27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mabingwa wa upasuaji ubongo kutoka China ‘watua’ MOI

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MADAKTARI bingwa watatu wa upasuaji ubongo na mishipa ya fahamu pamoja na magonjwa ya ndani wa Chuo Kikuu cha Kimataifa na Hospitali ya Peking, nchini China kwa mara ya kwanza wametua nchini katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface alisema huo ni mwanzo wa ushirikiano na kwamba lengo ni kuimarisha ubingwa wa ndani ili kuendelea kusaidia watanzania.

“Tumepokea ugeni wa mabigwa kutoka China, watarejea kwao Februari 26, mwaka huu, lengo hasa ni kushirikiano nao katika kujenga uwezo wetu wa ndani,” alisema.

Dk. Boniface alisema kulingana na sensa ya watu na makazi inakadiriwa watanzania wapo takriban milioni 50 lakini mabingwa wa upasuaji ubongo wa ndani waliopo nchi nzima ni wanane pekee.

“Tuna uhaba mkubwa wa wataalam ili kutosheleza mahitaji inahitaji wawe angalau 200, hapa MOI wapo watatu tu, na kwa siku katika kliniki yetu tunaona wagonjwa wapatao 500 hadi 600.

“Kwa wastani daktari mmoja hapa MOI anaona wagonjwa wapatao 30 kati ya hao, watatu huwa ni wanaohitaji upasuaji wa ubongo, hii ni kazi ya kujitolea tunafanya wakati mwingine hadi muda wa ziada, hatuwezi kuwaacha wagonjwa, tunapata muda wa kupumzika, pindi tunapomaliza kliniki,” alisema.

Alisema tayari wameshaandaa wagonjwa wanne watakaofanyiwa upasuaji na mabingwa hao siku ya jumatatu (Februari 25,mwaka huu).

Alisema pamoja na uhaba wa wataalam bado pia wanakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba ili kuweza kutosheleza mahitaji.

“Ndiyo maana tunaona ujio wao ni mwanzo wa ushirikiano mzuri kwani kwa wataalam tulionao wataweza kupata ujuzi zaidi utakaosaidia kuboresha huduma ya afya kwa watanzania,” alisema Dk. Boniface.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru, alisema ndani ya ushirikiano huo mabingwa wa chuo hicho watakuwa wakija nchini na mabingwa wa ndani watapata fursa ya kwenda China kujifunza zaidi.

“Ushirikiano huu tuliuanza rasmi mwaka jana baada ya Rais John Magufuli kutuagiza twende katika hospitali hii huko China, tulikwenda mapema April, mwaka jana.

“Tulikubaliana wataalam wao waje nchini kushirikiana nasi lakini pia wataalamu wetu watakuwa wanakwenda nchini mwao kujifunza zaidi,” alisema.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo wa Chuo Kikuu cha Kimataifa na Hospitali ya Peking, Profesa Yuanli Zhao alisema pindi watakaporejea nchini mwao wataishawishi serikali yao kusaidia upatikanaji wa baadhi ya vifaa tiba ili kuiongezea nguvu MOI.

“Ni mara yangu ya kwanza kuwapo Tanzania, nina matumaini makubwa kwamba ushirikiano kati yetu utakuwa wa manufaa zaidi kwa watanzania,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles