28.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 2, 2021

Mabeberu hawataki uzalendo wa Rais Magufuli?

MWANDISHI MAALUMU

NIMEKUWA najiuliza, kwanini Tanzania imeshambuliwa kwa kiasi kikubwa kutoka mataifa ya nje ambayo yana uchumi mkubwa? Nimejiuliza kwanini Rais wa Tanzania, John Magufuli, anashambuliwa mno kipindi hiki katikati ya jitihada zake za kuiletea maendeleo nchi yake pamoja na kupigania rasilimali ambazo ni halali yetu?

Licha ya juhudi hizo, bado mataifa ya nje, yakiwamo Marekani na yale ya Jumuiya ya Ulaya (European Union) yanailima barua Tanzania? Nikajiuliza kwanini Tanzania na si Cameroon?

Na swali kubwa likarejea, ni kwanini uongozi wa Rais John Magufuli ushambuliwe hivi na si mwenzake, Paul Biya wa Cameroon, ambaye anaongoza nchi akiwa anaishi Ulaya huko huko?

Cameroon chini ya Rais Paul Biya aliyedumu madarakani kwa takribani miaka 37 sasa na Cameroon iliyo na matatizo lukuki ya ndani tumeshuhudia jeshi likiwapiga wafuasi wa upinzani na kuua watu kinyama barabarani mwezi Oktoba mwaka jana, mauaji ya kutisha yalifanyika lakini hakuna hatua zinazochukuliwa kwa Paul Biya na serikali yake.

Mnamo Desemba 5 mwaka jana tuliona serikali ya Marekani ikipeleka msaada wa dola bilioni 27 nchini Cameroon, licha ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kutokuwapo na mabadiliko ya kisiasa, kwani Rais Biya yupo madarakani kwa miaka 37.

Tumeona namna Tanzania ikipigiwa kelele na mataifa makubwa ya Magharibi na matamko yakitolewa huku na kule na vitisho juu.

Mnamo Novemba 2016, Bunge liliishauri serikali isijiunge na mkataba wa EPA na serikali ilikataa kujiunga na EPA, lakini Jumuiya ya EU ikaja juu na kutoa vitisho mbalimbali, lakini serikali ilisimamia msimamo wake.

Baadaye EU wakawaomba Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Uhuru Kenyatta wa Kenya wamshauri Rais John Magufuli asaini mkataba kandamizi wa EPA. Licha ya ushawishi wa Rais Museveni, lakini Magufuli hadi sasa hajasaini.

Mkataba wa EPA ni mkataba wa ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi za Ulaya na Afrika Mashariki, lakini kwa sisi tutabaki kuwa ‘importers’ tu kuwanufaisha Ulaya na viwanda vyetu vitakufa na hata ndoto ya viwanda itakufa.

Rais Magufuli na Paul Kagame wa Rwanda walipiga marufuku uingizaji wa nguo za mitumba, tukaona Serikali ya Marekani ikija juu na kutishia kuiwekea vikwazo Tanzania, baadaye Serikali ya Tanzania ikalegeza.

Suala la sampuli za madini lilivyokuwa limeshikiliwa na Rais wa Tanzania kiukweli, iliwagusa mabeberu kwa kiasi kikubwa, ukizingatia dhahabu ni moja ya vyanzo muhimu vya mapato kwa Marekani na nchi za Ulaya.

Kutetereka kwa kampuni kubwa ya madini ya hawa wakubwa lazima wawatetee wafanyabiashara wao. Je, hawa mabwana wapo thabiti kweli na haki za binadamu zinazodaiwa kuvunjwa Tanzania au wanatafuta kumaliza hasira zao baada ya kuguswa maeneo nyeti na serikali?

Ndiyo maana ninatolea mfano nchi kama Cameroon chini ya Rais Biya, mbona haishambuliwi kama Rais wa Tanzania? Tuachane na mawazo ya kibeberu na vitendo vyao vya dhuluma dhidi ya mataifa madogo kama Tanzania na mengine. Ni lazima tuwe wazalendo. Huu uzalendo wa Rais Magufuli umekuwa mwiba kwa mabeberu.

Tunatakiwa kupambana sisi wenyewe tu kama vile babu zetu walivyopigania uhuru wa nchi, hakuna beberu aliyekuja kufanya ukombozi Afrika.

Kama wazee wetu ndio waliotuletea uhuru, basi nasi tunao wajibu wa kupigania rasilimali zetu. Hivyo basi hakuna yeyote atakayekuja kufanya ukombozi wa uchumi Afrika isipokuwa sisi wenyewe na wazalendo kama Rais Magufuli na wengineo.

Mabeberu siku zote wanapenda Afrika na Latin America iwe ni dampo la bidhaa zao na kunyonya maliasili za nchi za mabara haya kwa kuwarubuni viongozi kwa mikataba mibovu na kisha kuja kutoa fedha kwa mgongo wa msaada.

Ukiukwaji wa haki za binadamu kama Marekani na Ulaya wanavyosema, mbona Misri hakuna haki za mashoga na wasagaji na ni kosa la jinai kufanya ushoga na sheria zao ni kandamizi, kifungo ni maisha jela, mbona hatusikii wakitolewa kauli na wakilaaniwa kwa kuminya haki za binadamu na kila mwaka Marekani hupeleka pesa Misri kuchangia bajeti.

Kwanini Tanzania na si Misri? Kimsingi utajua ni hatua kali za Rais John Magufuli ya kufanya mapinduzi ya uchumi na kutetetea rasilimali zetu dhidi ya mabeberu.

Ipo siku Tanzania na Afrika kwa ujumla itakuwa huru kiuchumi, hata Mao Tsetung alivyofanya mapinduzi China alikumbana na misukosuko na vita kutoka kwa mabeberu lakini mwisho wa siku China imesimama na kuwa nchi iliyopiga hatua kubwa kiuchumi, kiteknolojia na viwanda.

Kwenye kila mapinduzi lazima changamoto na kupigwa vita kuwepo kwa njia na mbinu mbalimbali, hata kulazimisha mabadiliko ya kisiasa kwa kuzimega na kuchocheza siasa za nchi ziwe za vurugu badala ya kukuza uchumi. Kwa vurugu za Cameroon, pale wanatafuta nini kingine zaidi ya kuendelea kuona hali ile huku maendeleo ya kiuchumi yakiwa dhaifu?

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,646FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles