26.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Lugola: Lissu arudi nchini apambane na kesi yake

JANETH MUSHI-ARUSHA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameendelea kulia na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), safari hii akitaka arejee nchini kuendelea na kesi yake na kuacha kumchafua Rais Dk. John Magufuli.

Katika mkutano wa Bunge uliopita, Lugola alitoa tena kauli kama hiyo akisema uchunguzi wa shambulizi la mbunge huyo, unamsubiri arejee nchini ili yeye na dereva wake wahojiwe.

Akizungumza jijini Arusha jana, Lugola alisema. “Kumekuwa na baadhi ya Watanzania wanachonganisha vyombo vya dola na wananchi, serikali na mataifa ya nje wengine wakimtukana Rais.

 “Nitoe mfano wa Mtanzania mmoja, Lissu amezaliwa, amekulia, amesomea, amefanya siasa yake Tanzania, amepigiwa kura na Watanzania waliomuamini, amekuwa mbunge, haiwezekani kutumia tatizo lililompata mwenzetu kuchafua nchi.

 “Kumtukana Rais, kuchonganisha nchi na mataifa ya nje kuwahimiza Watanzania kuchukia vyombo vya dola kwa sababu ya tatizo lililokupata, ni Watanzania wangapi wanapata matatizo?

“Nimwombe Lissu aje kwenye kesi yake, kwa sababu tunamwona afya yake inaimarika na dereva wake aje kwenye kesi, ili hayo mengi wanayosema waje watueleze tunapopeleleza, waache kuwaambia wazungu kwa sababu hawaendeshi wala kupeleleza kesi.

“Amepata nafuu arudi atoe ushirkiano tumalize kupeleleza kesi tusonge mbele na itakuwa kituko cha ajabu Polisi kumaliza upelelezi na kusema tumefunga wakati wahusika na mashahidi muhimu wanazurura, halafu tuwe na interest ya kupeleka kesi mahakamani,” alisema na kuongeza.

“Lissu ni mwongo asiendelee kuwaambia Watanzania uongo anawadanganya naomba nieleze majengo yote ya TBA Dodoma, hakuna jengo lililowekewa ulinzi CCTV camera, amebaki anadanganya ili ionekane Polisi wanaficha ushahidi.

“Anasema kulikuwa na Polisi, waliondolewa hakuna ambapo kuna ulinzi wa Jeshi la Polisi hakuna, ulinzi katika zile nyumba ni ulinzi wa kawaida uliopo wa kampuni binafsi, geti ambalo huwa liko wazi siku zote na walinzi wale hawana hata silaha,” alisema.

USALAMA WA LISSU

Akizungumzia hali ya usalama wa mbunge huyo pindi atakaporejea alisema usalama wa nchi ni usalama wa Watanzania wote na hivyo Lissu arejee kwani hakuna anayeratibu mpango wa kumdhuru.

“Nimhakikishie Lissu na ndiyo maana kila wakati nasema arejee, usalama wake upo kama kawaida yeye ni mbunge na sisi wabunge tulivyo na yeye pia ana enjoy hivyo hivyo, kwa hiyo arudi kwa sababu hakuna anayeratibu mpango wa kumdhuru, asiogope,” alisema Lugola.

WANASHERIA

Waziri huyo alishangazwa na baadhi ya wanasheria wanao mwunga mkono Lissu wakidai sheria ya kusaidiana kwenye mambo ya jinai (Mutual Assistance in Criminal Matters), inatakiwa kutumika kumhoji mbunge huyo na dereva wakiwa nje ya nchi ambapo alidai mazingira ya kesi hiyo ni tofauti na matumizi ya sheria hiyo.

“Natofautiana na baadhi ya wanasheria eti Polisi inaweza kuwahoji wakiwa huko wanakozurura,”alidai na kuongeza

“Lissu ndiye mlalamikaji wa kesi, inakuwaje mwenye kesi naye mpaka tuanze kulazimishana ili aje mwanzoni tulidhani ni mgonjwa akipata nafuu atakuja kwenye kesi yake, tumemshuhudia amepata nafuu kaanza uzembe na uzururaji,” alisema.

ULINZI NA USALAMA

Alisema hali ya usalama ipo shwari hivyo asitokee mtu wa kuwadanganya Watanzania kuwa  nchi haina amani wala usalama.

 “Sitarajii mtu mwenye akili timamu akapotosha Watanzania kuhusu suala la amani. Mtanzamia anayeweza kusema nchi haina amani huyo atakuwa muhuni, wahuni hawachagui maneno ya kusema, wanabwabwaja kwa hiyo tukisikia kitu kama hicho tunajua kimetoka kwa  muhuni na mhuni hupuuzwa.

 “Mtakumbuka Rwanda walianza kuchochea na kupotosha baadaye mambo yakawa makubwa nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani nina mpuuza mhuni lakini siwezi kupuuza maneno ya mhuni.

 “Anapotokea mtu muhuni tu anasema Serikali ya Dk.Magufuli inaua watu ni mambo ya ajabu inakuwaje Rais wa nchi awe na kazi ya kuua watu waliomchagua?

“Inakuwaje watu wanachonganisha vyombo vya usalama na wananchi kwamba vinaua watu, mpaka wanafikia hatua ya kutaja idadi, hii si sawasawa,” alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles