23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Maiti yafukuliwa, yafanyiwa unyama

*Ni binti wa miaka 35, kaburi lake labomolewa usiku na watu wasiojulikana, mwili wake wavuliwa nguo, ndugu wadai umeingiliwa kimwili, polisi waanza uchunguzi

AGATHA CHARLES Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwili wa aliyekuwa Ofisa wa Wizara ya Nishati, marehemu Mary Maramo (35), uliokuwa umezikwa katika makaburi ya Pugu Mwakanga jijini Dar es Salaam, umekutwa ukiwa umetolewa nje ya kaburi na kisha kuvuliwa nguo.

Sintofahamu hiyo inadaiwa kufanywa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana, ambapo kaburi lake lililokuwa limejengewa baada ya kuzikwa juzi lilivunjwa pembeni na hivyo kupata upenyo wa kutoa sanduku lililokuwa na mwili wake.

Mtu wa kwanza kubaini tukio hilo jana asubuhi ni mmoja wa wachimba makaburi ambaye alifika eneo hilo kwa ajili ya kumwagia maji lakini alishangazwa na kukuta mwili wa Mary ukiwa nje na kaburi lake limevunjwa hali iliyomlazimu kuwapigia simu familia ya Mary ambayo ilifika muda mfupi baadaye.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika makaburini hapo jana, kaka wa marehemu Mary, Deogratius Maramo, alisema inadaiwa mwili huo uliingiliwa kimwili lakini walitegemea zaidi majibu kutoka kwa wataalamu wa uchunguzi na polisi.

Alisema alimsikia Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa huo akisema kuwa hilo ni tukio la kwanza kufanyika katika eneo hilo na kwamba linahusishwa na ushirikina.

Alisema alipata taarifa kuwa mwili wa dada yake uliwekwa nje ya kaburi na kuachwa mapaja yakiwa yamechanuliwa.

Maramo pia alisema walishangaa na kusikitishwa na kitendo hicho kwani kimewadhalilisha na hakifai.

Mmoja wa wanafamilia ambaye alizungumza na gazeti hili na kuomba kuhifadhiwa jina lake, alisema taarifa za kuvunjwa kwa kaburi la Mary alizipata jana asubuhi.

“Jana (juzi) tulizika, nikalala msibani, asubuhi wakati watu wanakwenda makaburini kusali mimi niliondoka kwa kuwa hakukuwa na mtu nyumbani. Sasa waliokwenda makaburini ndio waliopiga simu kueleza nini kimetokea,” alisema mwanafamilia huyo.

Alisema awali Mary ilikuwa azikwe katika makaburi ya Air wings alikozikwa baba yake miaka kama mitatu iliyopita lakini ilishindikana baada ya kuambiwa kumejaa.

Mwanafamilia huyo alisema Mary ambaye alifariki akiwa jijini Dodoma alikokuwa amehamishiwa kikazi, alifariki baada ya kuugua kwa muda wa takribani wiki mbili ambako alizidiwa na kuwekwa chumba cha uangalizi maalumu.

Alisema Wizara aliyokuwa akifanyia kazi ndiyo iliyohusika kusafirisha mwili wa marehemu kuuleta Ukonga, ambako ndiko nyumbani kwao kwa ajili ya taratibu za maziko.

Mwangalizi wa makaburi hayo Mzee Hela, alisema tukio hilo ni mara ya kwanza kutokea na kulitaja kuwa ni la kinyama na aibu.

“Ni imani potofu, mtu hawezi kufanya hilo akiwa na akili timamu,” alisema Mzee Hela.

POLISI

Tukio hilo lililazimisha Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kisha kulitolea ufafanuzi na kueleza hatua ilizochukua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana saa 11 jioni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Kamishna Msaidizi, Zuberi Chembera, alisema taarifa za kufukuliwa kwa mwili huo ziliripotiwa  jana saa moja asubuhi na fundi wa  kaburi hilo katika Kituo cha Polisi cha Staki Shari.

“Taarifa hizo nilizipata kupitia Kituo cha Polisi cha Staki Shari saa moja asubuhi wakati fundi ambaye anashughulikia kaburi alienda kwa ajili ya kumwagia maji baada ya kaburi kuwa limejengwa jana (juzi) na alipofika akakuta tukio hilo,” alisema Kamanda Chembera.

Alisema kwa mujibu wa ndugu wa marehemu Mary alifariki Aprili 8, 2019  mkoani Dodoma na baadaye mwili wake uliletwa Dar es Salaam  kwa ajili ya mazishi ambayo yalifanyika juzi saa 11 jioni.

“Mara baada  ya mazishi ndugu wakatawanyika lakini  leo (jana) ambapo fundi aliyejenga kaburi jana (juzi) alienda kwa ajili ya kulimwagia maji  ili zege ishike vizuri akakuta upande wa chini wa lile kaburi tofali zilikuwa zimevunjwa na mwili wa marehemu umetolewa nje nusu upo ndani nusu nje,” alisema Kamanda Chembera.

Alisema baada ya polisi kufika eneo hilo wakiwa na ndugu walifanya uchunguzi wa awali ambapo mwili huo ulikutwa  ukiwa hauna kasoro yoyote.

“Uchunguzi wa awali tulioufanya pale makaburini kwa kushirikiana na ndugu ulionyesha kuwa wahalifu waliofukua maiti hiyo hawakuchukua kiungo chochote, lakini walikuwa wameuvua nguo ambayo alikuwa amezikiwa nayo na ndugu waliokuwepo walithibitisha hilo,” alisema Kamanda Chembera.

Akizungumzia kuhusu taarifa za kwamba mwili huo uliingiliwa kimwili, Kamanda Chembera alisema hawezi kuthibitisha kwa kuwa suala hilo ni uchunguzi wa kitaalamu na kwamba kutafanyika uchunguzi zaidi.

“Kuingiliwa kimwili hatuwezi kuthibitisha kwa sababu ni uchunguzi wa kitaalamu pale tutakaposhirikiana na ndugu wa marehemu kufanya uchunguzi zaidi wakisayansi ama tukimkamata mtuhumiwa akakiri  hilo tunaweza kuliongelea,” alisema Kamanda Chembera.

 Alipoulizwa kama ndugu wamesharidhia kuhusu kufanyika kwa uchunguzi wa mwili huo  ili kubaini tukio hilo, alisema kuwa kwa jana ndugu hawakuwa tayari badala yake waliamuru mwili ule uzikwe kwa mara ya pili katika kaburi lile lile.

“Baada ya majadiliano kati ya ndugu wa marehemu na polisi waliokagua kaburi, kuhusu uchunguzi process (taratibu) za uchunguzi kwa miili iliyozikwa ni ndefu kwa sababu lazima uende mahakamani uombe kibali na mahakama itakapotoa kibali ndipo daktari baada ya kuona kibali cha mahakama tutakuwa tayari kufanya uchunguzi wa mwili na hautachukua muda mrefu,” alisema Kamanda Chembera.

Alisema polisi inaendelea na uchunguzi kwa kuwa pamoja na kwamba mwili umekutwa umetolewa na wahalifu, lakini bado wanaamini umetolewa kinyume cha sheria.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,636FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles