23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awashika pabaya watumishi wa serikali

*Awataka warudishe fedha za tiketi za ndege, aagiza orodha yao

*Ampa Kapteni Mapunda donge nono kwa kutorosha ndege Kenya

WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KWA mara nyingine tena Rais Dk. John Magufuli, ameandika histori mpya kwa Tanzania baada ya kupokea ndege kubwa ya kisasa aina ya Airbus A220 – 300.

Wakati akiandika historia hiyo, Rais Magufuli, ameagiza watendaji wa serikali takribani 100 ambao walikatiwa tiketi katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), lakini hawakusafiri warejeshe fedha hizo haraka.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kupokea ndege mpya ya Airbus A220 – 300 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakikatiwa tiketi kwa fedha za serikali bila kusafiri na kuisababishia hasara serikali.

“Baadhi ya tiketi zinakatwa na watendaji wa serikali halafu hawasafiri matokeo yake ndege inakwenda tupu. Niletewe orodha yote ya watendaji wa serikali ambao hawakusafiri ili tuwakate hizo fedha kwenye mishahara yao. Nina uhakika kufika wiki ijayo nitapata majina yao.

“Ndege inakwenda tupu na fedha ya serikali imetumika… nina uhakika kufika kesho majina nitakuwa nimeyapata yote. Ambao hawakusafiri na walikatiwa tiketi kwa fedha za serikali wajiandae kurudisha fedha ili kusudi mambo yaishe,” alisema Rais Magufuli.

HUJUMA KWENYE TIKETI

Rais Magufuli alisema pia wamebaini kuwapo kwa hujuma katika ukatishaji tiketi na malalamiko kuhusu huduma za shirika hilo.

“Tiketi zinazotolewa na mawakala zinauzwa kwa bei ya chini kuliko zinazotolewa na shirika. Wanaotaka kusafiri na ndege wanaambiwa imejaa lakini wanapoingia ndani inakuwa haijajaa.

“Baadhi ya makawala wanatumia kadi za benki kukata tiketi, kugushi kwa kutumia kadi za watu wengine. Naambiwa wako polisi washughulikiwe kwa sababu ndio wanahatarisha juhudi za kujenga uchumi wa Watanzania,” alisema.

Aliwataka wafanyakazi wa shirika hilo walinde dhamana ya Watanzania katika kutunza ndege hizo.

“Shirika hili lilikuwa limepotea, nitasikitika kama bodi na menejimenti ya ATCL watajisahau na kuturudisha tena kule tulikotoka, itakuwa ni aibu kwa Watanzania wote.

“ATCL wameazimwa ni ndege za Serikali, zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi, wasipozalisha tunawanyang’anya, vya kupewapewa bure watu wanasahau.

“Tutaendelea kuwabana watendaji ambao wanafikiri kila kitu ni sikukuu. Hakikisheni hizi ndege zinaendelea kuzalisha, mwelekeo uwe wa kufanya biashara na si kufanyiwa biashara,” alisema.

Rais Magufuli alisema usafiri wa anga ni huduma na ni biashara yenye faida hivyo aliwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na kuboresha huduma.

UNUNUZI WA NDEGE

Rais Magufuli alisema malengo ni kununua ndege mpya nane na hadi sasa zimewasili tano na nyingine zitawasili mwakani. 

Alisema tangu ndege hizo zianze kufanya kazi tayari zimeingiza faida ya Sh bilioni 28.

“Kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM (2015 – 2020) ukurasa wa 46 hadi wa 71 tuliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri wa barabara, reli, maji na anga.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumetekeleza ahadi hiyo kwa vitendo,” alisema.

Alisema usafiri wa anga ni salama, haraka na wa uhakika hivyo, umekuwa kichocheo kikubwa cha shughuli za kiuchumi na ukuaji wa biashara ya utalii.

Alifafanua kuwa ripoti ya mwaka 2017 inaonyesha watu bilioni 4 walisafiri kwa ndege duniani na watalii walikuwa bilioni 1.3.

Alisema shughuli za usafiri na utalii zilitoa ajira milioni 13.2 na mapato ya moja kwa moja yalikuwa dola trilioni 2.57 na mapato ya jumla yalikuwa dola trilioni 8.27.

“Nchi yetu inasifika kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii lakni idadi ya watalii waliongia nchini bado ni ndogo, mwaka 2017 tulipata watalii milioni 1.3. Kwa nchi ya pili duniani kuwa na vivutio hatukutakiwa tuwe na watalii wachache wanaokuja kutembelea,” alisema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mapato ya utalii mwaka jana yalikuwa dola bilioni 2.3 na watu waliosafiri kwa anga walikuwa milioni 3.4 tu na kwamba sababu kubwa ilichangiwa na nchi kutokuwa na ndege zake yenyewe.

Alisema pia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kitaimarishwa na karakana ya matengenezo ya ndege iliyopo KIA itafufuliwa.

“Kama tumeweza kununua bombadier hatuwezi tukashindwa vindege vidogo vidogo vya kufundishia.

“Matamanio yangu ni kwamba siku moja na sisi tufike kiwango cha kufanya matengenezo ya ndege, kama tuna anga kubwa kuliko mengine Afrika kwanini tushindwe,” alisema.

KAPTENI MAPUNDA

Rubani wa kwanza kuendesha ndege za ATC, Mapunda, jana alitambuliwa katika hafla hiyo na kupongezwa kwa uzalendo wake wa kuitorosha ndege iliyokuwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo.

Rais Magufuli alimkabdhi fedha taslimu Sh milioni 10 na akaliagiza ATC kwamba Mapunda na mkewe wawe wanasafiri bure.

“Inawezekana hatukumtambua kwa miaka mingi, ndugu Mapunda njoo hapa (akamuita mbele ya umati), Mapunda oyee, fagilia Mapunda.

“Huyu baba ali – risk (alihatarisha) maisha yake kwa ajili ya Tanzania, kila atakapokuwa anaingia kwenye ndege ya ATC asilipe tiketi yeye na mke wake…ila nawewe Mzee Mapunda usiwe unasafiri kila siku,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema Mapunda ana historia ya uzalendo kwani baada ya EAC kuvunjika ilitolewa amri ndege zote ziegeshwe Nairobi lakini mzee huyo aliileta Dar es Salaam.

“Alijifanya kama anaegesha halafu akairusha ndege akaileta hadi Dar es Salaam, hakujali kama atapigwa mizinga na kudondoka. Aliweka Utanzania wake mbele na hiyo ndege aliyokuja nayo ndio ikawa ya kwanza tukaanzisha shirika la ndege na ilipofika huku wala haikurudi tena kule,” alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania wajifunze kuwa uzalendo kama mzee Mapunda kwani ndege hizo ni zao.

“Tunanunua ndege tuaambiwa hazitakuja, mara mkweche, hazikimbii sana, kuna mmoja alisema hazikimbii sana nikamwambia kapande za jeshi hakuzungumza tena…kikubwa ninawaomba Watanzania tuwe wazalendo,” alisema.

Aliahidi kumkaribisha nchini Makamu wa Rais wa Air Bus na uongozi wa Canada kwa ushirikiano wao uliowezesha kwenda kutengeneza ndege nchini humo.

Naye Balozi wa Canada, alimuhakikishia Rais Magufuli kuwa mahusiano kati ya Tanzania na Canada yataendelea kuimarishwa.

SPIKA WA BUNGE

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Watanzania wanaweza endapo watathubutu kwa kuwa si wengi ambao waliamini kwamba rais ataweza kufanya anachofanya hasa katika kuhakikisha shirika la ndege linasimama na mapato yanaongezeka.

“Watanzania tunaweza tukithubutu si wengi ambao tuliamini hili na hii imedhihirisha kuwa Watanzania wanaweza. Hili limetujengea uwezo na fikra ya kujiamini hata endapo tutaona Twiga anaruka tunaona fahari kuwa Watanzania tunaweza,’’alisema Ndugai.

Alisema Bodi ya ATCL inatakiwa kufanya kazi kwa saa 24 na isiwe kama ile iliyopita kutokana na mapato yake kushuka siku hadi siku na kusema kuwa anaamini katika utawala wa Rais Magufuli hilo halitatokea.

Ndugai aliwataka Watanzania kuwa wazalendo kwa kutumia ndege za ATCL kabla ya kufikiria kupanda ndege nyingine.

KATIBU MKUU KIONGOZI

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, alisema ndege inayopokelewa ni matokeo ya utekelezaji ya uongozi wa rais na kwamba ni ya kisasa ya masafa ya kati na katika Bara la Afrika Tanzania ndio ya kwanza kuwa nayo.

“Katika Bara la Afrika Tanzania ni ya kwanza kuwa na ndege kama hiyo hivyo, tunaweka historia kwa kufungua Airbus 220 – 300  itakabidhiwa kwa ATCL kuweza kuiendesha kibiashara na kuhakikisha kuwa gharama zinarudi na kupata faida itakayotumika kununua ndege nyingine zaidi.

“Niwahakikishie tu mwaka Januari 2019 kutakuwa na ndege nyingine kama hiyo hivyo, kufanya ATCL kuwa na ndege sita za kisasa na kuongeza idadi ya ndege ya masafa marefu na ya kati,” alisema Balozi Kijazi.

Alisema uwekezaji huo umeanza kutoa matokeo chanya kutokana na kuongezeka kwa mtandao na kuimarika usafiri wa anga kwa safari za ndani na nje.

Alisema kutokana na ushindani huo nauli za ndege zimekuwa nafuu na hazipandi mara kwa mara kama ilivyokuwa awali.

WAZIRI WA UCHUKUZI

Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwele, alisema ATCL imefufuka kutokana na Serikali ya CCM inavyofanya kazi.

Waziri aliahidi kujengwa Uwanja wa Ndege wa Songea sambamba na kufanya matengenezo ya ndege hizo ambapo ndege moja inagharimu dola milioni tatu huku akimuahidi Rais kuwa watasimama na kujitegemea wenyewe hasa kwa kuanza na ukarabati wa hanga.

Alisema maspema mwakani ndege mbili za mwanzo znatakiwa kwenda matengenezo ya kawaida kwa mujibu wa utaratibu.

MAKONDA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema ununuzi wa ndege hizo ni matokeo ya Watanzania kulipa kodi na kwamba ni wakati mwafaka kwa kila Mtanzania kufanya hivyo.

Alisema Rais ameweza kufanikisha kusimamia na kuziba mianya ya rushwa na kuongeza uadilifu hatua iliyoongeza mafanikio hayo.

KUHUSU AIRBUS A220-300

Ni ndege yenye urefu wa mita 38.7 na kwa jumla inaweza kuketi abiria 141.

Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5  na upana wa mabawa yake ni mita 35.1.

Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa 5,920 km safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.

A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za kubwa za A220 na iliundwa kulenga soko la safai za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.

Ni ndege ambayo imeundwa kupunguza gharama ya matumizi yake ya mafuta kwa kila safari na pia ina uwezo wa juu.

Injini zake zimepunguza matumizi ya mafuta kwa kila abiria kwa asilimia 20 ukilinganisha na ndege za awali za aina hiyo.

Ndege za A220 zimejengwa kwa vipande vinavyoweza kutengenezwa kwa haraka kiwandani iwapo vitahitajika wakati wa ukarabati.

Injini zake pia huwa za aina moja moja. Marubani waliozoea ndege aina ya A220-300 na A220-100 hawahitaji mafunzo zaidi kuweza kuziendesha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles