28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Kesi ya kina Mbowe kuanza kusikilizwa Aprili 16


NA KULWA MZEEDAR ES SALAAM

KESI ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane imepangwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 16 na 17 mwaka huu.

Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini mshtakiwa wa tisa, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya hakuweza kufika mahakamani kwa sababu ya matatizo ya kiafya.

Nchimbi alidai wana mashahidi wawili lakini hawawezi kuendelea na ushahidi kwa sababu mshtakiwa Bulaya hayupo na hakuna barua ya kuruhusu kesi kuendelea.

Alidai misingi ya sheria inaelekeza ili kesi iendelee lazima mshtakiwa awe ameridhia kwa barua ama kiapo lakini Bulaya hajafanya hivyo.

Wakili Peter Kibatala akijibu aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji.

Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi, mahakama ilikubali kuahirisha kesi hadi Aprili 16 na 17 mwaka huu ambapo mashahidi watatoa ushahidi.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi ,  kula njama, kufanya maandamano isivyo halali, kuhamasisha chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali, tukio lililofanyika Februari 16 mwaka jana katika Viwanja vya Buibui, wilayani Kinondoni.

Pia washtakiwa wanadaiwa katika tarehe hiyo, barabara ya Kawawa, eneo la Mkwajuni washtakiwa wakiwa na wengine 12 ambao hawapo mahakamani, walikaidi agizo la SSP Gerald Thomas lililowakataza kufanya maandamano.

Washtakiwa wanadaiwa kuandamana walisababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na askari wengine wawili kujeruhiwa. Washtakiwa wote walikana mashtaka.

Mbali ya Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

- Advertisement -

Related Articles

Stay Connected

90,904FansLike
198,455FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles