29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kijana abuni mbinu mpya kupambana na watawala wabaya

Na Markus Mpangala

MKUSANYIKO wowote wa watu unatengeneza fursa ambayo inawagusa moja kwa moja au kupitia njia mbadala. Mathalani watu wanapoandamana katika mtaa wowote upo uhakika wa kukutana na watu wanaouza maji ya kunywa kwa waandamanaji. Wengine wanauza bidhaa mbalimbali ili kuwezesha shughuli nzima.

Jijini Khartoum kumekuwa na maandamano makubwa kuanzia Januari mwaka jana hadi mwaka huu. Wananchi wa Sudan waliitikia wito wa kuandamana lengo likiwa kumng’oa madarakani Rais Omar Al Bashir.

Mafanikio ya waandamanaji hao ni uamuzi wa Jeshi la nchi hiyo kumtimua madarakani na kumweka chini ya ulinzi kiongozi huyo wa zamani. Vilevile mafanikio mengine ni kuibua nguvu ya umma yenye uwezo wa kumtetemesha kiongozi yeyote nchini humo, pamoja na kushuhudia namna wanawake wanavyoshiriki kuhamasisha maandamano hayo.

Kuibuka kwa Alaa Salah ni mfano mmojawapo wa mashujaa wanaoshiriki maandamano na kuhakikisha Sudan inakuwa na utawala wa kiraia. Ingawaje Jeshi la Sudan linaendelea kuongoza tangu kuanguka kwa Bashir hadi leo, lakini wananchi wanaendelea kuandamana kupinga hatua ya jeshi hilo kusalia madarakani. Wananchi na Chama cha wanataaluma  wanaamini kuwa ni wakati mwafaka kwa jeshi hilo kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

Katikati ya maandamano hayo limeibuka jina jingine la Abdirahman Moalim. Huyu ni miongoni mwa watu wanaoandamana na kuweka kambi nje ya Makao Makuu ya Jeshi  jijini Khartoum.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Al Jazeera, Abdirahman Moalim aliungana na maelfu ya wananchi wenzake kushinikiza Omar Al Bashir aachie ngazi. Moalim ambaye kitaaluma ni mkutubi aliona upungufu ambao unatakiwa kurekebishwa kwenye maandamano hayo. Jicho lake liliona zaidi ya maandamano yaliyoitikiwa na maelfu ya wananchi wakimtaka kiongozi huyo  aondoke madarakani.

“Niliona waandamanaji wengi ni vijana. Mahali wanapokaa karibu na makao ya Jeshi ili kushinikiza liachie ngazi walikuwa na simu za mikononi na walikuwa wanasoma kupitia hizo. Nilifikiria sana jambo hilo, kisha nikajiuliza, je haiwezekani nikawaletea vitabu ili wavisome na kuandelea na maandamano kwa wakati mmoja?” anasema Moalim ambaye anafahamika kwa jina la Kabila alipozungumza na Al Jazeera.

Moalim ‘Kabila’ anafanya kazi katika Maktaba ya Modern Kabo iliyopo jijini Khartoum, aligundua aina ya vitabu ambavyo vinapaswa kusomwa na waandamanaji.

“Wengi wanasoma vitabu vinavyohusu siasa na nguvu za madaraka. Hakuna anayesoma riwaya,” anasema Moalim ‘Kabila’ mwenye umri wa miaka 35.

Kijana huyo amefanya kazi ya ukutubi kwa kipindi cha miaka 14, anasema alishangazwa na kasi ya mabadiliko iliyotokea nchini Sudan.

“Katika maisha yangu namfahamu kiongozi mmoja tu. Ni kiongozi mbaya. Kutokana na vitabu tunavyosoma na kulinganisha na uongozi wa al Bashir, hakika umeathiri kiasi kikubwa maisha yetu kwa njia mbaya.” Anaongeza Moalim huku pembeni kukiwa na kundi la waandamanaji wakisoma vitabu.

Vitabu vingi hususani vile vinavyohusiana na mgogoro wa Jimbo la Darfur lilipo magharibi mwa Sudan na vingine kuhusiana na mapinduzi yaliyofanyika katika nchi mbalimbali duniani, yalikuwa magumu au kuonekana hayawezekani.

Moalim anaongeza kwa kusema, “watu wameathiriwa sana na uongozi mbaya. Walivyosoma vitabu hivyo wamebaini na kuumizwa hasa kinachotokea Sudan. Wanataka kuendelea kuhamasisha watu waandamane na kuwaondoa gizani,”

Maktaba hiyo ya wazi imesheheni vitabu mbalimbali ambavyo vimepangwa katika mstari. Waandamanaji wanachukua vitabu wanavyopenda na kusoma wakati wa kusimama au kutembea. Miongoni mwa waandamanaji ni Arif Abdala ameshindwa kukaa mbali na maktaba hiyo kutokana na uzuri wa vitabu ambavyo vinamwelimisha.

“Ni mara yangu ya kwanza kuwa hapa na nimepapenda sana. Kuna vitabu vingi vizuri vya kusoma. vingi sikuwahi kuvipata mwanzoni, hapa nimekata kiu yangu. Ingawa sifahamu nitakuwepo hapa kwa muda gani, lakini tayari nimekaa saa tatu sasa, nasoma kitabu cha rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, cha Long Walk to Freedom,” anasema Arifa Abdala mwenye umri wa miaka 27

Waandamanaji wanaokuja katika maktaba ya wazi ya Moalim Kabila mwanzoni hawakutarajia kuona kitu kama hicho, kwao kimewatoka kama ajali wakati wakiwa wanatembea maeneo yaliyopo karibu na makao makuu ya jeshi la nchi hiyo.

Rafaa Muhammad aliona habari za maktaba ya wazi katikati ya waandamanaji kupitia mitandao ya kijamii baada ya rafiki yake kuweka picha ya baadhi ya vitabu vinavyopatikana katika eneo hilo.

“Nipo hapa na rafiki zangu,  bado hatujaamua ni vitabu vya aina gani tuvisome. Nitapiga picha na kutuma kwenye mitandao ya kijamii ili vijana wengi wanapafahamu hapa na kutumia fursa hii kujielimisha. Hakika ni jambo la kuvutia sana,” anasema Rafaa Muhammad mwenye umri wa miaka 23.

Baadhi ya waandamanaji wamekuwa wakinunua vitabu hivyo na kwenda navyo nyumbani.

“Nilinunua kitabu kuhusu mgogoro wa jimbo la Darfur. Nimekuwa nikitafuta vitabu vya aina hiyo kwa miaka mingi. Nafahamiana na Moalim Kabila, hivyo nilimweleza mahitaji yangu, kuwa siwezi kuondoka eneo la maandamano bila kupata kitabu hicho. Nilimwambia nataka vitabu vingi ili nikahifadhi kwenye maktaba yangu nyumbani. Vitabu kama hivi awali ilikuwa vigumu kupatikana humu nchini. Tunavihitaji ili kuelewa nchi yetu kwa mapana. Tunatakiwa kufahamu kwa kina, tunamshukuru Moalim Kabila.” anasema Hassan Gasim.

Ili kuwavutia na kuhamasisha waandamanaji wajisomee vitabu vingi, Moalim Kabila hubadilisha aina ya vitabu kila siku. Mahitaji ya watu ni makubwa kwake, hivyo amelazimika kuwaomba marafiki zake wawili wajitolee kumsaidia kazi hiyo.

“Ninapenda anachofanya. Anaibua na kuhamasisha watu wapate taarifa sahihi. Ndiyo maana niliamua kuja hapa ili kumsaidia kuwaelimisha watu. Kila siku baada ya kumaliza kazi zangu ofisini saa tisa alasiri, huwa ninafika hapa kumsaidia Moalim hadi saa usiku.“ anasema Alfadil Alkhidir ambaye kitaaluma ni mhandisi wa umeme.

Kwa Kabila kuhamasisha watu kujisomea vitabu ni jambo ambalo siku zote amekuwa akitamani kufanya kwani ni chanzo cha maarifa na taarifa sahihi.

“Vijana wetu wanatakiwa kuhabarishwa na hakuna njia nzuri zaidi ya kusoma vitabu. Nataka kuona mabadiliko yanafanyika katika nchi yetu na hasa yatatokea kama tutakuwa na taarifa za kutosha kwa nia njema,”

Kijana huyo amekuwa chachu si kwa wananchi wa Sudan pekee bali baadhi yao maeneo mbalimbali barani Afrika. Moalim amekuwa gumzo kama alivyokuwa Alaa Salah, mwanamke aliyehamasisha zaidi waandamanaji kwa kuimba nyimbo za mapinduzi.

Moalim ametumia nyenzo ambayo haikupewa kipaumbele mwanzoni mwa maandamano, lakini sasa amekuwa gumzo zaidi na kuwafundisha watu wengi juu ya njia bora ya kupambana na viongozi wabaya kwenye nchi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles