‘Kuna mbinu za kumng’oa Maalim Seif CUF’


GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti anayetambulika na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, unadaiwa kutaka kumwengua Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kupitia mkutano mkuu unaotarajia kufanyika Machi 12 hadi 15.

Kutokana na hali hiyo, upande unaomuunga mkono Maalim Seif umetoa onyo kwa wajumbe kutoka nje ya Dar es Salaam kutohudhuria mkutano huo na kudai wanachama wako tayari kukilinda chama chao kwa gharama yoyote.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Katibu Mkuu CUF Bara, Joran Bashange, katika ukumbi wa ofisi ya wabunge iliyopo Magomeni, ikiwa ni siku moja baada ya upande wa Lipumba kupitia Kaimu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya, kueleza kuwa bodi ya wadhamini wa CUF imepewa usajili na Wakala wa Usajili na Udhamini (Rita) baada ya kukidhi vigezo.

Bashange alisema Lipumba anayedaiwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, amepanga kumfukuza uanachama Maalim Seif na viongozi wenzake halali.

Alisema wameshapata taarifa za njama ya uitishwaji wa mkutano mkuu wa taifa feki wa Lipumba na genge lake, lakini Mei 9, mwaka jana yeye pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Nassor Ahmed Mazrui, walifungua shauri mama namba 84/2018 na shauri dogo namba 248/2018 kupinga kuitisha mkutano huo feki.

“Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Magoiga, Februari 28, mwaka huu ilitoa hukumu baada ya kuhitimisha kusikiliza shauri dogo namba 248/2018 na kutoa amri ya zuio, ikimzuia Lipumba na genge lake, wakala wao au yeyote anayefanya kazi chini yao kuitisha mkutano mkuu wa taifa kwa jina la CUF hadi shauri la msingi namba 84/2018 litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” alisema.

Pia alisema hata hivyo kwa jeuri na majivuno Lipumba na genge lake wameazimia kupuuza amri ya mahakama na kuamua kuendelea na mkutano mkuu wao uliotangazwa kufanyika Machi 12 hadi 15 katika Ukumbi wa Lekam uliopo Buguruni Malapa, Ilala Dar es Salaam.

Bashange alisema kwa mujibu wa taarifa ya Jaffari Mneke kupitia vyombo vya habari Machi 6, mwaka huu tayari Msajili wa Vyama vya Siasa alikwishawapatia fedha takriban Sh bilioni moja.

“Taarifa kutoka vyanzo sahihi zinaonyesha kuwa wameshaanza maandalizi yote ikiwemo uchapishaji wa fulana, kuchoresha mabegi ya mkutano huo na kuhakikishiwa ulinzi wa polisi,” alisema Bashange.

Alisema CUF  kwa kuheshimu sheria kimemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na kupeleka nakala kwa Rais, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, OCD Kituo cha Polisi Buguruni na jumuiya ya kimataifa kuwataarifu kusudio hilo la uvunjaji wa amri halali ya mahakama.

“Kwa hatua hizi tulizochukua tunaamini Mutungi, Lipumba na genge lake watatafakari upya kusuka au kunyoa,” alisema na kuongeza;

“Pia chama kinatoa wito na tahadhari kwa wale wote wanaojiita wajumbe wa mkutano mkuu huo feki wa Lipumba kutokuja Dar kwa makusudio hayo.

“Wanachama wa CUF Dar es Salaam na walinzi wake wote wa chama watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa wanakilinda chama kwa gharama yoyote na chama na viongozi wake havitawazuia kufanya lolote.”

Kuhusu usajili wa bodi hiyo uliofanywa na Rita, alisema mawakili wasomi wa chama hicho wako katika hatua za mwisho za kuwasilisha kesi mahakamani kuupinga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here