20.8 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

JPM awataka mawaziri wawe wakali

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amewataka mawaziri na watendaji wake kuwa wakali katika kusimamia miradi ya maji ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua barabara ya Mafinga-Nyigo-Igawa yenye urefu wa kilomita 138.7 katika eneo la Mtewele na Uwanja wa Polisi mjini Makambako mkoani Njombe.

“Zinazungumzwa fedha zimeenda kwenye miradi lakini hazikwenda, nikuombe waziri na watendaji mkawe wakali kweli kweli, kama unaweza ukavuta bangi ya Njombe ili uwe mkali kaivute, kaivute kisiri siri wasikuone ukiivuta,” alisema Rais Magufuli.

Aidha aliwataka watu wanaosambaza pembejeo hewa kuacha mara moja kwani kufanya hivyo wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

“Nchi hii tumepoteza fedha nyingi sana kwa malipo ya ajabu ajabu, tulikuwa na wafanyakazi hewa 20,000 na wenye vyeti hewa 14,000 lakini kuna pembejeo hewa pia.

“Ninajua wapo ambao walikuwa na pembejeo za haki na tukishamaliza ufuatiliaji wa pembejeo watalipwa, Serikali ilikuwa inatoa fedha za kununua mbolea za mahindi halafu zinaenda kuuzwa nchi za jirani.

“Mtu anadai amesambaza magunia kadhaa ya pembejeo wakati hayapo, hatuwezi tukaendelea na nchi yenye hewa kwa sababu hatuwezi kushiba hewa.

“Nilipoingia madarakani niliahidi nitakuwa daktari wa kutumbua majipu zikiwemo hizi hewa ili fedha halali zitumike katika masuala mengine halali, ninajua wapo waliopata pembejeo za haki na tukishamaliza ufuatiliaji wa pembejeo watalipwa,” alisema.

Aliwapongeza wakazi wa mkoa huo kwa ujenzi mzuri wa nyumba, huku akiitaka mikoa mingine kuiga mfano huo kwa kujenga nyumba nzuri na za kisasa.

 “Tangu nimeingia Njombe nimeona nyumba zilizojengwa ni tofauti na nyumba zilizojengwa huko kwetu kwani hakuna nyumba ya majani, zote ni za bati na zimejengwa kwa matofali ya kuchoma, ninafikiri mikoa mingine ambayo haijabadilika katika ujenzi wa nyumba waje wajifunze huku,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia barabara hiyo, alisema ilikuwa imefikia mahali pabaya ikisababisha ajali nyingi.

 “Barabara hii ilikuwa imefikia mahali pabaya, ilikuwa inasababisha ajali nyingi, lakini pia ilikuwa nyembamba na magari yalikuwa ni mengi, barabara hii ni muhimu sana sio tu kwa Makambako bali kwa nchi nzima.

“Kukamilika kwa barabara hii kutachochea shughuli za kiuchumi, lakini pia nina imani wakazi wa Njombe mtatumia barabara hii kupitishia mazao yenu kwenda mikoa mingine na hata nje ya nchi,” alisema.

Alisema Benki ya Dunia (WB), imewakopesha fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambazo tayari Serikali imeshaanza kulipa.

 “Benki ya dunia wametukopesha hizi fedha tunazotakiwa kulipa na tumeshaanza kuzilipa, hivyo hauwezi kumkopesha mtu ambaye unajua hawezi kukurudishia, lakini sisi tumekuwa walipaji wazuri.

“Hata sisi tunapokopa hapa malipo yake hatutayamaliza kwenye awamu ya tano, inaweza ikalipwa hata awamu ya kumi, lakini barabara zitaendelea kujengwa ili tuweze kukuza uchumi wa nchi, hakuna nchi yoyote ambayo haikopi, hata Marekani wanakopa.

“Hatuwezi kukopa kwa ajili ya mishahara, semina na kongamano wala kwa ajili ya mimi kusafiri kwenda nje, bali tunakopa kwa ajili ya miradi ya kusaidia wananchi wa chini.

 “Mkoa wa Njombe kwa vyovyote unashiriki kulisha mikoa mingine kwa kiasi kikubwa ndiyo maana sikushangaa mbunge alivyokuwa akichomekea vinavyotakiwa kufanywa na kwakweli mbunge mmempata.

“Kuyapata maendeleo lazima nguvu kidogo iwepo maana hata kumpa mtoto yai au uji huku unambembeleza hawezi kunywa, lakini mpe kibao uone kama hajaumaliza muda huo huo, hivyo watendaji hakikisheni mnatumia nguvu katika kutekeleza ujenzi wa nchi.

 “Nitoe ombi kwenu, barabara hizi mzitunze kufanyia biashara zisiwe machinjio ya watu wengine bali zilete ukombozi wa wananchi wa kweli,” alisema.

Aidha alisema miradi ya maji iliyohakikiwa katika Wizara ya Fedha ni Sh bilioni 119, lakini kati ya hizo iliyokuwa ya kweli ni Sh bilioni 17 mengine yote yaliyobaki ni hewa.

Pia aliwataka wahandisi wote wa halmashauri za wilaya kuhamia Wizara ya Maji badala ya kukaa na kuzungumza miradi ambayo iko kwenye makaratasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles