28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Jicho la tatu limulikwe zaidi kwa waamuzi wa soka Tanzania

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

WAAMUZI wa soka wamekuwa wakilalamikiwa kwa maamuzi mabovu wanayoyafanya uwanjani katika michezo mbalimbali wanayoiendesha.

Hongera Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwaondoa kwenye orodha ya  waamuzi msimu huu, waamuzi Abdallah Kambuzi, Godfrey Msakila na Consolata Lazaro.

Waamuzi hao wamefungashiwa virago baada ya kuonekana kuwa wakishindwa kutafsiri vema sheria za soka katika mchezo kati ya KMC na Simba SC, uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza  Aprili 25, mwaka huu.

Hatua iliyochukuliwa na TFF huenda ikaanza kurudisha matumaini kwa Watanzania wengi ambao wamekuwa wakilalamika waamuzi kufanya makosa na kutopewa adhabu zozote.

Waamuzi wamekuwa wakibeba dhamana ya kuchezea mechi, lakini wengine hushindwa kufanyia kazi maelekezo yote waliyojifunza kuhakikisha wanaboresha kazi zao.

Tanzania imekuwa ikiandamwa na matukio  mengi ya waamuzi kushindwa kutumia vema nafasi zao uwanjani, wengine kujikuta wakiingia kwenye mkumbo wa kupokea rushwa ili kuonyesha upendeleo kwa timu flani.

Waamuzi ndio wanaobeba mchezo mzima uwanjani na pindi wanapojikuta wanashindwa kufanya kazi zao kwa usahihi, kwa namna moja au nyingine lazima waondolewe.

TFF inapaswa kuwa makini zaidi kwani waamuzi wengi wamekuwa wakikosea, hasa kwenye ligi nyingine kama Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.

Ligi za chini ndiyo zimefunikwa na sheria za ovyo zinazofanywa na waaamuzi wanaosimamia, jambo ambalo limekuwa likipelekea wachezaji, mashabiki kujichukulia maamuzi yao binafsi kutafuta haki.

Waamuzi mnapaswa kubadilika, kujifunza kutokana na makosa yaliyofanywa na wengine, soka ni sehemu ya burudani na ajira kwa wachezaji.

Muhimu kila mmoja akatimiza majukumu yake bila kuonyesha upendeleo wa aina yoyote, hasa kipindi ambacho timu zinakuwa zinamalizia michezo yake ya mwisho kusaka nafasi ya kupanda daraja au kusaka ubingwa.

Matukio ya rushwa yamekuwa yakipigiwa kelele mara kwa mara, kwani hupelekea morali ya wachezaji kushuka na kushindwa kujituma, inachosha kujiandaa na kukuta tayari matokeo yameshaandaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles