24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Lukuvi asema Tanzania kutoka juu

WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  Makazi, William Lukuvi, amesema chanzo cha baadhi ya nchi wahisani kugomea kutoa misaada kwa Tanzania kunatokana na msimamo wa Rais Dk. John Magufuli kuhusu kulinda rasilimali za nchi.

Kwa mujibu wa Lukuvi msimamo huo haujazifurahisha nchi hizo na kuamua kuweka masharti magumu katika misaada yao kwa Tanzania.

Waziri Lukuvi, alitoa kauli hiyo usiku wa kuamkia jana, wakati wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpya  wa 2019, uliofanyika Kariakoo, Dar es Salaam ambapo alimwakilisha Rais Magufuli.

Waziri Lukuvi, alisema pamoja na hali hiyo, bado Serikali imeendelea kuwa imara na kuhakikisha inakusanya kodi za ndani ili kuweza kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya umeme wa maji wa Rufiji (Stiegler’s Gorge).  

“Leo (jana) tupo kwenye mkesha hapa, hakika nawaomba endeleeni kumwombea kwa dhati Rais Magufuli ili Mungu azidi kumpa nguvu na baraka za kuliongoza Taifa letu.

“Mnakumbuka hivi karibuni Tanzania kupitia Bunge, ilipitisha sheria ya kulinda rasilimali zetu za nchi (Sheria ya Madini ya mwaka 2017),baada ya kuanza kutumika mabwana wakubwa (wahisani) imewauma, sasa tunahitaji kujenga nchi inayokwenda kwa kasi kwa maendeleo na leo haya yote yanaonekana chini ya Rais Magufuli,” alisema Lukuvi.

Alisema pamoja na misimamo ya wahisani, bado Taifa linaendelea kupiga hatua kwa kasi ikiwamo kujenga miradi mkubwa kama wa reli ya kisasa (SGR).

Akizungumzia kero ya maji, alisema kwa sasa utekelezaji wa miradi ya maji kwa wananchi hali imekuwa ni nzuri huku lengo la Serikali ni kutaka kuona Watanzania wote wanapata huduma hiyo wakati wote.

Licha ya hali hiyo, alisema amekuwa akifanya mambo mengi makubwa  ambapo alitangaza kuanzia jana halmashauri zote zitaanza kutoa leseni za makazi kwa waliojenga kwenye maeneo ambayo hayajapangwa.

“Kuanzia kesho (jana) halmashauri zote ninaziagiza zianze kutoa leseni za makazi kwa wale waliojenga kwenye maeneo ambayo hajapimwa. Leseni hizo zitakuwa za miaka mitano na baada ya muda maeneo hayo yatapimwa na kupewa leseni. Lakini hata ukipewa leseni nenda kalipe kodi ya ardhi.

“Nami ninaawaambia Watanzania endeleeni kumwombea Rais Magufuli, maana hata sisi wasaidizi wake tumekuwa tukipata faraja kutokana na namna kiongozi wetu  anavyojitoa kwa ajili ya Watanzania.

“Tangu tumeingia madarakani, pale wizara ya ardhi hakuna migogoro mipya zaidi ile ya zamani ambayo ilikuwa inatengenezwa na watu wachache kwa masilahi yao.

“Tumuunge mkono Rais Magufuli tunataka nini, kila siku amekuwa akiweka mambo sawa sasa wafanyabiashara nchi nzima wamepewa vitambulisho aliyetenegeza ni Rais Magufuli twendeni tumuunge mkono kiongozi wetu kwa ajili ya Taifa letu,” alisema.

Akijibu hoja ya kuzuiwa kufanya maombi  Uwanja wa Taifa, Lukuvi alisema analichukua suala hilo na kulifikisha kwa Waziri wa Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk. Harrison Mwakyembe.

Awali akiendesha dua maalumu kwenye mkesha huo ,mwenyekiti wa mkesha mkubwa kitaifa, Askofu Dk. Godfrey Malassy wa Tanzania Fellowship of Churches, alishukuru serikali kwa upendo wake kwa Watanzania.

Pamoja na hali hiyo, waliwaombea viongozo mbalimbali, ikiwamo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai pamoja na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma.

Wengine waliombewa kwenye mkesha huo mawaziri, wabunge, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya, viongozi wa dini pamoja na Watanzania wote.

“Sisi wote kama Watanzania tunaamini kwamba, mwaka huu mpya wa 2019 utakuwa ni mwendelezo wa mahusiano, mshikamano na mashirikiano mema na chanya ambayo tumekuwa nayo kwa zaidi ya miaka 57 ya Uhuru wetu.

“Tuendelee kudumisha tunu zetu za Taifa ambazo ni amani, utulivu na uzalendo ili sote tuwe na ustawi na maendeleo chanya vizazi hata vizazi.

“Tunawatakia kila la heri Watanzania kila mmoja wetu kwa nafasi yake tusiache kushirikiana kwa kuwa kwa kila mtu kuna kitu cha thamani Mungu amekiweka na kutufanya tetegemeane.

“Watanzania, Sisi tunaweza kufanya mambo makubwa ya kuigwa na ulimwengu mzima kwa uwezo wa Mungu, juhudi, uzalendo na bidii katika kufanya kazi kwa weledi tukiongozwa na maono, hekima na busara za viongozi wetu wote na Serikali yetu makini,” alisema.

ASKOFU RUWA’CHI NA AMANI

ASKOFU Mkuu Mwandamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Thadeus Ruwa’ichi, amewataka waumini wa dhehebu hilo kuutumia mwaka 2019, kudumisha amani na kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Alisema hayo katika misa takatifu ya mkesha wa mwaka mpya iliyofanyika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana.

Alisema maana halisi ya amani ni mtu kuwa na uhusiano mzuri na jirani yake na kwamba mtu asiulize jirani yake amemtendea nini ili naye ampende.

“Kazi ya mwisho ya amani ni kudumisha uhusiano kati ya binadamu na Mungu ambaye alitupatanisha na mwanae wa pekee Yesu Kristo,” alisema Askofu Ruwa’ichi.

Aliwataka waumini wa dhehebu hilo kuhakikisha wanakuwa na malengo wanapouanza mwaka 2019 ili unapokwisha yatumike kama kipimo cha kujipima kama kama wanafifia au wanaimarika.

Aliwaasa waumini kuhakikisha wanaongozwa na imani safi, hai na thabiti kwa kumshirikisha Mungu kila jambo badala ya kumfanya kuwa Mungu wa mafanikio tu.

“Tunapoingia mwaka 2019, kwa wale unaokutana nao katika utendaji wako usiwe balaa, mzigo na kero kwao badala yake uwe baraka kwao,” alisema

MCHUNGAJI MALILO

Naye Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Alban, Mchungaji Meshack Malilo, aliwataka waumini wa dhehebu hilo kuhakikisha baraka wanazozipata wanazielekeza katika familia, kanisa na jamii zao ili kila mmoja wao aweze kuzifaidi.

“Kwa hiyo usiku huu tunapomaliza mwaka 2018, tuutumie kutafakari wapi tulikosea ili turekebishe. Kukosea kusitufanye kukata tamaa badala yake turekebishe pale tulipokosea kisha tusonge mbele,” alisema Mchungaji Malilo.

Wakati wa ibada za mkesha huo katika makanisa mbalimbali yaliyopo katika ya jiji zilitawaliwa na nyimbo za kusifu na kuabudu vilivyoambatana na shangwe.

 AZANIA FRONT

Kanisa la Kiinjili, Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Azania Front Dayosisi ya Mashariki na Pwani, lilitawaliwa na shangwe huku waumini wake wakionesha kuwa wenye furaha ya kuunza mwaka mpya.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Asia Kimaro alisema haikuwa kazi rahisi kuumaliza mwaka kutokana na vikwazo mbalimbali, lakini kwa mapenzi ya Mwenyezimungu hilo limewezekana.

“Mwanadamu wa kawaida unaweza kupanga mipango yako binafsi unayolenga kuifikia kwa mwaka mzima lakini bila kumweka Mungu mbele ni kazi bure maana yeye ndiyo aijuaye kesho yako,” alisema Asia.

Tofauti na miaka mingine ambayo kumekuwa kukishuhudiwa makundi makubwa ya watu mitaani wakisherehekea kuona mwaka mpya, mwaka huu hali ilikuwa tofauti katika maeneo mengi ya jiji ambayo ilikuwa na hali ya utulivu usio wa kawaida.

DORIA KILA KONA

Katika baadhi ya maeneo magari ya polisi yalionekana wakiimarisha doria kuhakikisha wananchi wanasherehekea vema mkesha huo.

Akizungumza wakati wa ibada ya mwaka mpya iliyofanyika jana, Mchungaji Chediel Lwiza ambaye ni Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), alisema kazi na mahangaiko ya kila siku yasiwe chanzo cha kusahau uwepo wa Mungu.

Alisema Watanzania wana uanza mwaka wakati watu wengi wakiwa wamevuka salama, wamepata mali lakini wamekosa baraka ya maisha kwa sababu hawakuwa na Mungu ndani yao.

“Ninawakumbusha kuwa mafanikio yetu tunayoyapata yasiwe sababu ya kuchukua nafasi ya Mungu. Mungu huyu aliye ndani yetu ndiye anayeona neema zenu zote, ndiye anayetoa baraka hata kwenye kazi zenu za kila siku,” alisema Mchungaji Lwiza.

Alisema wapo wanaowaza na kufikiri kuwa Mungu hayupo kwa kuona kuwa katika kutafuta kwao kila walichonacho ni wao wenyewe waliotumia nguvu na maarifa yao na kuondoa ile nafasi ya Mungu.

CUF NA SALAMU 2019

Chama cha Wananchi (CUF), kimetoa salamu za kuukaribisha mwaka 2019, huku wakitaka kurejeshwa kwa demokrasia nchini.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezo na Uhusiano wa Umma, Salim Bimani, ilisema mwaka 2018 ulikuwa na changamoto nyingi za kisiasa.

“Shukrani kwa mwenyezi Mungu kutuwezesha kuumaliza mwaka 2018 pamoja na changamoto kubwa za kisiasa na kidemokrasia zilizojitokeza. Tunamshukuru mola wetu mtukufu kwa kutuvusha salama na kutujaalia kuingia mwaka mpya wa 2019.

“Tunauanza mwaka mpya kwa Salamu za kheri na kuwakumbusha Watanzania kujua wajibu wao kwa Taifa katika kuheshimu, kulinda na kuitunza tunu ya amani,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,093FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles