujiulize ni kwanini sisi tulio na vivutio vingi kuanzia Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Ruaha, Sadani (Hifadhi pekee iliyopakana na bahari), Zanzibar ambako kuna fukwe maridadi, malikale,maporomoko ya maji na vingine vingi na baadhi ya hivi vivutio vimewekwa katika kundi la maajabu ya dunia tunapata watalii wachache,” alisema Majaliwa.

Alisema sekta ya utalii ni muhimu kwa kuwa inaiingizia nchi Dola za Marekani bilioni 2.3 sawa na Sh trilioni 5.04 kwa mwaka na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 1.5 wanaojihusisha katika shughuli mbalimbali zikiwamo usafiri wa ndani kwa watalii, uongozaji watalii katikamaeneo yenye vivutio, kuuza bidhaa kwa watalii kama vyakula, vinywaji, vinyago,nguo na zawadi.

Kuhusu chaneli hiyo, aliwataka watu wotewaliopewa dhamana ya kuiendesha wahakikishe wanazingatia viwango vya kimataifa katika vipindi watakavyokuwa wanaviandaa. 

 “Vipindi vyenu ni lazima vivutie kama vile tunavyoviangalia katika chaneli za wanyama za kimataifa kamavile National Geographic, Discovery, Travel na nyingine ili lengo lililokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwake litimie,” alisema.

Pia alisema Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizotenga moja yatatu ya eneo lote la nchi kwa uhifadhi na kuna tamaduni za makabila mbalimbali,ngoma za kuvutia, vyakula vya asili, sinema za maisha yetu na lugha adhimu ya Kiswahili.


“Hivyo kwa kuanzishwa kwa chaneli hii inayotengeneza vipindi na kuonesha vivutio hivi ndani na nje ya Tanzania, itasaidia watalii huko waliko kujua huu utajiri wetu na kuchagua kuja kutalii nchini,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisisitiza kuhusu uboreshwaji wa bustani katika barabara inayotokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, asimamie jambo hilona matangazo yanayowekwa yaoneshe vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, alisema Watanzania wanaona wizara hiyo haitangazi utalii kutokana na uchache wa watalii wanaoingia nchini, lakini sekta hiyo inachangia asilimia17.6 ya pato la taifa.

Alisema wizara yake inafanya jitihada za kuimarisha masoko na kutangaza utalii ndani na nje ya nchi na kuwa Tanzania  inaanza kuwatumia wasanii na amewataka kutumia vivutio vya utalii kurekodia filamu zao.

 “Nimetoa ofa kwa wasaniiwote wanaotaka kutengeza filamu ama video za nyimbo zao katika maeneo ya utalii wanione mimi moja kwa moja nitawapa vibali ili na wao watangaze vivutio vyetu,”alisema.

Uzinduzi wa chaneli hiyo ni utekelezwaji wa maagizo ya Rais Dk.John Magufuli aliyoyatoa Mei 16, mwaka jana alipotembea TBC, kuwa pamoja namambo mengine aliwataka waangalie uwezekano wa kuanzisha chaneli itakayotangaza hifadhi na vivutio vya utalii nchini.

Pia uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 29 iliyoielekeza Serikali kuweka mkakati wa kimataifa wa utangazaji wa utalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi.

Chaneli hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano wa wizara nne na taasisi zake zikiwemo Maliasili na Utalii, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Mamboya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles