30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu ataka Mashauri ya mirathi yamalizike kwa wakati

Lydia Churi-Mahakama, Mtwara

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma, ameagiza kupelekewa mashauri yote ya mirathi ili aweze kujua ni changamoto zipi zinazofanya yachelewe kumalizika kwa wakati.

Akizungumza katika ziara yake ya mkoani hapa, Profesa Juma alisema katika mahakama za mwanzo mashauri hayo yanatakiwa kuisha ndani ya miezi sita, lakini yapo mengine yamekaa zaidi ya miaka kumi.

Alisema kutokana na kuchelewa kumalizika kwa mashauri hayo, wakati mwingine humfanya msimamizi wa mirathi kuendelea kunufaika na mali za marehemu wakati warithi wapo na wanataabika kwa muda mrefu.

“Nimetoa agizo hili kwa kuwa mashauri ya aina hii huweza kuzalisha migogoro mingi katika jamii na kusababisha haki za watu kutokupatikana kwa wakati,” alisema.

Akizungumzia changamoto nyingine zinazoikabili Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki, Prof. Juma alisema mahakama inakabiliwa na changamoto kubwa ya wananchi kutofahamu taratibu za kisheria jambo linalosababisha washindwe kupata haki zao.

Alisema hivi sasa Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu za kisheria kabla ya kesi kuanza kusikilizwa mahakamani ili kuwasaidia wananchi kutambua nini cha kufanya.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama imeamua kuwa wazi katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni moja ya hatua muhimu za mapambano dhidi ya rushwa katika muhimili huo.

Awali akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, Jaji Mkuu aliwaomba wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na mahakama katika kuwaelimisha wananchi taratibu za mchakato wa upatikanaji wa haki.

Alisema mahakama inachangia utulivu na amani katika nchi pale inapotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki kwa wakati na endepo mahakama haitafanya kazi yake vizuri ni wazi amani hiyo itatoweka.

Wakati huo huo, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Solanus Nyimbi, alisema ili kutatua changamoto ya uchakavu na ukosefu wa miundombinu ya mahakama hususan majengo, muhimili huo umeandaa mpango kabambe wa ujenzi uliozingatia maeneo yanayotakiwa kujengwa majengo mapya ya mahakama.

Alisema hivi sasa majengo yanayoendelea kujengwa ni pamoja na mahakama za mwanzo 22, mahakama za wilaya 20, mahakama za mikoa (Hakimu Mkazi) 8 pamoja na mahakama kuu 2, zinazojengwa katika mikoa ya Mara na Kigoma.

Alisema Wilaya ya Tandahimba nayo iko kwenye mpango wa kupatiwa jengo litakalojumuisha mahakama ya wilaya pamoja na mahakama moja ya mwanzo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles