30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 9, 2022

Jeshi la Sudan lageukwa, lakaribisha mazungumzo

KHARTOUM, SUDAN

IKIWA ni siku moja tu tangu Jeshi la Sudan kumwondoa Rais Omar al Bashir madarakani, maelfu ya waandamanaji wameweka kambi nje ya Wizara ya Ulinzi mjini Khartoum kushinikiza iundwe serikali ya kiraia, na kukaidi amri iliyotolewa na baraza la mpito la kijeshi ya kutotoka nje usiku, pamoja na kuyapatia mwaliko wa mazungumzo makundi ya kisiasa kwa madhumuni ya kurejesha utulivu nchini humo.

Vyombo vya habari nchini Sudan vimeripoti kuwa, waandamanaji hao ambao wamekuwa wakiandamana karibu kila siku kuipinga serikali ya Omar al-Bashir, ambaye ameitawala Sudan kwa miaka 30, wameukataa uamuzi wa kuanzishwa kwa baraza la mpito la kijeshi ambalo limetangaza kuitawala nchi hiyo kwa miaka miwili na wameahidi kuendelea na maandamano hadi serikali ya kiraia itakapowekwa madarakani.

Kundi la wanaharakati nchini humo, jana liliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi nje ya Wizara ya Ulinzi, eneo kuu ambako maandamano yamekuwa yakifanyika. Mahema makubwa yamewekwa katika eneo hilo na watu wameleta vyakula na kugawa maji kwa umati mkubwa mahali hapo.

Ahmed al-Sedek, mwenye umri wa miaka 39, ambaye ni miongoni mwa waandamanaji, amesema hajalala nyumbani kwake tangu walipoanza kuweka kambi nje ya makao makuu ya jeshi wiki iliyopita.

Chama cha upinzani cha Congress kimeshauri kuanzishwa kwa baraza la pamoja la kijeshi na kiraia ili kutawala katika kipindi cha mpito cha miaka minne. Pia kimelitaka jeshi kukabidhi mamlaka kwa raia.

Katika hatua nyingine, Baraza la mpito la kijeshi limetangaza mipango ya ya kuanza mazungumzo na makundi ya kisiasa kuanzia jana ili kutafuta mwafaka wa kuongoza taifa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Kamati ya Kijeshi na Kisiasa, Omar Zein al Abidin, ambaye ameteuliwa na Rais wa Baraza la Mpito la Kijeshi, Mohammed Ahmed Awad Ibn Auf, amesema wanataka kujenga mazingira ya kufanyika mazungumzo na kwamba jeshi peke yake halina suluhisho katika mzozo wa Sudan, bali ushirikiano unawahusu waandamanaji.

“Baraza letu linawajumuisha Mkuu wa Polisi, Mkuu wa Usalama na Kamanda wa Vikosi vya Jeshi, na hatutalazimisha kitu chochote kwa wananchi. Tunatarajia kuwa kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka miwili, ingawa kinaweza kuwa kifupi hata kwa mwezi mmoja, iwapo mambo yatatatuliwa bila ghasia,” amesema Zein al Abidin.

Mataifa yenye nguvu duniani, ikiwamo Marekani na Uingereza, yamelitolea wito jeshi kuwaachia raia kuamua kiongozi wanayemtaka kuwaongoza na kwamba miaka miwili ni mingi kwa jeshi hilo kutawala. Mataifa hayo yamesema yanaunga mkono kipindi cha mpito cha amani na demokrasia mapema zaidi ya miaka miwili.

Umoja wa Ulaya nao umelisihi jeshi kukabidhi haraka madaraka kwa utawala wa kiraia na kuwepo hali ya utulivu. Hata hivyo, Umoja wa Afrika umelaani njia iliyotumika kumwondoa Bashir madarakani, ukisema haikuwa sahihi katika kuzitatua changamoto zinazowakabili watu wa Sudan pamoja na matakwa yao.

Kiongozi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ameitaka Sudan kulinda haki za binadamu na kujizuia na ghasia. Bachelet amewasihi viongozi wa Sudan kuwaachia huru watu waliokamatwa kutokana na kuandamana kwa amani na kuchunguza matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji ambao walianza kuandamana tangu Desemba mwaka jana. Amebainisha kuwa Sudan inakabiliwa na kipindi muhimu na tete na hakuna uhakika kuhusu mustakabali wake.

Ama kwa upande mwingine, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka Serikali ya Sudan kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ambayo awali ilitoa waranti wa kukamatwa Rais Bashir kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,291FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles