25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif abakisha saa chache CUF

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WAKATI Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kikiendelea na vikao vya uchaguzi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, amebakisha saa chache kuondolewa katika nafasi hiyo.

Hatua hiyo inatokana na chama hicho kuwa katika mgogoro wa ndani kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Kutokana na hali hiyo, inaonekana wazi kwamba sasa Maalim Seif ameondolewa rasmi kushika nafasi hiyo.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Abdul Kambaya, alisema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake, hatua inayofuata ni kuchaguliwa kwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi na hadi tunakwenda mitamboni uchaguzi huo ulikukuwa ukiendelea.

Kambaya alisema kutokana na mabadiliko ya katiba ya chama hicho, kwa sasa katibu mkuu atateuliwa na mwenyekiti na wajumbe wa bara watapiga kura kukubali ama kukataa.

Alisema kikao hicho kitafanyika leo na katibu mkuu mpya atajulikana.

“Hii inatokana na mabadiliko ya katiba ya chama yaliyofanywa na mkutano huu, ambapo tayari tumeshapata mwenyekiti na makamu wake na kesho (leo) sasa atajulikana nani katibu mkuu na manaibu wake wawili.

“Waliofikiri wanaweza kuyumbisha chama sasa umma umewatambua na wajumbe wa mkutano mkuu wamefanya maamuzi wao.

 “Hii sasa inakwenda kuonesha kwamba sasa CUF imezaliwa upya licha ya dhoruba kadhaa za baadhi ya watu ambao walikuwa wakihangaika huku na kule kwa lengo la kutaka kukiuza chama,” alisema Kambaya.

Alipoulizwa ni nani anatarajiwa kuwa katibu mkuu, alisema CUF ina wanachama wengi wenye sifa za kuongoza chama zaidi ya Maalim Seif kwani kwa muda mrefu alisusa kufanya kazi za chama, hivyo alishajivua mwenyewe katika nafasi yake kwa mujibu wa katiba.

“Unakumbuka mwenyekiti (Lipumba) kila mara alimtaka aje ofisini ampangie kazi, lakini alikaidi na badala yake amekuwa akitumia vikundi vya watu ili kuleta vurugu. CUF ni taasisi si mtu, mwanachama yeyote maadamu ana sifa anaweza kuongoza,” alisema.

LIPUMBA ACHAGULIWA

Akitangaza matokeo ya uchaguzi wa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Thinei Juma Mohamed, alisema Profesa Lipumba amechaguliwa tena kuiongoza CUF kwa kupata kura 516.

Wagombea wengine katika nafasi hiyo ya mwenyekiti, Diana Simba alipata kura 16 wakati Zuberi Hamisi alipata 36.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar alichaguliwa Abbas Juma Mhunzi kwa kura 349, wakati Makamu Mwenyekiti Bara alichaguliwa Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma kwa kura 231.

RAFU ZATAWALA

Wakati uchaguzi ukiendelea viliokotwa vipeperushi ndani ya ukumbi vyenye majina ya watu wanaodaiwa kuwa ndio wanaopaswa kuchaguliwa.

Tukio hilo lilitokea wakati wa uchaguzi wa makamu mwenyekiti upande wa Zanzibar.

Mmoja wa viongozi wa Kamati ya Uchaguzi alisimama na kuwaonesha wajumbe mojawapo ya kipeperushi kilichookotwa na kusema kuwa ni feki, hivyo kipuuzwe.

“Kamati ya Uchaguzi haijaandaa kitu kama hiki, ieleweke vipeperushi hivi ni feki na hatuhusiki navyo kama kamati,” alisema kiongozi huyo.

Aidha kuna wakati wajumbe walisikika wakiwakejeli baadhi ya wagombea waliokuwa wakijinadi na kusababisha meza kuu kuingilia kati mara kwa mara kuwasihi wawe watulivu kumsikiliza kila mgombea.

Mgombea aliyekumbana na kadhia hiyo ni Diana aliyekuwa akigombea nafasi ya uenyekiti ambayo alijikuta katika wakati mgumu kutokana na aina ya maswali aliyokuwa akiulizwa.

Elimu, uzoefu ndani ya chama na nchi alizowahi kutembelea ni kati ya maswali yaliyoelekezwa kwa mgombea huyo na alipokuwa akijibu baadhi ya wajumbe walisikika wakimkejeli.

“Ndugu mgombea nafasi unayogombea ni kubwa na inahitaji mtu mzoefu, hebu tutajie nchi ulizowahi kutembelea,” aliuliza mmoja wa wajumbe.

Akijibu, Diana alisema alijiunga na chama mwaka 2017 na amefanikiwa kutembelea Kenya na Uganda.

“Msifikiri Profesa Lipumba ndiye msomi peke yake, hata mimi ni msomi. Nina Stashahada ya Maendeleo ya Jamii, hivyo nina uwezo wa kuwaongoza,” alisema Diana.

AKIDI YA MKUTANO

Suala jingine lililoibua mjadala katika uchaguzi huo ni akidi ya wajumbe baada ya baadhi yao kudai kuwa kuna watu wameongezeka na hawapaswi kupiga kura.

Asubuhi wajumbe walitangaziwa kuwa akidi ya mkutano ni wajumbe 798, lakini haikufafanuliwa kama wote wanapiga kura.

Hatua hiyo ilimlazimu Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya kutoa ufafanuzi kuondoa mkanganyiko uliokuwa umejitokeza.

“Wajumbe waliopo ni 598, wengine ni wale wasiopiga kura, ni waalikwa kwa nafasi mbalimbali,” alisema Sakaya.

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, wajumbe walikuwa wakiendelea na uchaguzi wa wajumbe wa baraza.

MIKAKATI BAADA YA UCHAGUZI

Akizungumza baada ya matokeo hayo, Profesa Lipumba alisema wamejipanga kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

“Sitaki kusikia kuna kijiji, kitongoji au mtaa tunakosa mgombea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na 2020 tuunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF,” alisema Lipumba.

Naye Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Mhunzi alisema chama kilikuwa kina hali mbaya, hakifahamiki kinakwenda wapi na kuahidi kushirikiana na wenzake kukiendeleza.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti Bara, Maftah alisema wataboresha jumuiya zote za chama zikiwemo za vijana na wanawake kuhakikisha zinakuwa na nguvu kuliko vyama vingine.

MHUNZI NI NANI

Abass Juma Mhunzi ni mwanasiasa wa muda mrefu ndani ya CUF ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti mpya wa chama hicho upande wa Zanzibar.

Alikuwa Mwakilishi wa Jimbo la Chambani kisiwani Pemba, na alipata umaarufu mkubwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi kutokana na misimamo yake ya kupinga matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Tuhuma dhidi yake ziliibuka baada ya kutoa ushauri kwa wawakilishi wenzake akiwataka kuitambua Serikali.

Katika kipindi chake cha uwakilishi, aliwahi kukumbana na matatizo mengi, likiwemo la kufikishana mahakamani na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho baada ya kupewa adhabu ya kutohudhuria katika vikao kwa mwaka mzima.

Adhabu hiyo ilitolewa baada ya Mhunzi kukataa kuomba radhi baraza kutokana na matamshi yake ya kusema bei za mafuta zinapangwa Ikulu.

Katika kadhia hiyo, Spika Kificho alimwamuru Mhunzi kutohudhuria vikao kwa mwaka mzima, lakini mwakilishi huyo alipinga mahakamani na kushinda kesi na kulipwa haki zake kwa mwaka mzima.

Hata hivyo Mhunzi pia aliwataka wawakilishi wenzake wa kambi ya upinzani kubadili mwelekeo na kuitambua SMZ iliyo chini ya Rais Amani Abeid Karume.

Mwaka 2009, alijizulu ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kile kilichoelezwa kuwa na misimamo mikali dhidi ya katibu mkuu wake Maalim Seif jambo lililosababisha kubwagwa katika ujumbe wa Baraza Kuu la Uongozi katika uchaguzi wa ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles