24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ampongeza Hakimu Mbeya, amkumbuka Kandoro

Anna Potinus – Dar es Saalam

Rais Dk John Magufuli amekemea vikali vitendo vya ubakaji vinavyoendelea Mkoani Mbeya, amewataka viongozi na wananchi kushirikiana kwa pamoja kutokomeza tatizo hilo kwa kuwachukulia hatua wanaohusika na vitendo hivyo.

Ametoa kauli hiyo Jumamosi Aprili 27, wakati akizungumza na Wananchi wa wilaya ya Chunya mkoani humo katika ziara yake ya kikazi ya siku nane ambapo ameshazindua barabara ya Mbeya – Chunya yenye urefu wa kilomita 72 na kuweka Jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Chunya – Makongorosi.

Dk Magufuli amewataka viongozi hao kuiga mfano wa marehemu Abbas Kandoro kwa namna alivyosaidia kwenye hukumu ya mwanaume aliyehukumiwa kifungo cha maisha kutokana na kupatika ana hatia ya kulawiti mtoto ambaye hadi sasa yupo katika hali mbaya.

“Tatizo la ubakaji linaonekana linataka kuwa ugonjwa katika maeneo haya, jana kuna mama alijitokeza katika mkutano wetu akaeleza shida yake kwamba ana mtoto wake ambaye alilawitiwa akiwa na miaka sita kukawa na ujanja ujanja na baadaye alienda kumuona aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro akaishughulikia kesi hiyo vizuri na hakimu akatumia sheria zote na mtuhumiwa akahukumiwa kifungo cha maisha,” amesema.

“Nitoe wito kwa viongozi kuiga mfano wa Mzee kandoro maana alisimamia haki popote palipokuwa hakuna haki, hivyo yeyote atakayefanya vitendo vya ajabu apelekwe kwenye vyombo vya dola na nina imani tukilisimamia hili kwa pamoja tutazaa matunda mazuri,” amesema.

Aidha ametoa agizo kwa viongozi mkoani huo kuhakikisha wanafungua soko la madini katika Wilaya ya Chunya ndani ya siku saba na kwamba hilo ndilo litakuwa jaribio lao kubwa licha ya kuwa na utendaji mzuri mkoani humo.

“Kama Mkuu wa Mkoa wa Geita ameweza kufungua soko la madini wakuu wa mikoa mingine mnashindwa nini? Tunatoa mateso kwa wananchi hawa mkuu wa mkoa na viongozi wengine hili ndilo jaribio lenu na mnalipwa kwa wakati, magari mnayo sasa ndani ya siku saba mjipange wenyewe ili wananchi hawa wachimba dhahabu wapate maeneo ya kuuzia dhahabu zao,” amesema.

“Nilichaguliwa kusema ukweli na hili agizo sio la mkuu wa mkoa wa Mbeya peke yake siwezi kuwa na wakuu wa Mikoa ambao ninatoa agizo halafu hawatekelezi hawa wananchi ndio walionichagua mvua zikiwa zinanyesha, jua linawaka wakaniambia nikafunge makufuli yote hivyo achana na hizo dhambi za kutamani, kamilisha kwanza hili la kuanzisha soko hapa ndio ukatamani halafu ukimaliza ukatubu dhambi zako,” amesema Dk Magufuli huku wengi wakiangua kicheko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles