23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu ampongeza aliyekataa kusajili kesi ya Zitto

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, amemsifu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, S.S. Sarwatt, aliyekataa kusajili maombi ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, akipinga uamuzi wake wa kumwita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhojiwa katika Kamati ya Bunge.

Pia alisema wasajili hawatakiwi kusajili kesi yenye makosa na kuikataa kesi kama ile ni ujasiri unaotakiwa kufanywa na wasajili wote.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya wiki ya elimu ya sheria itakayofanyika kitaifa Dodoma kuanzia Januari 31, mwaka huu katika Viwanja vya Nyerere Square pia matembezi ya hisani yatafanyika Februari 2, mwaka huu yakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na siku ya sheria itafanyika Februari 6, mwaka huu katika Viwanja vya Chimala, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Rais Dk. John Magufuli.

“Kulikuwa na malalamiko kwamba Mahakama ya Rufaa inazitupa kesi zenye makosa ya kiufundi, sheria ikatungwa, mabadiliko yaliyopo sasa wasajili wasisajili kesi yenye makosa.

“Namsifu msajili aliyekataa kusajili kesi yenye makosa kama ile, ule ni ujasiri, majaji wote wanatakiwa kufanya hivyo,” alisema.

Pia alisema mahakama haiwezi kuwazuia wanasiasa kuzungumza kuhusu mahakama kwamba haiko huru kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao lakini yenyewe haijibu inafanya kazi kimya kimya.

Jaji Ibrahimu alisema mahakama iko wazi na kila kitu kinapimika, hakuna kinachofichwa na kama kuna mtu hajapata huduma bora au umeona maadili yamekiukwa namba zimeweka kila kona katika kuta za mahakamani ili apige Takukuru.

“Nenda Takukuru, kama rushwa ina jina la mtu, hatupendezwi na malalamiko ya jumla,” alisema.

Kuhusu wiki ya sheria alisema elimu itatolewa kwa wananchi na aliwaomba wafike kwa wingi katika viwanja vya Nyerere, Dodoma na Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Pia alisema wale wanaopita na mabango ya malalamiko siku ya sheria wanatakiwa kufika na malalamiko hayo katika wiki ya sheria kwa sababu muda unakuwepo wa kuyasikiliza na kupata ufumbuzi kuliko siku ya sheria muda hautoshi.

Alisema ni ukweli kwamba, mahakama haiwezi kufanya kazi bila ushirikiano wa wadau wakiwemo Magereza kwa kuleta watuhumiwa mahakamani, mashahidi kufika, mawakili na wengine.

“Nguvu yetu ni wananchi, tukiweza kuwaridhisha kwa asilimia 70, kuhakikisha wanapata haki tutakuwa tumepiga hatua kwelikweli, tukijenga imani kwa wananchi huko katika twitter tutakwenda pamoja,” alisema.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Feleshi, alisema suala la uhaba wa majaji linashughulikiwa na mamlaka ya juu kwa sababu mahakama ilishatimiza wajibu wake.

Alisema mafanikio makubwa yalipatikana mwaka jana kwa kupunguza mlundikano wa kesi na kufikia mwakani kipindi kama hiki kesi zitakuwa zimepungua zaidi.

Jaji Feleshi alisema mashauri ya muda mrefu yako kwa asilimia 20 na asilimia 80 yako ndani ya muda unaotakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles